JINA LA SIMULIZI............................LISA
AUTHOR...........................JOMBA WAJO
SPONSORED BY......SIMULIZI ZA DULLY
WHATSAPP..........................0628924768
SEHEMU YA................................268-269

Sura ya: 268

Mara baada ya Patrick kusikia maneno hayo, uso wake mzuri ulianza kuonyesha hasira. “Hili lieleweke vizuri, yeye ndiye aliyemvamia na kumpiga Linda bila sababu. Nimeachana naye kwa muda mrefu.”
“Unajua nini kilimfanya ampige Linda?”
Baada ya kusikia swali kali la Forrest, Patrick alipigwa na butwaa. "Haijalishi ni sababu gani, si sawa alivyofanya."
Pamela alitoa tabasamu, ambalo lilionekana kuficha huzuni kwenye uso wake wa machozi. Kwa kweli alijilaumu kwa kuangukia kwa mtu kama huyo wakati huo. Alikuwa kipofu?
Forrest alimpigapiga Pamela begani kwa huzuni. “Si sawa kumpiga mtu, lakini kwa kuwa ni mpenzi wako wa zamani, huelewi tabia yake? Kweli, labda usingeweza kujisumbua kumwelewa. Kwako, hata nywele tu za mwanamke huyu ni muhimu zaidi kuliko moyo wa Pamela. Labda, machoni pako, Pamela ni takataka tu.”
Patrick aliganda kwa muda. "Forrest, tunazungumzia tukio la kupigwa makofi, sio thamani ya Pamela ama Linda. Siwezi kujadili kile kilichotokea huko nyuma pia. Tumeachana kwa muda mrefu.”
“Uko sahihi. Nimesikitika tu kwa sababu dada yangu alipoteza muda wa ujana wake kwa mwanaume kama wewe.” Macho ya Forrest yalionyesha kutojali. "Kweli, kwa kuwa Pamela alimpiga Linda, inamaanisha kwamba anastahili kupigwa. Unaweza kuwaita polisi waje kwenye nyumba ya familia ya Masanja na kumkamata Pamela. Ngoja tuone kama utafanikiwa kumkamata.” Baada ya hayo, Forrest alimchukua Pamela na kuondoka naye.
"Forrest, kimsingi unampoteza Pamela kwa tabia hiyo." Akiwa ameumizwa na maneno yake, Patrick alihisi kuwa amepoteza heshima yake.
"Ndio, kwa sababu yeye ni dada yangu mpendwa, ninamjali, kwa nini nisimtetee?” Forrest alikoroma kisha akaondoka bila kuangalia nyuma.
Pamela, ambaye alilindwa mikononi mwa Forrest, hakugeuka na kumtazama Patrick tena.
Kwa upande mwingine, Patrick alihisi mzigo mkubwa wa hasira kifuani mwake ghafla. Alikumbuka Pamela akisema kwamba alijuta kuwahi kumpenda. Je, alisema tu kwa hasira au alimaanisha?
“Lo. Inauma…” Akiwa amejiegemeza kwenye mikono ya Patrick, Linda alifunika uso wake na kuugulia maumivu. "Inauma sana, Patrick."
"Ngoja nikupeleke hospitali." Patrick akamshika mkono.
“Siwezi hata kunyanyua mguu. Nadhani miguu yangu yote imejeruhiwa." Tabasamu la uchungu likaonekana usoni mwa Linda. Patrick hakuwa na la kufanya zaidi ya kumbeba na kuteremka kwenye ngazi.
"Unajua kwanini Pamela alishindwa kujizuia na kukupiga kofi, Linda?"
Sasa kwa vile Patrick alikuwa amerejesha utulivu wake, ilimgusa kwamba Pamela, ingawa alikuwa na kiburi, mara nyingi asingemshambulia mtu bila sababu hata awe na hasira kiasi gani. Zaidi ya hayo, ilikuwa imepita nusu mwaka tangu waachane. Ikiwa angekusudia kumsababishia Linda matatizo, angefanya hivyo kipindi hawajaachana.
“Ningejuaje? Nilikutana naye hospitalini mara ya mwisho. Sijakutana naye tangu wakati huo.” Linda aliongea kwa hasira.
Patrick akakaa kimya. Kuanzia siku hiyo na kuendelea, angejawa na majuto na kinyongo kwa Pamela kila alipokumbuka yaliyotokea siku hiyo, Kwa bahati mbaya, hakuna kitu ulimwenguni kinachoweza kuponya majuto.
Katika maegesho ya gari, muda mfupi baada ya Pamela kuingia ndani ya gari, alimuona Patrick akiwa amembeba Linda na kumwingiza ndani ya gari lake. Wakati huo, alihisi kukata tamaa sana. Angalau hakujuta kumpenda wakati huo, ingawa penzi lake lilikuwa la upande mmoja. Hata hivyo, sasa alijuta sana kwa kupoteza muda wake kwa mwanamume kama huyo. Hakuweza kujua jinsi alivyopofushwa na kumwangukia Patrick. Matone makubwa ya machozi yalitiririka mashavuni mwake.
Forrest akamkabidhi kipande cha tishu. “Usilie. Patrick hastahili thamani ya machozi yako. Mungu anakuonyesha haya kwa sababu anataka kukuepusha na unafiki wa mwanamume huyu"

“Kaka.” Pamela alilia kwa uchungu. “Mjinga kiasi gani mimi! Ni kwa sababu ya Patrick na mwanamke wake ndiyo maana nimeishia kuwatia marafiki zangu matatizoni.”
“Usifikirie kupita kiasi. Ulikuwa unamsaidia rafiki yako tu. Hukutegemea kama haya yangetokea.” Forrest alimtuliza na kusema. "Unatakiwa tu uwe makini, Patrick ni mhuni sana. Ni wazi mwanawake mzuri kama wewe hamstahili kabisa."

“Nifanye nini basi?” Pamela alikasirika sana. “Nimefukuzwa kazi sababu ya Linda na kuwekwa kwenye blacklist. Hakuna kiwanda chochote kitakubali kuniajiri iwe ni Kenya au Tanzania.”
"Unaweza kurudi Dar es Salaam na kusimamia kampuni ya familia yetu au uende tena kusoma nje ya nchi." Forrest alimtazama machoni. “Unapokuwa mwanakemia bingwa unayejulikana sehemu nyingi duniani, Rodney hataweza kukufanya chochote wakati huo. Zaidi ya hayo, ataweza hata kukubembeleza urudi ufanye naye kazi.”
Pamela alipokuwa akipata picha ya mawazo hayo ya kaka yake, wimbi la hisia lilimtawala. Muda mfupi baadaye, hata hivyo, alivaa uso wa ujasiri. "Hapana. Ninawezaje kumuacha Lisa akiwa juu na kuti kavu? Zaidi ya hayo, Charity yuko jela. Dhamiri yangu itanisuta nikiondoka na kuwatelekeza.”
"Huna chochote unachoweza kuwasaidia hata ukibaki kuwa nao, kuna faida gani ya wewe kuendelea kuwafikiria?" Maneno ya Forrest yalimuacha hoi kabisa.
•••
Baada ya Pamela kumjua aliyevujisha siri, alimtaarifu Lisa. Lisa alipopokea ujumbe kutoka kwa Pamela, akaenda jengo la jirani kumtafuta Alvin. Alisukuma mlango na kuingia ndani ya chumba hicho, na kumkuta mtumishi akisafisha sakafu ya chumba kilichokuwa tupu. “Alvin yuko wapi?”
“Bwana Kimaro amehamia kwenye nyumba nyingine pembeni ya hii. Hujui hilo, Bibi Mdogo?” mtumishi aliuliza kwa mshangao.
Lisa alitetemeka, akihisi baridi. Hapo awali, Alvin alisisitiza sana kulala karibu naye. Wakati mwingine, hata aliingia chumbani kwake kupitia dirishani usiku. Kwanini alibadirika ghafla? Je! ni baada ya Maurine kufariki? Je, ni kwa sababu alikuwa na matatizo naye?
Lisa alihisi Alvin amemchukia ghafla. Alichangia kifo cha Maurine na hivyo kuharibu uhusiano wa Alvin na Rodney. Alitoa kicheko cha uchungu alipogundua kuwa alikuwa akijipinga mwenyewe. Alvin alipokuwa akimsumbua, alijikuta akiudhika na kumtaka apotee. Sasa kwa kuwa alikuwa ameondoka, alikuwa akiumia kutokuwepo kwake.
Lisa alienda kwenye jengo la jirani kwa huzuni. Alipofika tu getini, akasikia kitu kikivunjika ndani. Harakaharaka akaingia ndani na kumkuta Alvin akiwa amekaa kwenye kochi huku akionyesha huzuni. Hans na Chester walikuwa wakimkandamiza pande zote mbili. Chester alikuwa anajiandaa kumchoma sindano ya kichwa.
“Kuna nini… Ana tatizo gani?” Kwa kuona macho ya Alvin ambaye alikuwa akitokwa na jasho baridi na maumivu, Lisa alikuwa mwisho wa akili yake.
“Kichwa kinamuuma, kwa hiyo ninamdunga sindano ili kumpunguzia maumivu,” Chester alijibu bila kujali.
“Kwanini uko hapa? Ondoka." Alvin alimkazia macho.
Lisa alikunja ngumi kwa hofu na hasira. Hakutarajia kwamba Alvin sasa alilazimika kutegemea sindano ili kukabiliana na maumivu ya kichwa. Kwa maana hiyo hali yake ilikuwa mbaya zaidi? Hofu ilizidi kutanda ndani yake.
"Siondoki." Lisa akamsogelea. Alipoona kiganja chake kikitetemeka, alisita kwa muda kabla ya kukishika.
Kope za Alvin zilitetemeka. Akainamisha kichwa kumtazama. Mwanamke huyo ambaye alikuwa amevalia pajama nyeupe, alikuwa akichuchumaa kando yake. Muda ulikuwa umepita tangu awe mpole na mwenye upendo kwake namna ile. Akaurudisha mkono wake nyuma na kufumba macho.

Sura ya: 269

Dakika 20 baadaye, zoezi la sindano lilikamilika. Chester akamtahadharisha. "Jitahidi kupata muda wa kupumzika zaidi na pia usikasirike hovyohovyo. Nimewasiliana na Dokta Nyasia amesema atakuja wiki ijayo. Ni yeye pekee anayeweza kutibu ugonjwa wako.”
“Ok!” Alvin alijibu kwa unyonge.
Chester alimtupia jicho Lisa na kumuuliza Alvin, “Unahudhuria mazishi ya Maurine Jumapili hii?”
Alvin alishindwa cha kusema.
"Afadhali uhudhurie, au Rodney ataendelea kukulaumu." Kwa hayo, Chester alisimama na kujiandaa kuondoka. “Naondoka sasa hivi.”
"Subiri." Lisa alisimama. "Nina kitu cha kuwaonyesha nyie."
Akabofya rekodi ya simu ya Linda na kuwasikilizisha. "Hii ilitokea wakati Pamela alipoenda hospitalini huko Dar es Salaam kupata ripoti ya uchunguzi wa DNA ya Maurine na Jones. Mwanamke anayeitwa Linda alikutana na Pamela akiwa idara ya uchunguzi wa vinasaba. Linda alisikia mazungumzo yetu wakati Pamela aliponipigia kunipa matokeo, kisha akampigia Lina. Inawezekana kuwa Lina alipofahamu ishu hiyo, haraka akamrudisha Maurine Langa halisi na yeye akatoweka—'”
“Unamaanisha nini?” Chester alikatiza sentensi yake kwa sura ya huzuni.
“Lina ndiye aliyejifanya Maurine Langa, na kuna mtu aliyemtengeneza kwa makusudi. Inawezekana alitoroka baada ya kupokea simu ya Linda, akamrejesha Maurine halisi. Alishuku kuwa nilitumia nywele zake kufanya kipimo cha DNA na Jones. Alijua kuwa tayari nimeanza kushuku kuwa yeye sio Maurine wa kweli, kwa hivyo Alvin alipoenda kumshika, tayari alikuwa ametoka kwa ujanja na kumrudisha Maurine halisi. Ikiwa huniamini, unaweza kusikiliza hii simu kutoka kwa Linda…”
“Sikukuambia sitaki kusikia tena jambo hili?” Alvin akauachia mkono wake, huku macho yake yaliyokuwa na huzuni yakionyesha ukali kwa namna fulani.
Lisa alitamani Alvin amwelewe, lakini alishindwa amwelewesheje. “Lakini inatia shaka. Hebu nyie angalieni—”
“Inatosha. Usiongelee tena kuhusu hilo.” Chester alikatiza hotuba yake kwa mshtuko. “Wewe ndiye uliyemtaka Alvin achunguze hivyo akamfungia Maurine. Kwa sababu hiyo, Maurine alipoteza maisha.”
Chester alikuwa na fikra nzuri kwa Lisa kabla ya hii. Hata hivyo, kwa vile alikuwa amechangia kifo cha Maurine, Alvin, Chester, na Rodney sasa walikuwa na maelewano mabaya kati yao. Hii ilikuwa imemweka Chester katika hali mbaya.
"Mkipuuza mambo haya ya kutiliwa shaka, muuaji aliye nyuma ya pazia atapata upenyo wa kuponyoka. Charity pia ni binadamu. Ikiwa kweli alifanyiwa njama na mtu, maisha yake yataharibiwa vile vile. Baada ya yote, yeye ni ex wako, Chester…”
“Ninachojutia na kuchukizwa zaidi ni kuwa pamoja na mwanamke huyo asiyefaa,” Chester alisema kwa uwazi, “Amekuwa hafai tangu nilipokutana naye.”
Lisa alihisi kana kwamba ametumbukizwa kwenye dimbwi la maji baridi. Kwanini watu hawa walikuwa wakaidi sana?
“Ulikuja kunitafuta kwa sababu tu ya jambo hili, sivyo?” Alvin alimtazama kwa hasira.
"Alvin, nakuomba..." Lisa alimtazama kwa kumsihi. “Kuchunguza rekodi ya simu ni jambo dogo tu..."
“Toka nje.” Alvin alielekeza nje. "Sina muda wa kupoteza na upuuzi wako." Alvin alikasirishwa na maneno yake alipomuelekeza nje. Kichwa chake kilianza kumuuma tena.
“Lisa, wewe ni mke wake. Kuwa mstaarabu kwa sasa! Usimkasirishe kwa ajili ya watu hao wasio na maana.” Chester alikasirika. "Hans, mwondoe."
“Samahani, Bibi Mdogo.” Hans akamkokota kuelekea mlangoni.
Wakati Lisa alitaka kurudi tena ndani ya jengo hilo, tayari Hans alikuwa ameshafunga lango. Hakuweza hata kumuona Alvin sasa. Ni lini Alvin na uhusiano wake walifikia hatua hii?
Sebuleni, Chester alimkumbusha Alvin, “Afadhali usikutane na Lisa kwa muda kuanzia sasa kwa faida yako, mpaka Dokta Nyasia atakapokuja. Siku zote nyie wawili mnashindwa kuelewana mkionana macho kwa macho na hatimaye mnaishia kugombana. Hali yako inazidi kuwa mbaya kila unapokutana naye.”
“Mm. Alvin akalipapasa paji la uso wake. Pengine ndiye angehisi kuumia zaidi ikiwa asingemwona. Baada ya yote, ni Lisa ndiye alitaka kumuona kwanza.
•••
Jumapili. Mbele ya chumba cha mazishi.

Wakiwa wamevalia suti nyeusi, Alvin na Chester walitoka kwenye gari na kuingia kwenye chumba cha maombolezo. Hawakugundua kuwa kuna mtu alikuwa akiwatazama kwa sura ya ushindi ndani ya gari jeusi lililokuwa mbali kidogo. Alikuwa Lina Jones, ambaye aliweza kukimbia.
‘Hehe. Kwa bahati nzuri, nilimrudisha Maurine kwa siri mapema. Nyinyi watu hamkuweza kamwe kufikiria kwamba nimekuwa nikimwiga Maurine Langa, sivyo?' Lina alijiwazia kwa furaha. Alitabasamu kutoka sikio hadi sikio. 'Alvin, Lisa, fikirieni juu ya madhara yote ambayo nyie mmenisababishia. ‘Season two’ bado itaendelea hadi nihakikishe nawapeleka kuzimu!'
“Umefanya kazi nzuri,” mwanamume aliyeketi kwenye kiti cha abiria alisema bila huruma, “Maurine amekufa, lakini Charity yuko jela. Zaidi ya hayo, Alvin, Lisa, na Rodney wako katika mzozo. Kila kitu kimekwenda vizuri zaidi kuliko vile nilivyofikiria."
Lina akajigusa usoni. “Baada ya kusema hivyo, uso huu hauwezi kutumika kwa sasa…”
“Nenda nje ya nchi ukampumzike kwa sasa. Bado utakuwa na kazi fulani.” Mwanaume huyo alipiga vidole vyake na kumtaka dereva awashe gari.
Alvin alipofika mlangoni ghafla aligeuka nyuma na kuliona lile gari jeusi likiondoka.
"Nini tatizo?" Chester aliuliza.
Alvin alikunja uso. "Ilionekana kama kuna mtu alikuwa akitutazama sasa hivi."
"Kipi cha ajabu, si kawaida kwa watu kukuangalia?"
"... Twende." Alvin akageuka.
Alipoingia tu ndani ya chumba kile, alikutana na Rodney ambaye alikuwa akitoa heshima zake. Rodney alitazama kando baada ya kumpiga Alvin jicho kali la kuchoma.
Chester alienda mbele kutoa heshima zake, huku Alvin akienda mbele na kuomboleza kifo cha Maurine kimya kimya.
Bi. Langa alisema kwa uwazi, “Bwana Kimaro, fanya haraka na uondoke mara baada ya kutoa heshima kwa Maurine. Kwa kuzingatia hali halisi, hapa si mahali unapopaswa kuwepo.”
Alex Langa Njau, baba mzazi wa Maurine, alipandwa na hasira pia. Lakini alipotaka kuongea tu, aliona sura ya mwanamke akiingia ndani. Alex akaganda, akabaki kutetemeka. Alitamani kukimbia lakini alihisi kama miguu yake imeota mizizi pale alipokanyaga. Haja kubwa na ndogo vyote viligonga hodi kwa wakati mmoja. Macho yake yalimtoka hadi mwisho kama yanayotaka kuchomoka kwenye soketi zake…
“Kuna nini? Mbona ume...” Bi. Langa alipogeuka na kutazama upande ule, alishtuka sana hadi akaanguka chali, akatua chini na kuzimia papo hapo.
Rodney, Chester, na Alvin walipigwa na butwaa kabisa. Wakageuza vichwa vyao na kutazama upande ule kwa wakati mmoja. Kila mmoja alichukua njia yake na kukimbia baada ya kumwona mwanamke aliyekuwa nyuma yao.
Walimwona mwanadada aliyevalia gauni jeusi lenye umbo dogo lililoangazia mwili wake mdogo. Nywele zake zilikuwa zimefungwa kwa upole, huku uso wake mzuri na wenye kung'aa ukipakwa vumbi la unga fulani. Huku taa nyeupe zikimulika usoni mwake safi, alionekana kustaajabisha kama mzimu.
Sigara aliyokuwa ameishika Rodney ilidondoka chini. Chester alipepesa macho yake pande zote kwa mshangao.
Alvin ambaye alikimbia na kusimama kwenye kona ya chumba, alijikaza na kumtazama yule mwanamke aliyemfahamu vyema na kumsogelea taratibu.
“Sa-Sarah… Sarah ni wewee…” Maneno hayo hatimaye yalimtoka kwa shida bila kujifahamu. “Sa-Sarah, wewe ni mzimu?”
“Umetumwa leo kuja kumchukua Maurine?” Rodney aligugumia kwa macho yasiyoamini.
Sarah alitoa tabasamu hafifu huku akimwangalia. "Rodney, bado una utani wako kama zamani?"
Chester hakuweza kujizuia kuuliza kwa fadhaa, “Sarah, si tayari umekufa? Mbona…”
“Samahani, niliwahadaa. Kwa kweli, bado niko hai, lakini…sikuweza kurudi kwa sababu ambazo siwezi kuzisema kwa sasa.” Mwonekano wa kukata tamaa na kutojiweza kihisia ulivuka uso wake mzuri.
“Ni nini kilikuzuia kurudi?” Rodney aliuliza kwa wasiwasi, “Unajua kwamba kila mtu anajua umekufa? Kwa miaka hii, tulivunjika moyo kabisa, hasa Alvin. Karibu avunjike…”
Alvin aliendelea kukaa kimya kama bubu huku akipigwa butwaa.
Sarah alimtupia jicho huku machozi yakimtoka. "Samahani, nilikuwa na sababu zangu za kutorudi."
"Ni kwanini ulilazimika kudanganya kifo chako huko nje ya nchi kwa miaka yote hii na usitake kutujulisha?" Rodney aliuliza kwa hasira.....ITAENDELEA..

Unafikiri nini kitafuata hapo, maana simulizi inazidi kuwa tamu kila siku lakini sina budi kuhitimisha kipande hiki ila niwasihi tukutane katika episode zijazo ili kujua nini kitafuata kwenye mkasa huu wa kusisimua na kuelimisha unaokwenda kwa jina la LISA.