JINA LA SIMULIZI............................LISA
AUTHOR...........................JOMBA WAJO
SPONSORED BY......SIMULIZI ZA DULLY
WHATSAPP..........................0628924768
SEHEMU YA................................260-261

Sura ya: 260

“Kuwa mpole. Huu ni wakati muhimu katika maisha yetu. Ni kwa ajili ya watoto wetu waliomo tumboni.” Alvin alimnyanyua na kumsaidia kuweka pedi.
Wakati wa mchakato mzima, Lisa alitaka kuvunja kichwa chake na kujiua kwa aibu. Aliporudi kitandani, uso wake wote ulikuwa umetapakaa aibu.
Alichukukua kisu na kutaka kula tunda moja, lakini Alvin aliinuka tena palepale aliposhika kisu ili kukata tunda. "Kaa chini, nitakumenyea.”
Kwa kifupi, Alvin alikaa wodini mchana na usiku, siku nzima. Lisa hakuruhusiwa kugusa chochote. Alichowezaa kufanya ni kukaa na kulala tu. Vingine vyote alifanyiwa na Alvin
Kwa sababu ya kulala sana, Lisa aliamka saa kumi na mbili asubuhi siku iliyofuata. Alipofumbua macho alimkuta Alvin amelala kwenye mto wake. Hakujua ni saa ngapi alibanana naye jana usiku. Hasira yake iliwaka alipokumbuka taswira ya jinsi Maurine alivyomshika mkono jana yake. Hata hivyo, sura safi ya Alvin alipokuwa amelala ilipendeza zaidi machoni kuliko alipokuwa macho.
Kope zake zilikuwa nene kama mbawa za kipepeo, ngozi yake haikuwa na vinyweleo, na macho yake, pua na midomo vyote vilipendeza sana. Vipengele vyake vilionekana kama kazi ya sanaa iliyoundwa kwa uangalifu na Mungu…
Alipokuwa akitafakari, macho meusi ya Alvin yakafunguka ghafla. Lisa aliogopa na kumpiga teke bila fahamu. "Ni nani aliyekuruhusu kupanda hapa jana usiku?"
Alvin alikaa kwa uchungu na kutazama huku na kule. Kulikuwa na mwanga wa kuchanganyikiwa katika macho yake. “Hii si hospitali? Mbona unavaa scrubs?"
Moyo wa Lisa ulizama mara moja. Ndani ya siku mbili walizokaa pamoja, alihisi kumbukumbu ya Alvin inazidi kuwa mbaya. Hata hivyo, hakutarajia kwamba angesahau kwamba alikuwa mjamzito baada ya kuamka. Hata kumbukumbu ya mzee wa miaka 80 isingekuwa mbaya kiasi hicho.
"Ni sawa ikiwa hukumbuki." Alishuka kutoka kwenye kitanda cha hospitali ili kuosha uso wake na kupiga mswaki.
'Niambie. Ni nini kilikupata? Una tatizo lolote?" Alvin alimkimbilia na kumshika mkono.
Shangazi Yasmine aliyekuwa amelala chumba jirani alisikia makelele hayo hiyo na mara moja akaamka kwenda kuwaangalia.
“Bibi mdogo, unataka kula nini kwa kifungua kinywa?”
"Sijisikii chochote."
“Haiwezekani. Unabeba watoto wawili wadogo tumboni mwako sasa hivi. Huwezi kuwa mzembe.” Shangazi Yasmine alitafakari huku akitabasamu. “Nitakupikia uji wa mtama—”
“Ulisema nini? Ana mimba?” Alvin alifoka kwa furaha.
Aunty Yasmine akanyamaza na kumwangalia Alvin kiajabu. “Bwana Kimaro, umesahau? Ulifurahi sana jana na hata siku nzima ulisoma vitabu vya kulea ujauzito."
Alvin aliganda kabisa. Kwanini hakuweza kukumbuka hata kidogo? Alitaka kufikiria zaidi, lakini ubongo wake ulianza kumuuma. Alifunika kichwa chake kwa mikono miwili. Alikuwa na maumivu makali sana hata akashindwa kusimama.
Lisa alimtazama Aunty Yasmine. "Mwambie daktari anayemhudumia aje."
Punde, Daktari Melisa na Dokta Chester walikusanyika kufanya uchunguzi wa kina juu ya Alvin. Dakika kumi baadaye, Daktari Melisa alisema kwa maneno mazito, “Hii ni dalili ya kupoteza kumbukumbu. Sikutarajia hali yake kuwa mbaya haraka hivyo, Bwana Kimaro.”
Alvin hakuweza kukubali. "Lakini nimekuwa nikinywa dawa na kwenda kwa dripu ya IV kila siku. Kwanini haifanyi kazi hata kidogo? Je, unafanya kazi yako ipasavyo? Haufai.”
Daktari Melisa alishtuka kwa aibu kutokana na karipio hilo. "Sielewi kwa nini hii inatokea pia. Nilijaribu niwezavyo…”
“Sawa, Alvin, tulia. Daktari Melisa ndiye mtaalam bora katika uwanja huu nchini,” Chester alizungumza.
“Ninapaswa kutulia vipi? Sikuweza hata kukumbuka kuwa mke wangu ni mjamzito. Je, inawezekana kesho sitamtambua mke wangu?” Uso wa Alvin ulionyesha kukereka. Midomo ya daktari Melisa ikasogea lakini hakusema chochote kwa muda mrefu.
Hata hivyo, Alvin angeweza kukisia kwamba alikuwa sahihi. Alikaa kwa hasira na kuvivunja vitu vilivyokuwa kwenye meza ya kitanda.
"Alvin, tulia." Chester na Daktari Melisa walikuja mbele kujaribu kumzuia, lakini Alvin akawasukuma mbali.
Lisa aliuma mdomo na kwenda mbele. "Alvin Kimaro, unajaribu kuwatisha watoto wako tumboni mwangu?"

Alvin aliganda na kulitazama tumbo lake huku akikunja ngumi kwa maumivu. "Mimi ni mgonjwa. Labda hata nisingewatambua kama wangesimama mbele yangu katika siku zijazo.”
“Hilo halitatokea. Tayari nimepata habari kuhusu Nyasia, mtaalamu wa saikolojia. Maadamu tutampata, tuna njia ya kukuponya.” Chester akampiga bega. "Nijuavyo, hakuna ugonjwa ambao Nyasia hawezi kutibu."
Macho ya Alvin yalififia. Hilo lingeweza kuwa tumaini lake pekee. “Lisa, usijali kuhusu mimi. Nenda kitandani ukapumzike.”
Lisa aliitikia kwa kichwa na kurudi wodini kwake. Chester alimfuata muda si mrefu. “Lisa, najua kwa sasa haujaridhika na Alvin, lakini pia unaifahamu hali yake ya sasa. Natumai utaacha kugombana na Alvin kwa muda huu. Ni kwa ajili yake na kwa ajili ya watoto.”
"Utasema kwamba ninaweza kuathiri hisia zake na kwamba hali yake inayozidi kuzorota inahusiana nami, sivyo?" Lisa bila fahamu alihisi kuchanganyikiwa na jinsi mtu huyu alivyokuwa akiuweka ugonjwa wa Alvin juu yake. Ni kana kwamba alikuwa akimwomba avumilie ingawa alionewa.
Chester aliifuta miwani yake kwa hasira. "Ugonjwa wa Alvin kwa kweli ulidhoofika sana wakati wa kukupa talaka."
"Lakini kwanini ninahisi kwamba afya yake ilianza kuzorota baada ya Maurine Langa kutokea?" Lisa alisema kwa unyonge.
Chester alikunja uso. "Sio lazima umtupie hili Maurine kwa wakati huu."
“Kwa kweli sielewi kwanini nyie wote mnamtetea. Ni kwa sababu tu yeye ni binamu ya Sarah Langa? Uliweza hata kuachana na Charity Njau kwa sababu ya Sarah?”
Uso mpole wa Chester ulipoa ghafla. “Charity alikuambia nini? Kuachana naye hakuhusiani na mtu yeyote. Nilimchukia tu…”
Lisa alitazama mlango nyuma yake na kujisikia vibaya. “Charity…”
Chester aligeuka na kumuona Charity akiwa amevalia suti nyeusi ya kikazi. Suti iliukumbatia vyema mwili wake na kukifafanua kiuno chake chembamba. Alikuwa amebeba matunda na juisi mikononi mwake. Nywele zake nyeusi zilikuwa zimefungwa, na uso wake ulikuwa umepoa.
Macho yao yalipogongana, Charity akadhihaki. "Ni bahati mbaya. Mimi pia nilichukizwa na wewe. Kwa bahati nzuri, tuliachana mapema. Vinginevyo, ningekuwa na wasiwasi kuhusu kupata STD.”
Uso wa Chester ukafifia ghafla, akageuka nyuma na kumuonya Lisa, “Kumbuka nilichokuambia. Usimchokoze Alvin. Vinginevyo, ninaweza kumfanya Daktari Angelo amwache baba yako.”
Macho ya Lisa yalimtoka, akainamisha kichwa chini huku akikunja blanketi kwa nguvu. Chester akageuka na kuelekea mlangoni, akampiga kwa nguvu Charity begani.
Charity alijikwaa na kumlaani, "Chester Choka, huna aibu kiasi gani kumtishia mwanamke?!"
"Fuatilia mambo yako mwenyewe, au usinilaumu kwa kukutupa tena kwenye maji." Chester aliondoka na uso ulionyooka.
Charity akauma meno na kusema. "Achana nao. Ni kundi la wahuni wasio na akili!"
Lisa alikuwa tayari amekasirika na ghafla alicheka aliposikia laana ya Charity. "Hawana akili. Wanacheza tu kwenye kiganja cha Maurine Langa.”

Sura ya: 261

Lisa alikaa hospitalini kwa siku sita. Siku moja kabla ya kuwa tayari kuruhusiwa, Bibi Kimaro alimpigia simu Alvin.
“Utakuwepo nyumbani kwako leo? Zabibu zimeiva, kwa hivyo nitakuletea na kuja kukusalimia pia. Hutaki hata kuja kumuona bibi mzee kama mimi mpaka nianze kuja kwako kwanza?”
“Zabibu ni nzuri. Ikiwa mwanamke mjamzito atakula zabibu nyingi zaidi, labda watoto watazaliwa na macho yenye nguvu zaidi,” Alvin alisema baada ya kufikiria.
“Nini… ulisema nini?” Bibi Kimaro alishikwa na kigugumizi.
'Ni nini hasa ambacho hujaelewa? Nitakuwa baba.” Alvin alitabasamu. Sauti yake ilifurahisha alipotamka kwa mbwembwe, "Baba wa mapacha."
"Alvin, kwanini hukutuambia habari muhimu kama hii?" Sauti ya Bibi Kimaro ilikaribia kumtia uziwi. “Mapacha! Mungu wangu! Familia ya Kimaro haijawahi kupata mapacha.”
Mzee Kimaro, ambaye alikuwa akisoma gazeti na miwani yake ya macho, pia aliketi na kutega masikio yake.
“Kwanini nikuambie? Najua humpendi Lisa.” Alvin akasimama kwa mbwembwe. “Ningekuambia huenda ungemtesa tena.”
Bibi kizee yule alihisi moyo ukimuuma kwa kuambiwa vile. “Mimi… Hiyo ilikuwa zamani. Ikiwa ana mimba ya mapacha, bila shaka, nitamhudumia ipasavyo. Mko nyumbani sasa, sivyo? Nitakuja mara moja…”
“Hayupo.” Alvin alishtuka ghafla. “Yupo hospitalini. Alianguka na karibu vitoto vitoke."
"Nini? Hiyo ilitokeaje? Wajukuu zangu wa thamani wako sawa? Angewezaje kuwa mzembe hivi wakati tayari ni mama…”
“Hapana, si kosa lake. Ilisababishwa na uzembe wangu,” Alvin alijibu bila kufafanua.
“Usie na maana wewe… Huna hata haya.” Bibi Kimaro akakata simu. Chini ya dakika 40 baadaye, yeye na Mzee Kimaro walionekana hospitalini kwa wakati mmoja.
Kuonekana kwa wazee hao wawili kulimtia hofu Lisa. Baada ya yote, alikutana na Bibi Kimaro mara tatu tu na Mzee Kimaro mara mbili. Kila wakati, hawakuwa wameonekana kuwa na furaha kumuona. Sasa, mara tu walipoingia ndani, nyuso zao zilijaa tabasamu za kupendeza. Ilimfanya ajisikie wa ajabu sana.
“Babu, Bibi…” Lisa alinyanyuka, lakini Mzee Kimaro mara moja akasema kwa sauti ya kusikitisha, “Usinyanyuke. Watoto walio tumboni mwako ni muhimu zaidi.” Lisa alishangaa. Kweli, tayari alikuwa ametarajia hii.
"Babu, Lisa ni muhimu vile vile," Alvin alimkatiza, akiwa na kinyongo.
Bibi Kimaro mara moja alimkazia macho. "Ikiwa unajua yeye ni muhimu, kwanini ulisababisha vitoto vyake vikajeruhiwa?"
Alvin alikunja uso lakini alikuwa mtiifu na hakukanusha. Wazee wale wawili walipoona hivyo, Mzee Kimaro aligonga miwani yake na kusema. “Mjinga sana wewe. Kwanini huna akili ya kujizuia. Unawezaje kuwa na tamaa wakati mkeo tayari ni mjamzito?"
Alvin na Lisa waliganda kwa wakati mmoja. Sentensi hiyo iliwatia aibu kwa kiasi fulani. Kisha, Bibi Kimaro alisema kwa dhati, “Ninaelewa kwamba nyinyi ni wachumba wapya na hamwezi kujizuia, lakini bado mnapaswa kuzingatia watoto walio tumboni. Hamuwezi kulala pamoja kwa muda huu, au mwishowe mtawadhuru watoto.”
Uso wa Lisa uliganda na kusinyaa kwa aibu. Je, walifikiri kwamba vitoto vyake viliathirika kwa sababu alikuwa amelala na Alvin? Mungu wangu!
Uso wa Alvin nao ukawa mtupu. Hakuweza kuelewa jinsi gani wazee hao wawili walifikia hitimisho hilo hata kidogo.
“Hapana, Bibi. Sisi—”
“Inatosha, msitake kusema zaidi.” Bibi Kimaro aliwakatisha, “Ukiruhusiwa kesho, uje nyumbani uishi kwenye makazi ya familia ya Kimaro. Nitaajiri mpishi bora wa kuhudumia lishe yako urudi kwenye afya. Pia, hali ya hewa kwenye makazi yetu ni nzuri na inafaa kwa wewe kulea watoto wako. Nitabaki na uhakika ikiwa nitawaona mkilala katika vyumba tofauti."
“Siendi.” Alvin alikataa kabisa. Alikataa kulala katika vyumba tofauti. Hakuweza kuvumilia hata ikiwa ni kwa siku moja tu.
Hapo awali Lisa alitaka kupinga, lakini moyo wake uliguswa kidogo na maneno ya Bibi Kimaro. Alikubali kwa kichwa. "Niko tayari kuhamia katika nyumba yako. Bibi, wewe ni mtu mwenye uzoefu na umezaa watoto kadhaa, kwa hiyo nadhani uko sahihi.”
"Hiyo ni sawa." Bibi Kimaro alimpa sura ya kuidhinisha. Kwa mara ya kwanza, aliridhika kidogo na Lisa.

Macho mazito ya Alvin yakatua kwenye uso wake mdogo. Alijua anachofikiria. Alitaka kumkwepa na hakutaka kulala naye. “Sikubaliani."
“Ni bure kwako kukataa,” Mzee Kimaro aliamuru, "Kwa vyovyote vile, mapacha wa kwanza wa familia ya Kimaro lazima wazaliwe wakiwa na afya njema."
Alvin akajilaumu mwenyewe. Hakupaswa kuwaambia wawili hao kuhusu ujauzito. Kiherehere chake kilimponza.
Wazee hao wawili walipoondoka, alimwangalia Lisa bila furaha. "Ulifanya hivyo kwa makusudi."
“Ndiyo.” Lisa alitazama juu na kusema, "Alvin Kimaro, kumbukumbu yako sio nzuri, lakini sitasahau jinsi mimba yangu ilivyotaka kutoka. Labda ni salama zaidi kwangu kuishi na hawa wazee kwa sasa. Angalau sitalazimika kuvumilia vitisho vya rafiki zako, ugonjwa wako usije ukadhoofika na kuwa kosa langu.”
Mwale wa mwanga baridi uliangaza machoni mwa Alvin. Mara moja alielewa kwamba lazima Chester na Rodney walimwambia kitu. Alvin alikuwa amezungumza nao hapo awali, lakini walikuwa marafiki kwa zaidi ya muongo mmoja, wasingeweza kugombana kirahisi.
“Samahani…”
“Hakuna haja ya samahani. Sidhani tu kwamba nina thamani kuzidi Sarah. Ikiwa moyo wako ungejazwa na mimi, ningebeba jukumu lote.Lakini unanificha mambo yako mengi, na uhusiano wako na Maurine Langa haueleweki. Kwanini niwajibike kwa hali ya ugonjwa wako? Nalazimika kuvumilia hata kama sina furaha.”
Lisa alijiachia na kujilaza kitandani, hakutaka tena kumtilia maanani. Alikuwa amekasirika sana Chester alipomtumia Joel kumtishia.
Asubuhi iliyofuata. Bibi Kimaro alimtuma dereva kwenda kumchukua Lisa. Mlinzi wa nyumba alimpangia kukaa kwenye chumba cha zamani cha Alvin.
Alikuwa ameingia kwenye chumba hiki hapo awali, lakini kilikuwa kimeachwa wakati huo. Hata hivyo, sakafu ilikuwa imefunikwa na kapeti ya manyoya kwa muda huo, na pia kulikuwa na TV na viti viwili vya mapumziko. Chumba hicho pia kilipambwa kwa maua yenye harufu nzuri.
"Kwanini hii inaonekana tofauti na nilipokuwa nalala mimi?" Alvin alionyesha mashaka yake.
"Bibi Kimaro alisema kuwa chumba cha hapo awali kilikuwa baridi sana na hakifai kwa wanawake wajawazito, kwa hivyo mbunifu aliongeza vitu vichache mara moja." Mlinzi wa nyumba alisema, "Bwana Kimaro, chumba chako kiko kwenye jengo linalofuata."
Alvin aliuma meno na kusema. “Kwanini mniweke kwenye nyumba tofauti? Nataka chumba cha jirani.”
"Hapana, Bibi Kimaro alisema kwamba anaogopa utaingia katikati ya usiku."
Alvin alikasirika kiasi cha kutaka kutapika damu. “Inatosha. Nitalala chumba cha jirani. Huo ndio uamuzi wangu wa mwisho. Vinginevyo, nitaondoka naye moja kwa moja.”
"Sawa Bwana Mkubwa." Mhudumu wa nyumba alinyamaza kwa muda kabla ya kukubaliana kinyonge.
Mchana, Lisa alilala hadi saa kumi jioni Aunty Yasmine akampelekea glasi ya mtindi. Baada ya kumaliza kunywa, alienda kwenye matembezi uani.
Ilibidi akubali kwamba makazi ya familia ya Kimaro yalikuwa yakifahari sana. Yalichukua eneo kubwa, na hewa ya pale ilikuwa safi sana. Hakuwa ametembea kwa muda mrefu alipowaona Valerie na Queenie wakiingia kwenye makazi yale ya kifahari.
"Lisa Jones, unawezaje kuthubutu kuonyesha uso wako hapa?" Valerie alilipuka ghafla baada ya kumuona......ITAENDELEA....

Unafikiri nini kitafuata hapo, maana simulizi inazidi kuwa tamu kila siku lakini sina budi kuhitimisha kipande hiki ila niwasihi tukutane katika episode zijazo ili kujua nini kitafuata kwenye mkasa huu wa kusisimua na kuelimisha unaokwenda kwa jina la LISA.