JINA LA SIMULIZI............................LISA
AUTHOR...........................JOMBA WAJO
SPONSORED BY......SIMULIZI ZA DULLY
WHATSAPP..........................0628924768
SEHEMU YA................................266-267

Sura ya: 266

Baada ya kukata simu, Lisa aliendelea kumtafuta Alvin bila mafanikio, hatimaye akampigia simu Hans. Hans alipokea baada ya kuita kwa muda mrefu. "Bibi mdogo, kuna nini, mbona una wasiwasi sana?"
“Mbona Alvin hapokei simu zangu?”
"Bwana Kimaro yuko ... kwenye mkutano."
“Tangu jana, na juzi hapokei simu zangu,” Lisa alisema kwa hasira, “Mwambie arudi nyumbani jioni, au… Au nitaenda kwake badala yake.”
“Bibi mdogo usiwe na wasiwasi, Kimaro ana shughuli nyingi…”
“Ana shughuli gani zinazomfanya asifike nyumbani kwa siku kadhaa na hapokei simu zangu? Au labda amepata mwanamke mwingine tena?" Lisa alicheka kwa kejeli.
“Hapana, Bwana Kimaro amebanana tu na shughuli nyingi” Hans, akihisi maumivu ya kichwa yakimjia.
Saa nane usiku, Lisa alipokea tena simu kutoka kwa Pamela. "Charity alikamatwa na polisi. Walisema alikodi watu wa kumuua Maurine Langa. Baba yake alipatwa na mshtuko wa moyo na kupelekwa hospitalini. Mama yake anatafuta msaada kila mahali lakini hakuna aliye tayari kumsaidia. Uvumi umeenea kwamba familia za Kimaro, Choka, na Shangwe zilitoa agizo. Yeyote atakayethubutu kumwokoa Charity Njau watashughulika naye.”
“Inawezaje kuwa hivyo?” Lisa alihisi kama ubongo wake unaweza kulipuka. "Maurine Langa amekufa?"
“Ndio. Maurine Langa ameteketea kwa moto" Pamela alisema, “Niko hospitalini na wazazi wake sasa. Wanatia huruma sana. Ndugu zao wote wanawakwepa sasa, na watumishi wao wote pia wamekimbia. kampuni yao pia ina hatihati ya kufilisiwa.”
"Naenda kumtafuta Alvin." Kichwa cha Lisa kilikuwa kimekufa ganzi.
Hakuweza kusubiri hadi kupambazuke. Aliendesha gari moja kwa moja hadi getini, lakini mlinda mlango alikataa kumfungulia geti.
"Bibi mdogo, huwezi kutoka peke yako bila ruhusa ya Bibi au Mzee Kimaro." Mlinda mlango akatazama pembeni.
“Fungua. Lazima nitoke nje leo. Naenda kutamtafuta Alvin.” Lisa hakuwa na subira tena. "Usipofungua milango, nitagonga."
“Usifanye hivyo! Tulia." Mlinda mlango huyo alikuwa amefikia mwisho wa akili yake wakati gari nyeusi aina ya BMW lilipoingia ghafla na Alvin akatoka ndani yake.
“Bwana Kimaro, afadhali umefika kwa wakati. Bibi mdogo alikuwa anataka kwenda kukutafuta." Mlinda mlango akafanya kama amemwona mwokozi wake.
Lisa alikaa kwenye gari akiwa ameegemea usukani. Alvin aliposogea kwenye dirisha la gari, alimuona akiwa bado amevaa nguo za kulalia za pinki. Katika kipindi hicho, watumishi walikuwa wakimhudumia chakula na vinywaji vyenye lishe kwa wingi, kwa hiyo ngozi yake ilikuwa ikipendeza zaidi kuliko hapo awali.
"Nimerudi. Hebu tuingie ndani.” Alvin alifungua mlango na kumshusha kutoka kwenye gari.
“Alvin, niache!” Lisa alilalamika. “Nataka kukuuliza hivi ni kweli Charity alimuua Maurine Langa? Siamini kama anaweza kufanya hivyo, hizi ni njama tu mnamfanyia. Kwanini mnakuwa makatili hivi kwa kumuonea mwanamke asiye na hatia?”
Alvin alikaa kimya na kumbeba hadi ndani na kumuweka taratibu kwenye sofa.
“Alvin, umesikia nilichosema? Kwanini mnampakazia Charity kesi ya mauaji kisha Rodney anamfukuza kazi Pamela na kumweka kwenye blacklist? Wote ni marafiki zangu. Walifanya kosa gani?" Lisa alishindwa kujizuia na kusimama. “Vipi kuhusu Maurine Langa? Nilikuambia kuwa yeye ni Lina Jones. Nini kingine unahitaji kufanya ili uamini?"
"Lisa nyamaza." Uso mzuri wa Alvin ulionyesha jeuri fulani. "Umedanganywa na Charity tangu mwanzo."
“Sikudanganywa, Lina ndiye Maurine…”
“Jionee mwenyewe.” Alvin alitoa ripoti mbili mikononi mwake. "Moja wapo ni ripoti ya uchunguzi wa nywele, ambapo nyingine ni ripoti ya uchunguzi wa maiti ya Maurine. “Haya yote yanathibitisha kuwa yeye ni mtoto wa familia ya Alex Langa Njau. Daktari amemchunguza uso wake na kugundua kuwa hajawahi kufanyiwa upasuaji wa plastiki. Yeye ndiye Maurine halisi. Charity amekuwa akikudanganya.”
Lisa mara moja akapitia taarifa hizo. Mara tu alipoona maneno yaliyoandikwa juu ya ripoti hiyo, kichwa chake kilikaribia kulipuka.
“Hii haiwezekani. Charity asingeweza kunidanganya.” Alitikisa kichwa akiwa haamini.

“Nadhani utakuwa umepumbazwa naye. Umemjua kwa muda gani? Kwa nini unataka kumwamini Charity kuliko mimi? Nimekuambia kwa muda mrefu kuwa huyo mwanamke hafai, si mtu mzuri.”
Tabia yake ya ukaidi ilianza kumfanya Alvin kupandwa na hasira. “Nilikusikiliza na kumfungia Maurine, lakini Charity baadaye aliagiza watu wachome moto nyumba na kumteketeza Maurine hadi kufa. Aliyewasha moto huo amejulikana, na ni mtu ambaye alitekeleza maagizo ya Charity.”
Lisa alirudi nyuma na kukaribia kujikwaa kwenye kochi bila kujijua. Alvin alishika kiuno chake kwa haraka na kumwonya kwa upole, “Jihadhari Lisa. Una mimba sasa…”
Kabla hajamaliza kusema, Lisa alimsukuma. “Nina uhakika Maurine ni Lina. Nilipokutana naye mara ya kwanza, nilimfahamu vizuri…”
“Acha kung’ang’ana Lisa. Unamuonea wivu Maurine tu, ndiyo maana unatoa visingizio vya kila aina kuunga mkono madai yako kuwa yeye ni Lina.” Macho yenye huzuni ya Alvin yalidhihirisha hali ya kukata tamaa. “Mbona huniamini? Kwanini unaelemewa kirahisi hivi na wivu na kulaghaiwa na Charity? Sasa kwa kuwa Maurine amekufa, wazazi wake wamepoteza binti. Je, huoni hatia hata kidogo?”
“Hivi ndivyo unavyoniona?” Lisa alianguka katika hali ya kukata tamaa kabisa. “Kwanini na wewe huniamini, basi? Jambo hili sio rahisi kama inavyoonekana. Pia, Pamela amefanya nini?"
“Hakufanya lolote. Ulimwomba akusaidie kupima DNA paternity, na kitendo hicho kilimkasirisha Rodney,” Alvin alijibu bila kujali, “Unapaswa kujisikia mwenye bahati kwa kuwa upo na mimi. Vinginevyo, Rodney angekufanya kitu kibaya sana. Angeiharibu kabisa Mawenzi Investments.”
Sura ya Lisa ilipwaya kabisa. Je, hii ilimaanisha kwamba Pamela alifukuzwa kazi na kuwekwa kwenye blacklist kwa sababu tu alikuwa amemkosea Rodney? Charity alipakaziwa kesi kwa kuwa alimshtukia Maurine Langa feki? Na Lisa alipona tu kwa sababu ya Alvin? Alitazama huku macho yake yakiwa yametua kwenye uso wa Alvin, hakutaka kuamini kabisa alichokisema. Ni lini watu hao kama Alvin na Rodney walianza kufikiria kuwa wanaweza kumwangamiza mtu yoyote bila kujali hadhi yake?
"Ni kosa langu," Lisa alinong'ona kwa macho mekundu ghafla. "Sikupaswa kukutongoza nilipokuona pale baa kwa mara ya kwanza."
Ikiwa asingemtongoza, asingeolewa naye, na asingeingia kwenye matatizo yote yale.
"Lisa, unajua unachosema?" Alvin alikasirishwa na tabia yake ya dharau. Anawezaje kujuta kuolewa naye kwa sababu watu hao?!
Je, Charity na Pamela walikuwa muhimu kuliko yeye? Alikuwa mume wake, wakati wao walikuwa ni marafiki zake tu.
“Utawasaidiaje Charity na Pamela? Ni marafiki zangu.” Lisa alimsihi huku machozi yakimtoka bila kujizuia. Alifahamiana na Pamela tangu wakiwa shule ya sekondari. Pamela alikuwa kando yake licha ya magumu aliyopitia miaka yote hiyo.
“Siwezi kuwasaidia.” Alvin hakujisikia tena kubishana na Lisa. Akageuka na kuondoka.

Sura ya: 267

"Nakuchukia, Alvin." Lisa alitokwa na machozi.
“Pumzika vizuri. Usirudi ofisini kwa sasa. Nitashughulikia kila kitu kinachohusiana na Mawenzi Investments kwa niaba yako hadi utakapojifungua watoto hao wawili.” Alvin hakuwa na la kufanya zaidi ya kusema hivyo bila kupenda kwani alishindwa kuvumilia kumuona akilia. Kwa hayo, akapiga kisigino na kutembea kuelekea getini.
“Simama…” Lisa alitaka kumfuata, lakini Hans alimzuia. “Bi Kimaro, bora uache kubishana na Bwana Kimaro. Kwa sababu yako, uhusiano wake na Rodney Shangwe umegeuka kuwa mbaya hivi karibuni. Wazazi wa Maurine pia walikuja kumlaumu Alvin kwa kifo cha binti yao, ana huzuni sana kwa sasa na huenda hali ya ugonjwa wake ikawa mbaya tena.”
Lisa alisimama na kuuliza kwa mshangao, "Hans, ni kweli maiti ni ya Maurine?"
“Ndio. Madaktari waliofanya uchunguzi wa kitaalamu na kipimo cha DNA ni waaminifu sana kwa Alvin, kwa hivyo matokeo hayawezi kuwa na makosa. Hakika ulikosea, Bi Kimaro.”
Inawezekana kweli alikosea? Alvin alidai kuwa Charity amekuwa akimdanganya, lakini Lisa mwenyewe alihisi kwamba Maurine alionekana kufanana na Lina, hasa macho yake na tabia zake fulanifulani.
Kwanini taarifa alizozipata Alvin zilipingana na za Pamela? Kwanini za Pamela zilionyesha kuwa ni Lina na za Alvin zilionyesha kuwa yeye ndiye Maurine halisi?
Je, inawezekana kwamba Lina, ambaye alikuwa akijifanya kuwa Maurine, alimrudisha Maurine halisi baada ya kujua kwamba Lisa alikuwa ameujua ukweli? Baada ya yote, ikiwa Lina angejifanya kuwa ni Maurine, basi walipaswa kumteka kwanza Maurine halisi ili mchongo wao usishtukiwe. Moyo wa Lisa ulishtuka sana.
Kadiri Lisa alivyozidi kuwaza kuhusu jambo hilo, ndivyo alivyoona kuwa inawezekana. Alimpigia simu Pamela mara moja. “Ulipofanya kipimo cha DNA, uligongana na mtu yeyote? Inawezekana kwamba suala hilo lilistukiwa?”
“Ulinisisitiza niwe makini. Kwa kawaida, sikumwambia mtu yeyote, isipokuwa wakati wa kupata nywele za Jones. Nilimwomba kaka yangu msaada kwa hilo. Hata hivyo, unajua tabia ya kaka yangu, sivyo? Hatuwezi kumtilia shaka.”
Lisa alikunja uso kwa kuchanganyikiwa. Kwa kweli, alimwamini sana Forrest. "Hakuna mtu yeyote aliyekuona kwenye idara ya uchunguzi, kama mtu yeyote ambaye alikuwa karibu na Lina?"
'Sidhani hivyo… Nilipoenda kuchukua ripoti hospitalini, nilikutana na wapenzi wasio na haya, Patrick na Linda. Siku hiyo Patrick hakujisikia vizuri, hivyo Linda akampeleka hospitali.”
“Linda?” Lisa alinong'ona baada ya kusikia hilo, "Inawezekana yeye ndiye aliyeunguza picha. Lina alikuwa na marafiki wengi matajiri wa kike huko Dar es Salaam alipokuwa bado kwenye chati, na pia Linda alihudhuria hata sherehe ya uchumba ya Lina na Ethan akiwa na Patrick. Ni rafiki mkubwa wa Lina.”
“Unashuku anaweza kuwa Linda?” Pamela alipigwa na butwaa.
“Mwambiye kaka yako afanye uchunguzi ili kujua ikiwa Linda alipiga au kupokea simu yoyote siku hiyo mlipokutana naye hospitali.”
Lisa alimweleza Pamela kilichotokea baada ya yeye kumtumia ripoti yake, jambo ambalo lilimfanya ashangae. "Unashuku kuwa Lina aligundua kuhusu hilo, ndiyo sababu wakabadilisha haraka na kumrudisha Maurine halisi?"
"Ndio. Mtu aliye nyuma ya tukio hili ametufanya sote tuanguke kwenye mtego wake. Kwa sababu yake, uhusiano wangu na Alvin unaanza kuvunjika. Pia amesababisha uhusiano wa Alvin na Rodney kuwa mbaya. Hata familia ya Njau sasa iko kwenye kona kali huku Charity akiwa jela.”
“Charity ndiye anayeteseka zaidi. Huenda akakaa gerezani milele licha ya kuwa hajafanya kosa lolote,” Pamela alinung’unika, “Ingekuwa bora nisimjue aliyefanya hivyo, au nitamuua bila shaka.”
"Kwa maana hiyo, Lina atakuwa ametoroka. Sijui ameenda wapi,” Lisa alisema huku akitabasamu kwa uchungu.
"Ni nyota ya ajabu." Pamela alikasirika. Baada ya kukata simu, alipanga kurudi Dar es Salaam kwa ndege ya mapema zaidi.
Ndege ilipotua tu, alipokea rekodi za simu ya Linda kutoka kwa Forrest, kaka yake. Baada ya kuzichambua, alipata rekodi ya simu ambayo Linda alipiga kwenda kwa Lina siku hiyo walipokutana hospitalini.

Hata hivyo, kila kitu kilikuwa sawa na matarajio ya Lisa. Linda ndiye aliyebumbulua mchongo mzima. Alikuwa ni Linda ambaye alisababisha Lina amfanyie njama ya kesi ya mauaji Charity.
Akiwa amesimama kwenye uwanja wa ndege, Pamela alihisi kizunguzungu. Moja kwa moja akaelekea kwenye kampuni ya Patrick bila hata kujua aliisimamishaje teksi.
Linda alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya Patrick wakati huo. Pamela mara moja alipanda ghorofani baada ya kufika. Linda, ambaye alikuwa amevalia maridadi, alipigwa na butwaa mara tu alipomwona. “Pamela, nini kinakuleta hapa? Unamtafuta Pat—”
“Ninakutafuta wewe.” Pamela alipiga pande zote mbili za uso wa Linda mara moja. Kwa muda mrefu Pamela alikuwa akitaka kufanya hivyo, lakini alikuwa akiungojea tu muda muafaka.
Hata hivyo, sasa…
Kwa sababu ya Linda, Charity alienda jela.
Kwa sababu ya Linda, Alvin hakumwelewa Lisa.
Kwa sababu ya Linda, Rodney alimfukuza kazi na kumweka kwenye blacklist.
“Linda, ningeweza kukuvumilia kama ungefanya kitu kingine chochote, lakini hukupaswa kuwasiliana na Lina. Ulimwambia nini? Umetuweka kwenye kona kali!”
Kwa kuzingatia sura yake ndogo, Linda ni wazi hakuweza kurudisha mapigo ya Pamela. Muda si muda, uso wake ukavimba.
Kwa bahati nzuri, baadhi ya watu katika kampuni walikuja kumtoa Pamela nje. Kila mtu alijua kuwa Pamela hapo awali alikuwa mpenzi wa Patrick, kwa hivyo hawakuthubutu kumvuta kwa nguvu. Mwishowe, ikawa kwamba Linda aliumizwa kabisa.
"Niache, Pamela! Sijui hata kidogo unachokiongelea.” Linda alihisi kana kwamba ngozi yake ya kichwa itnachunika kwa nguvu.
“Acha kujifanya mbele yangu. Nionyeshe simu yako na tutaweka kila kitu wazi. Nina uhakika huwa uliwasiliana na Lina kupitia WhatsApp.”
Pamela alipounyanyua mguu wake ili ampige teke Linda, sauti ya Patrick ilisikika nyuma yake ghafla. "Unafanya nini Pamela?" Alimsukuma Pamela akaanguka chini.
Patrick alimvuta Linda mara moja. Akiwa na nywele chafu na uso uliovimba, Linda alianguka mikononi mwake mara moja. "Patrick, nimeumiaaa!"
"Samahani kwa kuchelewa." Baada ya kuona mikwaruzo kwenye ngozi ya Linda, Patrick alizidi kung'aka kwa Pamela. “Pamela, angalia jinsi ulivyo mkorofi sasa. Nilipokuja kukutafuta huko Nairobi, ulinionyeshea jeuri mbele ya mwanamume mwingine. Sasa, umekuja ofisini kwangu kumpiga Linda bila sababu. Unafikiri sina ujasiri wa kukufanyia chochote?”
"Mambo yangu hayakuhusu." Pamela akauma meno na kusimama. “Najuta kabisa kukufahamu Patrick. Kama nisingewafahamu, msingenipeleleza pale hospitali juzi .”
“Sijui unasema nini. Hata hivyo, lazima uombe msamaha kwa Linda sasa hivi, au nitapiga simu polisi.” Maneno yake yalimkasirisha sana Patrick.
“Niombe msamaha? Haha. Ninajilaumu kwa kutokuwa mkatili vya kutosha. Nitampiga makofi kila nitakapomuona Linda!” Pamela alishindwa kujizuia na kupiga kelele.
Huku akitetemeka kwa hasira, Patrick akatoa simu yake kuwapigia polisi, lakini Linda akamzuia mara moja. “Usiwaite polisi. Pamela labda ana wivu tu—”
'Kuna kikomo cha wivu. Angalia, haonyeshi hata kujutia makosa yake. Nani anajua kama atakupiga tena?” Patrick aliongea kwa unyonge huku akiwa ameweka uso wa wasiwasi.
"Bwana Jackson, unamtetea sana mfanyakazi wako, huh?" Forrest, ambaye alikuwa mrefu na mwenye umbo lenye nguvu, ghafla alimsogelea. Macho yake meusi yalikuwa mazito kwa huzuni. “Upo radhi mpenzi wako wa zamani, ambaye ulikuwa na uhusiano naye kwa miaka minane, apelekwe kituo cha polisi kwa ajili ya mwanamke huyu. Si ajabu kwamba Pamela alichagua kutokuwa nawe.”
Wafanyakazi waliokuwa karibu nao walianza kunong’onezana wao kwa wao.
"Si ajabu kwamba Pamela alikasirika. Inawezekana kwamba Bwana Jackson alimsaliti kwa Linda?”
"Ina maana kwamba Pamela amesalitiwa?"
“Hilo linawezekana. Ninawaona wakiwa pamoja mara nyingi sana.”.....ITAENDELEA.....

Unafikiri nini kitafuata hapo, maana simulizi inazidi kuwa tamu kila siku lakini sina budi kuhitimisha kipande hiki ila niwasihi tukutane katika episode zijazo ili kujua nini kitafuata kwenye mkasa huu wa kusisimua na kuelimisha unaokwenda kwa jina la LISA.