JINA LA SIMULIZI............................LISA
AUTHOR...........................JOMBA WAJO
SPONSORED BY......SIMULIZI ZA DULLY
WHATSAPP...........................0628924768
SEHEMU YA................................301-302
Sura ya: 301
Lisa alikuwa ametoka tu kumpumzisha Pamela wakati Sarah alipokimbilia wodini na kupiga magoti chini, akiegemea kitanda alicholala Pamela huku macho yake yakiwa yamezama kwenye dimbwi la machozi. “Lisa, Bi. Masanja, samahanini. Naomba msamaha kwenu kwa niaba ya kaka yangu.”
Sarah aliinamisha kichwa chini kwa nguvu na paji la uso wake liligonga chini kwa nguvu, na punde, likawa limevimba.
Mara Alvin naye akaingia. Baada ya kuona tukio hilo, mara moja alimvuta Sarah na kumyanyua.“Sarah, inuka.”
Hata hivyo, Sara alikataa kuinuka. Alisema katikati ya kwikwi, “Alvinic, usinizuie. Ni kosa la kaka yangu…”
"Inatosha. Uso wako umetoka kuumia juzijuzi tu, kwanini unauumiza tena kwa kuubamiza chini? Sitakuruhusu upige magoti,” Alvin aliamuru kwa nguvu.
"Alvinic, si sahihi alichokifanya kaka yangu kwa Bi. Masanja. Hata kama kichwa changu kitapasuka, ni sawa tu mradi amsamehe...” Sarah alimshika mkono na ghafla akajitupa mikononi mwake. "Alvinic, ninamuonea huruma sana."
“Usilie.” Alvin aliinamisha kichwa chini na kumshika.
Wakati huo huo, Lisa alisimama tu kando akiwa kimya na kutazama tukio hilo likiendelea. Mumewe alikuwa amemshika mwanamke mwingine aliyemchukia na kumwonyesha mapenzi mazito mbele yake. Alikuwa amekufa ganzi kabisa. Kwake, ilikuwa kama anatazama kichekesho cha Futuhi tu. Alipochoka na kuchoshwa nayo, alisema kwa upole, “Je, show imekamilika? Kama mmemaliza ondokeni tafadhari. Ni usiku wa manane, na mgonjwa anahitaji kupumzika.”
Alvin alikunja uso, lakini Sarah alimsukuma kando na kusema huku akitokwa na machozi, “Nipo hapa kuomba msamaha kwa dhati. Natumaini unaweza kumsamehe kaka yangu, nakuomba sana. Nitakubali masharti yoyote utakayotoa, hata… hata kama utataka nimwache Alvinic.”
“Sarah…” Uso mzuri wa Alvin ukazama. Alionyesha kuwa na hasira kali. “Unawezaje kusema hivyo? Ina maana hunipendi?”
"Hapana, Alvinic. Ninakupenda sana.” Sarah akasonga. “Lakini sina jinsi. Nahitaji tu msamaha wa kaka yangu kwa gharama yoyote, lakini upendo wangu kwako hautabadilika kamwe. Siku zote nitakupenda hata kama…”
“Nyamaza, huwezi kufanya hivyo.” Alvin akamkatisha. Kulikuwa na hisia ya kina ya mapenzi machoni pake. “Usiseme hivyo tena. Niachie mimi jambo hili.”
"Kweli Alvinic?" Sarah na Alvin walitazamana kwa upendo.
Akiwatazama, Lisa alihisi kama yeye ndiye mvamizi tu katika uhusiano huo. Hata hivyo, ni yeye mwenyewe tu ndiye aliyejua kwamba wakati mwingine moyo wa mtu unaweza kufa ganzi kiasi cha kutosikia maumivu yoyote. Alichohisi ni kitu kikimjia kooni. Haraka alilikimbilia pipa la taka na kuliachamia. Alichukizwa sana hadi akajisikia kutapika.
Lisa alikuwa hajawahi kutapika kiasi hicho hapo awali. Alitapika kuanzia chakula chote alichokula hadi nyongo yote, na machozi yakatoka. Alijua kwamba lazima Alvin alikuwa akimchukia sana, lakini hakuwa na la kufanya kurejesha upendo wake uliopokonywa kwa njia za hila.
"Uko salama?" Akiwa amekunja uso, Alvin alimtazama kwa mshtuko. Sarah kwa haraka akachukua rundo la tishu na kumkabidhi pia.
Lisa aliutoa tu mkono wake na kucheka kidogo huku mwili wake ukiwa umeinama. “Niko sawa, bila shaka. Nilitapika kwa sababu nilichukizwa nanyi, enyi wapenzi msio na haya.”
Uso wa Alvin ulibadilika sana. "Lisa Jones, bora uchunge mdomo wako."
“Nimesema kitu kibaya?” Lisa alitazama juu huku macho yakiwa yana machozi. Sarah, ulikuja hapa kuomba msamaha au kunifanyia show?” Kisha akamgeukia Alvin na kusema, “najua hunipendi, lakini kisheria, mimi bado ni mke wako. Huwezi kunionyeshea dharau na mchepuko wako kiasi hiki.” Alimtazama tena Sarah. “Kwa upande wako, umekuwa ukilia na kupiga magoti kuomba msamaha tangu ulipoingia mlangoni. Nilikuambia upige magoti? Unafikiri tunaweza kupuuzia kila kitu kilichotokea kwa sababu tu ulipiga magoti? Alichokifanya Thomas ni uhalifu. Alimchoma kisu na kumshambulia , na kumtilia Pamela dawa za kulevya, na pia kufanya uhalifu mwingine mwingi tu. Unafikiri kupiga magoti na kusema maneno machche tu kama samahani kunaweza kutatua yote? Ikiwa nitamuua Thomas na kupiga magoti mbele yako, unaweza kunisamehe?"
Midomo ya Sarah ilitetemeka. "Hiyo sio ninamaanisha ..."
"Toka nje." Lisa alielekeza mlango. “Hatutasuluhisha suala hili faraghani. Uhalifu wowote aliofanya utashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.”
Mdomo wa Sarah ulisogea na alipotaka kuzungumza, Lisa akaendelea, “Usinipige magoti wala usiombe msamaha. Hata ukigonga kichwa hadi kipasuke, ni bure. Mimi sio Alvin Kimaro, kwa hivyo sitajisikia vibaya.”
“Lisa Jones,” Alvin alimuonya. Alikuwa mwisho wa subira yake.
“Nimesema kitu kibaya? Yaani kaka yake atufanyie ubaya na bado sisi ndiyo tuwe wanyonge kwenu, kweli? Anafanya kana kwamba yupo juu ya sheria, lakini badala yake sisi ndiyo tumegeuka kuwa wabaya.” Lisa alicheka. “Ondokeni machoni mwangu. Nikiwaona tena, naogopa ninaweza hata kutapika mpaka utumbo. Ninahofia ninaweza kuwatapika hata watoto...”
Alvin alikasirika, lakini kwa kuzingatia watoto tumboni mwake, alimkumbatia Sarah na kuondoka.
Lisa alifunga mlango kwa nguvu na kuuegemea mlango kabla hajashuka taratibu. Alizika uso wake katika magoti yake. Alikuwa na maumivu, kiakili na kimwili. Mwanaume aliyempenda hakuwa naye tena moyoni mwake. Angeweza kufanya nini ili asiumizwe tena na watu hao wawili?
•••
Saa moja asubuhi, Lisa alienda kumuona Kelvin kwenye wodi ya jirani kabla ya kwenda kununua kifungua kinywa. Alipokuwa anelekea kwenye mlango wa wodi ya Pamela baada ya kununua kifungua kinywa, alisikia sauti ya Pamela akirusha vitu huku na kule. “Wewe b*star, hivi Lisa alimpendaje mwanaume kama wewe? Hapana, wewe si mwanaume. Wewe ni shetani.”
“Pamela…” Lisa aliingia ndani haraka, na kumuona Pamela akiwa ameegemea kitanda cha hospitali kama mnyama aliyejeruhiwa aliyepandwa na hasira. Hata hivyo, hakuwa na nguvu na punde si punde alianguka kwa kutetemeka kwenye mto.
Kwa upande wa Alvin, alisimama mbele ya kitanda huku uso wake ukiwa umekunja sura ngumu.
“Ulimwambia nini jamani?” Lisa alimsukuma Alvin kwa hasira. “Angalia jinsi alivyomnyonge! Kwanini bado hutaki kumwacha?”
Alvin aliwatazama wale wanawake wawili wenye hasira na kukunja ngumi zake kwa nguvu. "Nilisema nitampa yeye na Kelvin milioni 300 kila mmoja, kisha waachane kabisa na suala hili."
"Sawa, nimekubali," Pamela ghafla alisema kwa upole.
“Pamela, una kichaa?” Lisa aliuliza huku akiwa haamini. “Alvin, kakutishia kitu? Najua wewe na Kelvin msingekubali hivhivi tu hata kama mgekuwa na shida na pesa. Lazima kuna kitu amekutishia, ni kipi hicho? Ikiwa Thomas Njau hataenda jela, ataendelea kukusumbua tena na tena. Yeye haogopi chochote katika ulimwengu huu.”
"Lisa, hapana." Pamela aliinua kichwa chake na kumtazama kwa kusihi. “Sitaki mambo haya yafike mbali na kuwaumiza watu wengine…”
“Pamela, usiseme hivyo. Wewe ni jasiri kuliko maneno unayoongea.” Lisa alimkazia macho Alvin. "Sema! Umemtishia nini? Kwanini usinitishie mimi basi badala yake?”
Akiwa amekereka, Alvin akalegeza tai yake. "Lisa Jones, ikiwa utaendelea kufuatilia suala hili, nitamzuia Daktari Angelo kuponya ugonjwa wa baba yako."
Lisa alihisi ngurumo kwenye ubongo wake. Alimtazama Pamela. “Ndivyo alivyokutishia hivyo?”
Pamela alisema kwa uchungu, “Lisa, una baba mmoja tu. Sitaki umpoteze.”
“Ndiyo, nyie wote mnajua jinsi baba yangu alivyo muhimu kwangu kwa sababu ninaye mmoja tu. Ndiyo maana ananitisha na baba yangu tena na tena.” Lisa alimtazama Alvin kwa ukali. "Mara ya mwisho, ilikuwa ni kwa ajili ya sifa ya Sarah ukanilazimisha kutangaza kwamba tumeachana, na watu kwenye mtandao bado wananikosoa hadi leo. Sasa unanitishia maisha ya baba yangu kwa sababu ya huyo fisadi Thomas?”
Sura ya: 302
Alvin aliuma midomo yake myembamba kimya kimya. Lisa alikosa subira na kumkimbilia kumsukuma. “Alvin Kimaro, mbona unanifanyia Ukatili sana? Wewe ni binadamu kweli? Kwa sababu ya Sarah, umeniumiza mimi na watu walio karibu na mimi tena na tena. Kukutana na wewe lilikuwa kosa kubwa.”
Hakuweza tena kuyazuia machozi yake huku akiinama chini. Alvin alihisi uvimbe kooni. Kwa sababu fulani, moyo wake ulihisi kama unakandamizwa na mkono, na kufanya iwe vigumu kwake kupumua.
"Lisa, usilie." Pamela alijaribu kuinuka na kumfariji. Lakini, mara tu aliposogea, alianguka kitandani.
"Pamela, usisimame, bado hauna nguvu." Lisa alimsaidia kwa haraka kurudi nyuma.
“Lisa nisikilize. Mimi nimekubali tu kuachana na hii kesi. Usiifuatilie. Kwa vyovyote vile… sikulazimishwa.” Pamela alimshika mkono na kulazimisha tabasamu.
"Hapana." Lisa akatikisa kichwa. "Ikiwa Thomas Njau hatahukumiwa wakati huu, atavuka mipaka zaidi wakati ujao. Sitaki upatane kwa ajili yangu. Nataka aende jela.” Alimtazama Alvin na kuuma mdomo. “Sawa. Mwambie Daktari Angelo aondoke. Kwa kiwango kikubwa, nafasi ya baba yangu kuweza kupona ni ndogo sana.”
"Lisa Jones, kwanini unataka kulazimisha hasira yangu?" Uso wa Alvin haukuonekana kupendeza.
Lisa aliangua kicheko. "Ni nani aliyelazimishwa hapa?"
“Bwana Kimaro, Lisa siye aliyevamiwa, ni mimi. Hawezi kuniamulia,” Pamela alisema kwa haraka. “Nilisema sitafuatilia suala hilo, kwa hiyo tuachane nalo. We ondoka kwa amani tu. Hii ni kauli yangu ya mwisho."
“Pamela…”
“Usiseme chochote Lisa.” Macho ya Pamela yalijawa na dhamira. “Sisi ni marafiki. Hata kama ungekuwa ni wewe kwa ajili yangu, ungefanya vivyo hivyo.”
Macho ya Lisa yakawa mekundu mara moja. Uhusiano wake ulikuwa umejaa fujo, lakini kwa bahati nzuri, alikuwa na rafiki ambaye asingemwacha. Lisa alisimama na kuinua kichwa chake kwa ukaidi. "Hata kama Pamela atakubali, kuna mwathirika mwingine. Hata…”
“Ninakubali pia.” Sauti ya Kelvin ilisikika ghafla kutoka mlangoni.
Lisa aligeuka na kumwona Kelvin akiwa ameshikwa mkono na msaidizi wake. Alikuwa amesimama pale muda mrefu sana lakini kwa kuwa walikuwa kwenye zogo hawakuweza kutambua uwepo wake. Mkono wake bado ulikuwa kwenye banzi. Kelvin akasogea kuinga chumbani, kila hatua aliyopiga ilikuwa ya uchungu sana. “Endelea kumtibu baba yake. Suala hili litaishia hapahapa.”
“Kelvin…” Lisa aliuma midomo yake, lakini machozi yalikuwa bado yakitiririka mashavuni mwake.
Kelvin hakumtazama. Badala yake, alimtazama Alvin kwa huzuni na chuki. "Hujui jinsi ya kumtunza mwanamke huyu na unaishia tu kumuumiza mara kwa mara. Alvin Kimaro, kama wewe bado ni mwanamume, basi mtaliki. Acha kumuumiza kwa mwanamke mwingine. Tayari amefunikwa na makovu chungu mzima kwa sababu yako.”
Alvin alimtazama Lisa mwenye machozi, na kisha akamtazama Kelvin, ambaye alikuwa akimlinda. Mlipuko wa hasira ukapanda moyoni mwake. "Ni uamuzi wangu ikiwa nitaachana naye au la. Kwa kuwa mwanzoni alinitongoza bila aibu, haya yote ni yake mwenyewe.”
“Nani alikutongoza? Ni wewe uliyempokonya kutoka kwangu kwa ndoana au kwa hila. Alikuwa mchumba wangu.” Kelvin alikasirika.
"Kwa hivyo kama angekuwa mchumba wako?" Alvin alitabasamu huku akionyesha ujeuri machoni mwake, jambo ambalo hakulitambua. "Mbona alikubali kulala na mimi na kubeba watoto wangu tumboni mwake, na hata sasa bado ananisumbua na kunibembeleza?”
Lisa hakuweza kuvumilia tena. “Nani anakusumbua? Maadamu uko tayari kunitaliki, nitaondoka mara moja.”
"Nini? Je, ulifikiri kwamba ungeweza kunitongoza tu na kuniacha muda wowote unaotaka, ndiyo maana ukaamua kuwa na Kelvin kama mpango wako mbadala?” Alvin alibana kidevu chake kikatili. "Lisa Jones, sitaruhusu watoto walio tumboni mwako kumwita mtu mwingine baba yao. Hata ukitaka talaka, itabidi uzae watoto kwanza. Itakuwa wakati muafaka kwako kumfungulia Sarah nafasi.”
Maneno yake yalikuwa kama visu vinavyouchoma moyoni mwa Lisa tena na tena. Yalikuwa machungu sana hadi yakamzuia kupumua vizuri.
“Kwa kuwa unampenda sana Sara, kwanini usimzalishe watoto wako? Nendeni mkazae watoto wenu wenyewe. Kwanini ukae na mwanamke mwingine kisha uwatolee macho watoto wangu?” Alisihi huku akitokwa na machozi. “Alvin nakuomba sana. Niache na watoto wangu, sawa?"
Macho ya Alvin yalimtoka. Kisha, akageuza uso wake uliojaa jeuri. “Hapana, kuzaa ni uchungu sana. Siwezi kuvumilia kwa Sarah kupata uchungu wa uzazi. Anachopaswa kufanya ni kuwa Bibi Kimaro na kulea watoto wangu tu, basi!”
“Alvin Kimaro, wewe b*star. Wewe si binadamu.” Lisa hakuvumilia tena kumsikiliza. Sarah hakustahili maumivu, hivyo uchungu wa kuzaa watoto ukasukumwa kwa Lisa badala yake. Bado alikuwa binadamu kweli?
Wakati huo, alikimbia kwenda kumpiga na kumng'ata kama mnyama. Ni kana kwamba alikuwa amesahau kwamba alikuwa mjamzito.
Akiwa ameshtuka, Alvin aliumwa kwenye mkono wake. Lakini, alijaribu kila awezalo kujizuia asimsukume.
"Njoo mumshike haraka." Alvin akaamuru na walinzi kadhaa waliingia ndani kwa sauti yake. Sekunde chache tu, wakamkandamiza Lisa chini.
“Alvin Kimaro, unafanya nini? Achana naye.” Kelvin alivumilia maumivu ya majeraha yake na kusonga mbele. Pamoja na hayo, harakaharaka alisukumwa pembeni na mlinzi mmoja. Ilimuuma sana hata akashindwa kuamka tena.
"Alvin, unaweza kunifanya utakavyokavyo, lakini usiwadhuru watu wasio na hatia." Macho ya Lisa ya wasiwasi yalijaa chuki.
“Usijali. Sitamlemaza, lakini ili kuepusha usiendelee kunipandisha hasira ukiwa mjamzito, hutaruhusiwa kwenda popote ukiwa mjamzito.” Uso wa Alvin uligeuka kuwa mbaya alipoona jinsi Lisa alivyokuwa na wasiwasi juu ya Kelvin. Baada ya hapo, alimnyanyua kwa nguvu na kutoka nje ya chumba hicho.
“Niache niende.” Haijalishi jinsi Lisa alimpiga sana njiani na kuchana mikwaruzo michache kwenye uso wake, haikuwa na maana. Wakiwa ndani ya gari, Alvin alimfunga kamba.
“Alvin Kimaro, kwanini unanifanyia hivi? Niache niende.” Lisa alijitahidi sana, lakini Alvin akafumbia macho.
Gari lilimpeleka moja kwa moja hadi New Metropolis Park. Alimbeba hadi chumbani na kumuonya kwa uso wa huzuni, “Kwa kuwa hutabaki kwenye nyumba ya Mzee Kimaro tena, basi utakaa hapa kuanzia sasa. Huruhusiwi kwenda popote bila idhini yangu. Kaa tu hapa kama msichana mzuri hadi watoto watakapozaliwa.
"Unanifungia?" Lisa alihisi kana kwamba anapandisha kichaa. Sio tu kwamba Alvin angempa Sarah watoto ambao Lisa alingezaa, lakini pia alikuwa akimfungia. Je, bado alikuwa binadamu? “Unawezaje kufanya hivyo? Hii ni kinyume cha sheria. Napiga simu polisi.”
Lisa alichukua simu yake, lakini Alvin alimpokonya na kuivunja kwa kuibamiza chini. “Lisa Jones, nilishawahi kukupa nafasi. Ni kosa lako kujihusisha na Kelvin Mushi.” Alvin alishindwa kujua kwanini yeye mwenyewe alikuwa amekasirika hivyo. Labda ndiyo yale wahenga walisema ‘mkuki kwa nguruwe!?’.
“Una haki gani ya kuniambia hivyo? Wewe ndiye unayeendekeza uhusiano wa kimapenzi na Sarah ukiwa bado kwenye ndoa. Usifikiri sijui kuwa tayari umeshalala naye.”
“Kwahiyo kama nimelala naye itakuwaje? Angalia jinsi unavyoonekana kuwa mbaya na mwendawazimu. Unawezaje kujilinganisha na Sarah?" Kadiri alivyozidi kusema ndivyo maneno yake yalivyokuwa makali na makali zaidi.
Lisa alipigwa na butwaa. Alipougusa uso wake usio sawa, moyo wake ulimuuma zaidi. Ni nani aliyesema hajali kuharibika kwake? Lakini sasa, alisema kwamba alikuwa mbaya.
Uso wake uliharibika kwa sababu gani hapo mwanzo? Je, hakukumbuka hilo hata kidogo?
"Alvin, ikiwa utatoa watoto wangu kwa Sarah, ni bora niruke kutoka kwenye jengo hili." Lisa alisema kwa uthabiti na uso wa kumaanisha.
“Ruka, fanya haraka. Ukithubutu kuwaumiza wanangu, nitawazika rafiki zako na baba yako ambaye amelazwa hospitalini,” Alvin alisema kwa ukali. Kisha akaufunga mlango kwa nguvu na kuondoka zake.....ITAENDELEA....
Unafikiri nini kitafuata hapo, maana simulizi inazidi kuwa tamu kila siku lakini sina budi kuhitimisha kipande hiki ila niwasihi tukutane katika episode zijazo ili kujua nini kitafuata kwenye mkasa huu wa kusisimua na kuelimisha unaokwenda kwa jina la LISA.
