JINA LA SIMULIZI............................LISA
AUTHOR...........................JOMBA WAJO
SPONSORED BY......SIMULIZI ZA DULLY
WHATSAPP..........................0628924768
SEHEMU YA................................250-251
Sura ya: 250
Lisa aliposhuka chini ili kuchota maji, ghafla alikumbuka tukio la yaya wa Alvin kumfungia chumbani alipokuwa mdogo…
Glasi mkononi mwake ilidondoka chini na kuvunjika sakafu. Alikimbia ghorofani na kufungua chumba alichoingia Alvin.
Mwili wa Alvin ulikuwa umejikunja ndani ya kabati na kuwa kama mpira, na kichwa chake kilizikwa kwenye magoti yake. Alikuwa akitetemeka kama mbwa aliyenyeshewa mvua.
"Alvin, toka nje." Lisa alijaribu kumtoa lakini akashindwa.
“Nasikia baridi sana… Usinipige…” Alvin alikuwa akiziba masikio yake kwa nguvu zake zote.
Lisa hakutaka kumuonea huruma, lakini moyo wake ulimshinda na kujikunja kwa maumivu wakati huo.“Sitakupiga. Usilale humu twende kitandani. Kila kitu kitakuwa sawa.” Lisa alimkumbatia na kumpigapiga mara kwa mara.
Mwili wake ulipoacha kutetemeka, alimsaidia kumkokota hadi kitandani, akamlaza na kumfunika blanketi. Hata hivyo, Alvin alimshika mkono kwa nguvu. Hakuweza kumwacha aondoke hata kidogo.
Lisa alijaribu kuutoa mkono wake mara kadhaa lakini akashindwa. Hatimaye, hakuwa na chaguo ila kulala upande mwingine. Awali alipanga kwenda kulala chumba cha wageni baada ya yeye kulala, lakini yeye mwenyewe alipitiwa na usingizi kwa sababu alikuwa amechoka sana.
Hakujua alikuwa amelala kwa muda gani. Katika hali ya ukungu, alihisi mtu akibusu midomo yake kwa hamu. Wimbi la msisimko lilitanda kwenye ngozi yake.
Alifumbua macho yake ghafla. Alipomuona Alvin akiwa juu yake, alimsukuma kwa hasira. “Nani amekuruhusu kunibusu?”
“Lisa, hakika una wasiwasi na mimi. Ulilala kando yangu jana usiku. Unanijali.” Alvin alitabasamu na kumtazama kwa furaha. "Hebu tufanye kidogo."
"Si Maurine alikukataza mpaka umalize dozi?" Lisa akakumbuka tukio la Maurine akiwa ameketi juu yake chumbani. Alihisi kichefuchefu na kukimbilia chooni kutapika.
Alvin alimfuata chooni akiwa na wasiwasi. Lisa alimtazama baada ya kutapika na kutaka kuendelea kumbusu. “Usinibusu, nahisi kichefuchefu sana nikiguswa tu na wewe.”
Macho ya Alvin yaligeuka kuwa mabaya mara moja. Kwanini alimchukia kiasi hicho? Ndiyo, alikuwa na nafasi kwa Sarah moyoni mwake, lakini hakuwahi kufanya jambo lolote lililomsaliti Lisa. Akakunja uso kisha akageuka kuelekea chini.
Lisa alishuka baada ya kufanya usafi. Harufu ya mayai ya kukaanga ilikuwa ikitoka jikoni.
“Sandwichi, maziwa, na mayai ya kukaanga. Karibu tule.” Alvin alikuwa amevaa aproni na kwa kushangaza alitengeneza seti mbili za kifungua kinywa. Kutokana na mwonekano wake, alikuwa akijaribu kumfurahisha Lisa.
Lisa karibu alitaka kufungua madirisha na kuchungulia nje ili kuona kama jua lilikuwa limechomoza kutoka magharibi badala ya mashariki siku hiyo. Walikuwa pamoja kwa muda mrefu sana, lakini aliwahi kumtengenezea chakula mara moja tu—na kilikuwa na ladha mbaya sana.
Ingawa kifungua kinywa hakikuonekana kutosha kumvutia kula, alikuwa na njaa kwani alikuwa ametoka kutapika. Hata hivyo, hakutaka kula.
"Samahani, lakini mimi siwezi kula aina hii ya kifungua kinywa." Alikataa kwa kiburi na kuelekea mlangoni.
Alvin alijisikia kama sehemu ya moyo wake imeondolewa kwa kuambiwa jibu kama hilo. Lakini akakumbuka hakuwa na haki ya kukasirika kwani alikuwa amemwambia hivyhivyo wakati alipomwandalia kifungua kinywa kwa mara ya kwanza huko nyuma. Mwanamke huyo alijua jinsi ya kuweka kinyongo.
Kuona kiamsha kinywa ambacho Alvin alimtayarishia hapo awali kulimfanya awe na njaa. Aliendesha gari hadi kwenye mgahawa wa kifungua kinywa. Alisikia kutoka kwa Pamela kwamba chakula kwenye mgahawa huo hakikuwa kibaya. Alvin alimpigia simu Hans na kumwambia amfuatilie Lisa kimyakimya, na endapo ataona amekutana na Charity ampigie simu.
Lisa alipoanza tu kula baada ya kuagiza kifungua kinywa chake, Melanie na Jerome waliingia kwenye mgahawa huo wakiwa wameshikana mikono.
Meneja wa mgahawa aliwafuata wote wawili kwa makini. “Bwana Campos, Bi Ngosha, mngependa kuketi wapi?”
Melanie alitazama huku na kule na kugonganisha macho na Lisa. Macho yake yakaangaza. Alimvuta Jerome na kwenda mara moja kuelekea kwa Lisa.
“Oh, huyu si mke wa Bwana Kimaro? Kwanini unakula kifungua kinywa hapa peke yako? Yuko wapi Bwana Mkubwa Kimaro ambaye anakupenda sana?" Melanie alitazama pande zote kuangaza.
Lisa alikunja uso. Alikuwa na kifungua kinywa kizuri, lakini walipotokea tu hao watu alihisi kama inzi wameingia kwenye bakuli la supu yake ya mbuzi.
Msimamizi wa cafe aliogopa. "Bi Kimaro, samahani…"
“Huna haja ya kumwomba msamaha Bw. Cameron.” Jerome alitoa tabasamu zito. "Nadhani hatakuwa Bi Kimaro tena hivi karibuni. Nijuavyo, Bi. Jones amefukuzwa nyumbani kwa Bwana Kimaro. Nilisikia kwamba hata alitafuta nyumba ya kununua na kuhamia kwa haraka siku chache zilizopita.”
Bwana Cameron alielewa maneno yake na hapohapo heshima aliyokuwa nayo hapo awali kwa Lisa ikatoweka. Mtazamo alioutoa kwa Lisa haukuwa wa heshima tena, hata ulijawa na dharau.
"Bwana Campos, una taarifa sahihi kabisa." Lisa alijifuta mdomo na kumtupia macho makali Jerome. "Unajua zaidi kuliko vyombo vya habari. Inawezekana kwamba ulikuwa na jasusi uliyemwajiri ili kunipeleleza?"
Jerome alifoka. “Nani asiyejua kuwa Alvin alileta binamu wa mpenzi wake wa zamani nyumbani siku chache zilizopita ili amtunze? Ni kwa sababu ameona wewe hufai na unazidi kumpandisha wazimu wake.”
“Umekuwa mjinga sana.” Sauti ya Melanie ilijaa kejeli. “Alvinarah, Alvinarah, haimaanishi Alvin na Sarah? Angalia uso wako wa kutisha. Ulijidanganya kwamba unaweza kukalia nafasi ya Sarah kwa Alvin Kimaro. Lakini sina budi kukushukuru pia. Kama usingempokonya Alvin, nisingeweza kukutana na Jerome wangu ambaye ananithamini sana.”
Jerome alizipapasa nywele za Melanie. Ingawa hakuwa amempenda Melanie hapo awali, alijifanya kumpenda sana kwa sababu fulani. Joel asingekuwepo tena, kwa hivyo Melanie alikuwa mrithi wa Ngosha Corporation. Hakutaka kupiga teke kapu la bahati iliyokuwa ikimdondokea mapajani mwake. Familia ya Ngosha na familia ya Campos zingeungana. Alvin angekuwa si kitu kwa wakati huo.
"Bwana. Cameron, nadhani meza yake karibu na dirisha si kibaya,” Melanie alisema huku akinyoosha kidole kwenye meza ya Lisa. “Tutakaa hapa.”
"Basi mtoe haraka na umpeleke kwenye meza nyingine," Jerome aliamuru kwa kiburi.
Bila kukawia zaidi, Bwana Cameron alimmwambia mhudumu kusogeza vitu vya Lisa kwenye meza iliyokuwa karibu na ukuta kwenye kona ya mgahawa huo. “Bi. Jones, tafadhali kula kifungua chako huko.”
“Nyie ni…” Lisa akatikisa kichwa na kusimama.
Melanie alitabasamu. "Lisa Jones, unaona hii? Hutanishinda kamwe. Mimi ni makamu wa mwenyekiti wa Ngosha Corporation sasa. Wiki ijayo, nitaolewa na Jerome. Kufikia wakati huo, familia za Campos na Ngosha zitakuwa timu yenye nguvu. Hakuna mtu nchini Kenya atakayethubutu kusema chochote hata nifanye nini.”
“Oh, hongera basi.” Lisa akasimama taratibu. "Baba bado amelazwa kwenye kitanda cha hospitali na haijulikani ikiwa ataishi au atakufa, lakini wewe? Unapata wapi hata hiyo hamu ya kuolewa?”
"Melanie anamjali sasa baba yake, anataka amletee zawadi ya wajukuu wenye akili." Jerome alijibu mbele ya Melanie.
“Eti anamjali sana Baba! Mbona sijawahi kuwaona mkimtembelea hata mara moja baada ya kuzimia?” Lisa alitoa tabasamu la uwongo.
"Niende au nisiende sio kazi yako." Melanie alidhihaki, “Vipi kuhusu wewe? Ulipata haki za kumtunza Baba, lakini kwa faida ipi? Ngosha Corporation ni yangu, na kila kitu ambacho Baba anamiliki ni mali yangu. Huna chochote cha kurithi. Nilisikia kwamba Daktari Angelo amekufa. Hakuna mtu anayeweza kumwokoa Baba sasa. Unaweza kuukumbatia mwili wake maisha yako yote, ndicho kilichobakia.”
"Angalia sauti yako. Inaonekana huna huzuni hata kidogo kwamba Daktari Angelo amekufa na Baba hawezi kuamka.” Lisa alishtuka na kuinua kichwa chake.
Koo la Melanie lilikwama kwa muda. Alisema kwa hasira, “Je, unaweza kupotea haraka? Usitusumbue tukiwa tunapata kifungua kinywa chetu.”
"Endelea kuwa jeuri kwa sasa, lakini siku zako zinahesabika." Lisa akatoa noti kadhaa na kuzitupa mezani. “Nitawaachia meza, lakini siku nyingine… msitarajie kama itatokea tena.” Alichukua mkoba wake na kuondoka baada ya kumaliza kuzungumza.
Hans, aliyekuwa amejificha kwenye kona moja, aliripoti kwa Alvin kila kitu alichokiona akifanyiwa Lisa
Sura ya: 251
Baada ya Lisa kuondoka, Melanie alinyamaza kwa muda na kugeuka kumwangalia Jerome. “Ulisema Alvin kamleta binamu wa Sarah ili kumuuguza. Ni kweli?
“Una wasiwasi kuhusu Alvin?” Jerome alimshika mkono na kuuchezea. "Bado huwezi kumsahau tu, huh?"
"Hapana. Ni wewe tu moyoni mwangu sasa." Melanie alishusha macho na kutabasamu. “Nina hamu tu ya kutaka kujua.”
Jerome alijibu kwa kujiamini. “Si hivyo tu, ugonjwa wa Alvin umezidi kuongezeka. Hata alizimia siku chache zilizopita na kupelekwa hospitali kwa dharura.”
Hans aliyekuwa kajificha kwenye kona fulani, alishuhudia kila kitu kilichotokea. Papo hapo alichukua simu kisha akampigia Alvin na kumpa ubuyu wote.
“Bwana Mkubwa, Bibi mdogo alikutana na Jerome Campos na Melanie Ngosha. Wawili hao walishirikiana pamoja na meneja Cameron kumfedhehesha Lisa hata kumfukuza kwenye meza aliyokuwa amekaa."
Mbele ya kibaraza akiwa anaota jua la asubuhi, Alvin alisikiliza simu hiyo na kupandwa na ghadhabu. “Ni wakati wa kuwaadhibu watu hao wawili. Wape zawadi kubwa. Kuhusu mgahawa huo, hakuna sababu ya kuendelea kufanya kazi tena.”
Katika mgahawa, Jerome na Melanie walikuwa ndo kwanza wameanza tu kula kifungua kinywa chao wakati kundi la maafisa wa Afya kutoka jiji walipovamia mgahawa huo na kumkamata meneja wa mgahawa huo. "Kuna mtu aliripoti kwamba aliumwa na tumbo baada ya kula kifungua kinywa hapa. Kwa hiyo, mgahawa huu lazima ufungwe kwa uchunguzi. Watu wote wasio watumishi wanapaswa kuondoka."
Maafisa waliwafukuza watu wote nje ya mgahawa huo. “Ondoka haraka.”
Melanie alikasirika. “Bado sijamaliza kula kifungua kinywa changu. Unajua mimi ni nani?"
"Sina haja ya kujua wewe ni nani, lakini najua unatuzuia kufanya kazi yetu." Maafisa waliwafukuza na hata kutupa vitu vyao nje.
Melanie aliendelea kusema kwa hasira, “Nitawaripoti!”
Jerome pia hakuwa katika hali nzuri. “Usijali mpenzi, najuana na watu wa juu zaidi. Ninaweza kuwafanya watu hao wapoteze kazi kwa simu moja tu.”
"Jerome, kweli? Wewe ni ‘so amazing!’ Wafunze adabu mbwa hawa!" Uso wa Melanie ulijaa jeuri.
Jerome alitabasamu na kutoa simu yake. Alikuwa karibu kupiga simu sehemu wakati alipoona simu ya sekretari wake ikiingia ghafla. “Bwana Campos, tuko taabani. Idara ya sheria ya KIM International ilimtuma mwanasheria wao. Walisema katika kipindi cha miaka 20 familia ya Campos imevuna faida ya bilioni 80 kutoka KIM International isivyo halali, wakati familia za Campos na Kimaro zikishirikiana katika miradi ya pamoja. Wametuma notisi kutaka warudishiwe fedha zao.”
"Nini?" Uso wa Jerome ulibadilika ghafla. “Alvin ana wazimu?”
“Wameleta nyaraka zote. Kila kitu kiimewekwa wazi." Katibu akatabasamu kwa uchungu.
"Damn!" Jerome alikasirika. Hatimaye alielewa, kuanzia tukio la Lisa hadi tatizo la akaunti za kampuni, hayakuwa ni bahati mbaya tu. Lazima kulikuwa na mkono wa Alvin. Huyu Alvin alikuwa anakaribia kuwa kichaa, na kichaa chake sasa kilimgeukia yeye. Kwa bahati mbaya, yote yalikuwa kweli.
Miaka hiyo yote Lea alipokuwa akiongoza kampuni ya KIM, alikuwa ameisaidia sana familia ya Campos. Hata alishirikiana na familia ya Campos kwenye miradi mingi ya pamoja. Kwa kawaida, KIM International haikushiriki katika miradi hiyo, hivyo kimsingi walifumba macho na kuwaachia familia ya Campos kupitia kampuni yao ya Campos Ltd. kupata faida. Ni siku chache zilizopita ndipo walipokaza sera zao baada ya Alvin kushika nafasi ya uongozi.
Sio kwamba familia ya Campos haikuwa na bilioni 80, lakini, kutoa kiasi kikubwa cha pesa kama hicho kwa ghafla kungeathiri mradi mkubwa ambao familia ya Campos ilikuwa karibu kuanza. Mradi huo ungeweza kubadilisha mustakabali wa familia ya Campos. Kwa hiyo, wasingeweza kutoa pesa hizo.
•••
Lisa alifika kwenye ofisi za kampuni yake asubuhi na mapema. Meneja Mkuu alipokuja kuchukua saini yake, alisema kwa wasiwasi, “Nimesikia kwamba… umetengana na Bw. Kimaro na unajitayarisha… kwa talaka?”
Kalamu iliyokuwa ikisaini karatasi ilisimama. Lisa aliinua kichwa chake kwa utulivu. “Inazungumzwa hivyo nje?”
"Ndio, kampuni zingine ambazo zilikuwa na makubaliano ya mdomo na sisi hapo awali zilighairi ushirikiano wao tena na sisi. Hawapokei hata simu za kampuni yetu sasa hivi.” Meneja alieleza kwa wasiwasi.
"Usijali. Kipaumbele chetu kwa sasa ni kuzingatia tu kuendeleza ujenzi wa jengo letu la ofisi kwenye uwanja wetu mpya.” Lisa hakuwa na wasiwasi hata kidogo. "Pia, uwaonye wafanyakazi kufuatilia mambo yasiyowahusu. Ni vyema kila mtu azingatie tu kufanya kazi zake kwa bidii.”
“Sawa.” Meneja Mkuu aliinamisha kichwa kwa simanzi baada ya kutoka ofisini. Alidhani nafasi ya Mawenzi Investments ingepanda kwa kasi baada ya kuungwa mkono na Alvin Kimaro.
Hali katika kampuni ilikuwa tulivu asubuhi nzima. Ilipofika karibu saa sita mchana, Alvin aliingia ghafla kwenye lango la ofisini za Mawenzi. Wafanyakazi kwenye ofisi ya mapokezi walihisi kutetemeka kwa kila hatua ambayo Alvin alikuwa akipiga kuwasogelea.
Kama kawaida, minong’ono ya mishangao ikasikika miongoni mwa wafanyakazi hao;
“Ni Alvin Kimaro…”
“Ooh! Jmani huyu kaka ni mzuri! Nilikuwa sijawahi kumuona kwa karibu hivi. Kwa kweli ni mzuri, bosi atakuwa anafaidi sana....”
“Thubutu! Nasikia ndoa yao ina migogoro kama nini, hivi tunavyoongea wanataka kuachana…”
“Mbona sasa yuko hapa? Au ndo atakuwa kamletea talaka bosi wetu?
“Oh Mungu wangu, hapana.”
“Bwana Kimaro, karibu…” Mhudumu wa mapokezi wa kike alimpokea kwa tahadhari. “Tukusaidie nini?”
“Huoni hii?” Alitikisa kontena la chakula alilokuwa amebeba. “Nimekuja hapa kumletea chakula mke wangu.”
Mhudumu yule aliingiwa na hofu. Si alisikia walipeana talaka? Kwanini Bwana Kimaro alimpelekea chakula yeye binafsi basi?
"Yuko wapi?" Alvin aliinua macho yake na kupepesa.
Yule mhudumu wa mapokezi alikaribia kupofushwa kwa hofu ya kumkaribia tu Alvin, na alikuwa kwenye hatihati ya kuzimia. "Saa hii ... ameenda kwenye mgahawa kula."
Alvin alielekea kwenye mgahawa bila wasiwasi. Hii ilikuwa mara yake ya pili kutembelea ofisi za Mawenzi. Aliiona sura ya Lisa kwenye mgahawa haraka sana. Alikuwa anavutia macho kweli. Alivaa suti ya rangi ya khaki siku hiyo, na nywele zake ndefu zilikusanyika upande mmoja. Kutokana na mwonekano wake wa kipekee, alikuwa anaonekana kama ametoka ulimwengu mwingine kabisa.
Watendaji wachache wa kampuni walikusanyika karibu naye. Hakujua wanazungumza nini, lakini hali ilikuwa wazi walikuwa na mazungumzo ya kupendeza. Alvin akakunjua uso wake kwa tabasamu. Alitembea kwa hatua ndefu kuwasogelea.
Lisa alikuwa akijadiliana na watendaji hao kuhusu maendeleo ya ujenzi wa ofisi za kampuni ya Mawenzi kwenye uwanja wake aliopewa na Joel. Kisha, alihisi mazingira yakitulia ghafla na kila mtu alikuwa akitazama nyuma yake.
Wanawake walikuwa hoi huku wanaume wakiwa na sura za woga na zenye heshima. Lisa aligeuka kuangalia kulikoni, na ghafla macho yake yakakutana na uso mzuri wa Alvin. Mapigo ya moyo wake yalianza kwenda kasi.
"Babe, nimekuandalia chakula cha mchana." Sauti ya Alvin ilikuwa ya upole, tamu na ya kuvutia utadhani asali ilikuwa ikichuruzika kutoka kwenye maneno yake.
Lisa alikunja uso. Alikuwa karibu kusema kitu wakati Meneja Mkuu alisimama mara moja na kusema. "Katika hali hiyo, Mwenyekiti Jones, unapaswa haraka kwenda ofisini na kula chakula chako na Bwana Kimaro."
Meneja wa Idara ya Masoko alitabasamu kutoka sikio hadi sikio. "Bwana Kimaro, una mapenzi mazito sana kwa mkeo."
Meneja wa Idara ya Mahusiano ya Umma ambaye alikuwa ni mdada, alisema, “Wanaume wazuri kama Bwana Kimaro wanakaribia kutoweka duniani. Mume wangu hajawahi kuniandalia chakula maishani mwangu.”
Mambo yalitiwa chumvi zaidi wakati msimamizi wa mgahawa alipoishiwa nguvu na kusema, “Chakula katika mgahawa wetu hakika hakiwezi kuwa kitamu kama kile ambacho Bwana Kimaro amekuandalia. Bi. Jones, hupaswi kuruhusu juhudi zake zipotee.”
Hao walikuwa wafanyakazi wake au wa Alvin? Lisa alikosa jibu.
"Twende," Alvin alizungusha mkono kiunoni mwake na kumnong'oneza sikioni, "Hutaweza kugombana nami ambapo kila mtu anatutazama, sivyo?"
Lisa alikosa la kusema. Hakuwa na budi ila kuelekea naye ofisini kwake....ITAENDELEA.......
Unafikiri nini kitafuata hapo, maana simulizi inazidi kuwa tamu kila siku lakini sina budi kuhitimisha kipande hiki ila niwasihi tukutane katika episode zijazo ili kujua nini kitafuata kwenye mkasa huu wa kusisimua na kuelimisha unaokwenda kwa jina la LISA.
