JINA LA SIMULIZI............................LISA
AUTHOR...........................JOMBA WAJO
SPONSORED BY......SIMULIZI ZA DULLY
WHATSAPP..........................0628924768
SEHEMU YA................................281-282

Sura ya: 281

“Pia, huruhusiwi kutumia muda mwingi na Sarah peke yako isipokuwa unapoenda kutibiwa. Najua Rodney na Chester wako kwenye uhusiano wa kirafiki, kwa hivyo watakutana mara nyingi. Mkikutana nyinyi wanne wakati ujao, lazima na mimi niwepo.”
Lisa aliuzika uso wake kwenye kifua cha Alvin kwa sura ya kupendeza.
Ilikuwa ni muda mrefu tangu aongee kwa upole hivyo mbele ya Alvin. Akawa na moyo mpole na kuchanganyikiwa mara moja. “Lakini Rodney na Chester—”
“Najua hawanipendi, lakini ni sawa. Ninaweza kuvumilia maadamu nitaweza kuzuia mume wangu asinyang’anywe na mwanamke mwingine.” Lisa aliinua kichwa chake na kupepesa macho yake makubwa ya kupendeza. “Ni kwa sababu wewe ni mzuri sana. Nakupenda."
“Babe, nitakusikiliza.” Macho ya Alvin yakaangaza. Akainamisha kichwa chake na kumbusu kwenye midomo.
Akashusha pumzi huku akiwa ametawaliwa kabisa na mahaba ya yule mwanamke. Katika hali hiyo, jambo gani lingeweza kutokea kati ya Sara na yeye? Lakini, haikujalisha. Maadam alitaka kuwa naye anapokuwa pamoja na marafiki zake, ilibidi amkubalie mradi tu alikuwa na furaha.
Alvin aliamka na kuelekea sebuleni huku mkono wake ukiwa umeshika kiuno cha Lisa. Mdomo wa Lisa ulikuwa umevimba kidogo, na mashavu yake yalikuwa yamepauka.
Akiwa na uzoefu wa miaka mingi wa mambo kama hayo yeye mwenyewe, Bibi Kimaro hakuwa mgeni juu ya kile kilichotokea kwao baada ya kuwaona asubuhi wakiwa vile. Alifarijika na kuwa na wasiwasikwa wakati mmoja. “Hivi ndivyo nyinyi wawili mnapaswa kuishi kama wanandoa. Lakini mnapaswa kuwa waangalifu. Daktari alisema hivyo hospitalini—”
“Hatukufanya chochote, Bibi. Sio lazima uendelee kunikumbusha. Mimi si mtoto.” Uso wa Alvin ulisinyaa baada ya kusikia maneno hayo, huku Lisa akitamani ardhi immeze.
Moyoni mwake, Jack alikuwa akionyesha kutoridhika kwake wakati anapata kifungua kinywa chake. Alvin na Lisa walikuwa na mzozo mkali jana yake, lakini walionekana kuwa na uhusiano mzuri asubuhi hiyo kama mbaazi mbili kwenye ganda moja. Kweli mambo ya wapendanao usipende kuyafungia kibwewbwe.
Jack hakuwa na uhakika kama ni Alvin ndiye alikuwa mtaalam wa kutuliza wanawake, au Lisa alikuwa mtaalam wa kushughulika na wanaume. Lakini, wanandoa hao kweli walikuwa wataalam.
"Halafu, nilisikia kuwa ninyi watatu mmerudi pamoja jana usiku," Mzee Kimaro ghafla aliuliza. “Mlikuwa wapi usiku huo?”
"Khooh, khohooh!" Jack karibu apaliwe sandwich yake.
Alvin alimtazama kwa hasira. "Lisa alinikuwa ameni’miss, kwa hivyo Jack alimleta kunitembelea nyumbani kwangu jana. Tulikula chakula cha jioni pamoja kabla ya kurudi nyumbani.”
Kwa hayo, Lisa alikanyaga mguu wake. Alimm’miss? Ha! Hakuwa na aibu kama nini kusema uwongo kama huo. Kwa kweli, alikuwa ameenda kumfumania kama alikuwa kitandani na Sarah.
Alvin alimtazama kwa jicho la huzuni. Hata hivyo, Lisa alitazama pembeni na kumpuuza.
Mzee Kimaro hakuona mkanganyiko wao na hivyo alitikisa kichwa kwa hali ya utulivu. "Sikutarajia kwamba ungeenda kula chakula cha jioni na Jack."
Jack alikoroma. "Ni Shemeji ndiye aliyeomba, vinginevyo nisingekula naye chakula cha jioni."
Bibi Kimaro alikodoa macho. Alifurahi kwamba Lisa alikuwa amefaulu kuwapatanisha ndugu wale mahasimu. “Hiyo ni nzuri. Kama ndugu, mnapaswa kuungana katika hatua hii. Hatima imewafunga nyinyi kwa damu, kwa hivyo mnapaswa kuthamini udugu wenu milele.”
Alvin na Jack wote walivuta nyuso ndefu. Hawakuthamini kifungo chao cha damu hata kidogo.
Baada ya kiamsha kinywa, Lisa alisema, “Bibi, mwanasaikolojia wa Alvin atakuja nyumbani kumtibu. Unafikiri matibabu yanapaswa kufanyika wapi? Na pia, nadhani unamjua mwanasaikolojia mwenyewe. Yeye ni Sarah Langa Njau.
Mshindo ukasikika! Kijiko katika mkono wa Bibi Kimaro kilianguka kwenye meza. Aliuliza kwa msisimko, “Si amekufa?”
“Hapana, amerudi. Hakuwa amekufa, ila tu kuna mkanyiko ulitokea.” Alvin alieleza.
Mzee Kimaro alikunja zaidi uso wake. Alikuwa amekutana na Sarah enzi hizo na hakumpenda zaidi kuliko Lisa. “Je, hakuna wanasaikolojia wengine duniani? Kwanini ni lazima umwambie Sarah atibu ugonjwa wako? Tafuta mtu mwingine."

Bii Kimaro aliitikia kwa kichwa. “Hasa. Unawezaje kumwomba mpenzi wako wa zamani akutibu? Umewahi kufikiria hisia za mkeo?”
Lisa akashusha pumzi. Kwa mwonekano wake, Bibi Kimaro na Mzee Kimaro hawakuwa wakimpenda Sarah.
Tabasamu la uchungu likatokea usoni mwa Alvin. "Chester alisema kuwa yeye ndiye mwanasaikolojia mahiri zaidi nchini Ujerumani. Nilipomwomba aje hapo awali, sikutarajia angekuwa Sarah pia.”
Mzee Kimaro alikaa kimya kwa muda kabla hajakubali kwa kichwa. "Sawa, lakini lazima uwe mwangalifu na tabia yako. Usipotee. Natumai hutafuata nyayo za mama yako.”
'Bila shaka sitaweza, babu." Alvin akaitikia kwa kichwa.
Akiwa njiani kuelekea ofisini, alimpigia simu Sarah ili wazungumze kuhusu eneo la matibabu yake.
“Kwa kweli nilitarajia hii. Nitakutibia kwa Mzee Kimaro, basi. Lakini babu na bibi yako hawakunipenda kabisa kipindi kile. Ninaogopa—”
“Nimewajulisha kuhusu hilo. Wanaelewa.”
“Sawa basi.” Sarah alinyamaza kwa muda kabla ya kuendelea, “Kusema kweli, nilikuja na mpango wa kutibu ugonjwa wako katika mazingira ya awali. Sasa kwa kuwa eneo limebadilishwa, lazima nipange upya kila kitu. Katika hali hii, huenda usiweze kupona haraka kama tulivyopanga. Natumai umeelewa.”
Alvin alikunja uso. Bila shaka, alitarajia kupona haraka iwezekanavyo. Hata hivyo, kwa kuwa ilimsumbua Lisa kwamba alikuwa peke yake na Sarah, hakuweza kufanya chochote kuhusu hilo. “Sawa basi. By the way, ulikuwa sawa jana usiku? Mbona hukuniambia kuwa hukuwa na gari? Ningemwomba dereva wangu akupeleke nyumbani.”
“Siyo ishu kubwa. Ungeendelea kunijali zaidi jana usiku, ndivyo mke wako angetuelewa vibaya zaidi,” Sarah alisema kwa sauti ya chini, “Sitaki kuharibu uhusiano mzuri ambao uko nao na mkeo hatimaye.”
Alvin alijikandamiza kwenye paji la uso wake. “Sarah, unaweza kuwa na furaha pia. Cha kusikitisha ni kwamba hatujapangiwa kuwa pamoja, lakini kuna mtu ambaye amekuwa akikujali sana tangu zamani…”
“Unamaanisha… Rodney?” Sarah alifungua kinywa chake na kusema kwa hisia mseto.
“Mm. Kwa kweli, amekuangukia kwa muda mrefu.”
"Hapana. Rodney anastahili mtu bora zaidi. Wanawake waliochafuliwa kama mimi hawastahili kuwa naye. Hebu tuishie hapa. Unaweza kuendelea na mambo yako. Nitakutana na wewe kkwa babu yako usiku wa leo."
Alvin alishusha pumzi baada ya kukata simu. Alitumaini kwamba Sarah hatimaye angempata mpenzi wa kumweka busy. Kwa njia hii, Lisa asingeweza kuwa na wasiwasi juu yake baada ya kujua kwamba Sarah ana mpenzi.
•••
Akiwa katika ofisi yake ndani ya kampuni ya Mawenzi, baada ya kuangalia utendaji wa kampuni ofisini, Lisa aligundua kuwa kampuni hiyo imefanya vizuri zaidi licha ya kutokuwepo kwake kwa siku kadhaa.
Meneja Mkuu alisema kwa tabasamu, "Bwana Kimaro kwa hakika anastahili kutambulika kama mtu tajiri zaidi nchini Kenya na talanta yake ya ajabu katika mambo ya biashara. Licha ya kutumia muda mfupi kushughulika na mambo ya Mawenzi, aliiingizia kampuni hiyo mapato makubwa kwa kutoa maagizo machache tu. Mauzo ya bidhaa yameongezeka kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea.
Lisa alijikuta anaingiwa na wivu. Sio tu kwamba Alvin alikuwa mzuri, lakini pia alikuwa na kipaji cha biashara zaidi kuliko wengine. Jinsi gani alipendelewa! Jambo hilo lilimfanya Lisa, ambaye alikuwa mkurugenzi wa kampuni hiyo, ahisi kana kwamba hahitajiki.
"Pamoja na hayo, kampuni yetu imekuwa hapa Nairobi kwa karibu nusu mwaka. Kando na ujenzi wa ofisi zetu mpya hapa Nairobi, kwanini hakuna miradi ya ujenzi kwenye mikoa mingine?” Lisa aliuliza kwa kutoridhika.
Meneja Mkuu alilazimisha tabasamu. “Mwenyekiti Jones, Baada ya kampuni ya Ngosha kuungana na Campos Ltd. Wamekuwa na kiburi sana. Melanie sasa ni naibu Mkurugenzi mkuu na amekuwa akitufuatilia sana. Amekuwa akipandilia bei kila eneo tunalotaka kununua huko mikoani na hivyo kuharibu biashara.”
Lisa aliinua uso wake na kugonga meza kwa upole. "Sawa. Hakuna haraka."
Angesubiri tu aone Melanie bado angeweza kuwa na jeuri baada ya taarifa za Melanie kutokuwa binti Joel kufichuka.

Sura ya: 282

“Halafu, Mkurugenzi mpaya wa kampuni ya New Era Advertisings amechaguliwa leo tu. Amekuletea mwaliko wa kushiriki party ya kumpongeza.” Meneja Mkuu alimkumbusha Lisa.
Lisa alipigwa na butwaa. "Nani huyo?"
"Thomas Njau, mtoto mkubwa wa Boris Langa Njau na mke wake wa zamani.” Meneja Mkuu alieleza. “Hapo awali, nilisikia kwamba New Era Advertisings ilinyimwa nafasi ya kuuza matangazo yao kwenye mtandao wa Alvinarah Media Network Group na KIM Outdoor hivyo kukaribia kufilisika baada ya kupoteza wateja wao wote. Lakini cha kushangaza, AMEN Group na KIM Outdoor wamekubali kuwapa nafasi ya kuendelea kufanya nao biashara hivi punde mara tu Thomas alipochukua kampuni hiyo.
Hali ya Lisa ikabadilika kidogo. Aligundua kila kitu ndani ya muda mfupi. Thomas Njau, yule mwanaharamu, alichukua nafasi hiyo mara tu baada ya Charity Njau kuhukumiwa kifungo cha maisha. Bila kupepesa macho Alvin na Sarah walikuwa na mkono katika uamuzi huo.
Haijalishi ni kiasi gani Lisa na Charity walikuwa wamemsihi Alvin wakati huo, alikataa katakata kuiruhusu New Era Advertisings kuchomoka kwenye ndoano. Hata hivyo, sasa Sarah alikuwa amerudi, Thomas akawa Mkurugenzi wa kampuni na kupewa nafasi ya kuendelea na biashara.
'Alvin, oh Alvin, unaweza usiwe na wazo la kurudiana na Sarah, lakini bado ana nafasi ya pekee moyoni mwako.’ Lisa alijiwazia. Kama si Lisa ambaye alikuwa mjamzito, pengine Alvin angempa umuhimu zaidi Sarah kuliko yeye. Lisa akashusha pumzi ndefu. Alilazimika kudhibiti hisia zake kwa ajili ya watoto wake.
Akiwa katika mawazo yake, alipokea ujumbe wa WhatsApp kutoka kwa 'Ni Wako Pekee'. [Babe, uko sawa katika siku yako ya kwanza ya kazi? Una njaa? Unataka kula nini? Nitamwomba Hans akuletee chakula.]
'Jamani wewe, mpuuzi. Nenda kafie mbele huko!' Lisa alitamani kumwambia maneno hayo lakini bila kupenda akayazuia kwenye mawazo yake. Aliitupa simu yake na hakutamani hata kujibu ujumbe huo.
Dakika kumi baadaye, Alvin alimpigia simu. “Babe, kwa nini hukujibu ujumbe wangu?”
"Sikutaka kujibu." Lisa alitamani sana kuficha kinyongo chake dhidi ya Alvin, lakini alikasirika sana hivi kwamba alishindwa kufanya hivyo.
"Nini tatizo?" Alvin alichanganyikiwa. "Kuna mtu katika kampuni amekukosea?"
“Umeniudhi.” Kwa hasira, Lisa aliongeza, “Kwanini ulimruhusu Thomas kuchukua nafasi ya Mkurugenzi wa New Era Advertisings? Unajua kwamba alinidhalilisha katika baa wakati huo na kufanya yale matendo maovu ambayo yalikaribia kumfanya Zigi aniue? Lakini umeamua kumsikiliza Sarah na kumsaidia Thomas haijalishi ni mwovu kiasi gani, sivyo? Hapo awali, uliahidi kwamba hautamjali tena. Umesahau kuhusu hilo tayari?"
Alvin kichwa kilianza kumuuma. "Nilikuwa nalipa somo New Era Advertisings hasa kwa sababu ya Charity-"
"Sawa. Kabla ya hili, ulikuwa ukitaka kuharibu New Era Advertisings. Sasa Sarah amerudi, umesitisha mipango yako yote. Nina hakika alikubembelezai. Alipokusihi, ulikubaliana naye. Lakini nilipokusihi, ulikataa. Mke wako ni nani hapa?"
"Lisa, tutabishana tena juu ya hili? Mbona siku zote unataka kunichokoza tu? Kwani utakuwaje ikiwa utaachana na mambo ya familia ya Njau?” Alvin aliongea kwa ukali kidogo.
Lisa akakata simu. Alijiona si muhimu kama Sarah katika moyo wa Alvin. Aliumia sana moyoni hata akakaribia kutokwa na machozi. Hata hivyo, hakutaka kulia kwa sababu yake tena. Hakustahili machozi yake.
Alasiri, Lisa alienda hospitali kumtembelea Joel. Daktari Angelo alimweleza kipande cha habari njema. "Baba yako anaweza kupata fahamu baada ya miezi miwili."
“Kweli?” Lisa alifurahi sana. Ilikuwa habari nzuri zaidi ambayo alikuwa amesikia kwa kipindi hicho.
Lisa hakuwahi kutamani uwepo wa Joel zaidi ya wakati huu. Alitamani sana apate fahamu ili angalau awe na mwanafamilia wa kumtegemea.
“Baba naomba uamke upesi. Ninateseka, na ninakukumbuka sana.”
Matone yake ya machozi yalitua nyuma ya mkono wa Joel. Hakuona kwamba vidole vyake vinatetemeka.
Baadaye, alienda kumwangalia Boris Langa katika wadi nyingine ya hospitali. Aligundua alipokuwa akiingia ndani kwamba mtu huyo alikuwa akihangaika kufikia beseni chini ya kitanda.

"Mjomba Boris, niruhusu nikusaidie." Haraka akasogea kumshika mkono. "Mimi ni rafiki wa Charity."
“Asante.” Akalipokea lile beseni huku akionekana kuwa na aibu kidogo. Lisa akatoka kidogo kumuachia faragha.
Dakika kadhaa baadaye, Lisa alirudi na kwenda kumimina yaliyokuwamo kwenye beseni ndani ya sinki la choo.
"Mjomba Boris, mbona uko peke yako? Aunty Jennifer na mlezi wako wapi?
“Mlezi hakuwa na nafasi asubuhi ya leo, na Jennifer aliondoka nyumbani kwenda kufungasha mizigo yetu. Alisema anataka kunihamisha hadi hospitali nyingine huko Dar es Salaam. Lakinitangu aondoke hajafika na siwezi kumpata kwa simu pia.” Alisikika akiwa na wasiwasi. “Natamani kwenda kumtafuta lakini siwezi katika hali hii. Kwa bahati nzuri, Pamela alifika hapo awali kwa hivyo nilimwomba amchunguze Jennifer.”
Lisa alikuwa na hisia mbaya na ghafla akakumbuka ombi la Charity la kuwatoa wazazi wake kutoka Nairobi haraka iwezekanavyo. “Vipi kuhusu mwanao? Au Sarah? Alirudi si muda mrefu uliopita. Si alikuja kukuchunga?”
“Sarah?” Boris alionekana kushtuka. “Si amekufa?”
“Nadhani bado hujui kwamba hajafa. Hata nilikutana naye ana kwa ana.”
Hakuwa na la kusema. Sarah alikuwa na muda wa kuhudhuria mazishi ya Maurine na wala hata hakumtembelea baba yake mzazi ambaye alikuwa amelazwa hospitalini kwa siku chache. Hakupaswa kuwa hivi hata kama baba yake alikuwa ameoa mwanamke mwingine.
'Kwa kweli sikuwa na wazo.” Alitikisa kichwa kwa unyonge huku tabasamu la uchungu likitanda usoni mwake. "Hata hivyo, sitarajii chochote kutoka kwa hao watoto wangu wawili. Tangu mwanzo nimekuwa nikiwategemea Charity na Jennifer, lakini sasa Charity yuko ndani…” Machozi yalimtoka. "Kabla polisi hawajaja kumkata, niilikuwa tnikimwambia Charity mchana huo kwamba tunapaswa kuuza kampuni na kuondoka Nairobi kabla hatujafilisika kabisa ..."
Lisa aliuliza baada ya kusita kidogo, "Unajua kwamba Thomas amechukua New Era Advertisings?"
“Thomas?” Mshangao ulimwagika usoni mwake kabla ya kutikisa kichwa. “Huyo mpuuzi hana uwezo wa kuendesha kampuni. Majuto yangu makubwa katika maisha haya ni kumzaa mtoto huyu. Amefanya mambo mengi ya kutisha katika maisha yake lakini kwanini hajafungwa gerezani? Atakuwa mbaya zaidi baada ya kuwa Mkurugenzi."
Hilo lilimshangaza Lisa. Hakujua kuwa Boris hakuridhika na mtoto wake, ingawa kwa mawazo ya pili, alikuwa akisema ukweli tu. Sekunde chache baadaye, Boris alishusha pumzi ndefu na kutikisa mkono wake hewani. “Sawa, mimi sijali kuhusu biashara tena. Ninachotaka sasa ni kuondoka Nairobi na Jennifer. Tunaweza kujaribu tuwezavyo kumtoa Charity gerezani. Ninajua kwa hakika kwamba hana hatia. Hakuwa na sababu ya kumuumiza Maurine. Walikuwa marafiki na walicheza pamoja tangu walipokuwa wadogo…”
Lisa aliuliza kwa kusitasita, “Kwa hiyo, wewe pia huna uhusiano mzuri na Sarah? Vinginevyo, kwa nini hajaja kukuona…”
Kimya kirefu kilipita hadi Lisa akajishtukia kwa kumuuliza swali hilo. "Samahani. Huna budi kujibu hili…”
“Ni sawa. Labda ananilaumu kwa kuoa tena.” Alitabasamu kwa uchungu. “Sikuwa na namna nyingine. Wakati huo nilikuwa busy sana na kazi na mama yake Sarah alikuwa akinisaliti na wanaume wengine nyuma yangu. Sikuweza kuvumilia tena na mwishowe nikampa talaka. Lakini ili kuhakikisha watoto hao wawili wangekua katika mazingira yenye afya, sikuwahi kumsema vibaya mke wangu wa zamani hata mara moja. Labda walidhani mimi ndiye niliyemsaliti mama yao na polepole wakajitenga nami kwa sababu hiyo. Kwa kweli, Jennifer aliwajali kama watoto wake lakini wao hawakuthamini upendo wake—kama vile mama yao.”
Lisa alishangaa kujua hivyo. Ilionekana kuwa Boris pia alikuwa na hali ngumu. Ni wazi kwamba Sarah na kaka yake hawakuwa watu wazuri lakini Alvin na marafiki zake hawakuliona hilo. Jambo hili lilimvunja moyo sana Lisa.
Muda si mrefu, Pamela alimpigia simu. “Lisa, kuna kitu kibaya kimetokea. Mama yake Charity amekufa.”
Lisa alipigwa na butwaa na kukaa kimya. Alijilazimisha kuitikia kwa utulivu kabla ya kutoka nje ya wodi.......ITAENDELEA.....

Unafikiri nini kitafuata hapo, maana simulizi inazidi kuwa tamu kila siku lakini sina budi kuhitimisha kipande hiki ila niwasihi tukutane katika episode zijazo ili kujua nini kitafuata kwenye mkasa huu wa kusisimua na kuelimisha unaokwenda kwa jina la LISA.