JINA LA SIMULIZI............................LISA
AUTHOR...........................JOMBA WAJO
SPONSORED BY......SIMULIZI ZA DULLY
WHATSAPP..........................0628924768
SEHEMU YA................................242-243

Sura ya: 242

Lisa alimtazama Kelvin kwa butwaa. Sarah Wonderland Park? Bila shaka, alikuwa amesikia kuhusu bustani hiyo kubwa zaidi ya burudani ya Nairobi ambayo ilitoa burudani zenye kusisimua zaidi kutoka duniani kote. Moja ya jumba hilo liligharimu dola milioni 30 kulijenga. Hata hivyo, hakujua kuwa ni Alvin ndiye aliyemjengea mpenzi wake wa zamani uwanja huo wa burudani.

Kelvin aliongea kwa sura ya huzuni. "Na kumkumbuka, jina la Alvinarah ni mchezo wa maneno wa majina yao. Lisa, watu wengi mtandaoni wanakuonea wivu, lakini unajua kuna watu wengi katika jamii ya matajiri ambao wanakudhihaki?”

"Basi, inatosha!" Lisa alitikisa kichwa, akikataa kusikia zaidi.

"Kuna jambo moja zaidi ambalo hujui." Kelvin ghafla, akamshika mkono. “Unajua kwanini Zigi Kabwe alitaka kukuua?”

Midomo ya Lisa ilitetemeka. Hakumruhusu kukwepa swali hilo. "Familia ya Zigi ilikasirika kwa sababu Alvin alimwakilisha Thomas Njau kwa kesi ya ubakaji. Alifanya hivyo kwa sababu tu mwanamume huyo ni kaka wa Sara. Hakujali chochote kwamba Thomas Njau ni mtu mbaya ambaye alikuwa amefanya mambo mengi haramu maishani, alichojali ni kumsaidia tu kaka wa mpenzi wake. Alisaliti kanuni za kazi yake mwenyewe kwa sababu ya Sarah!”

Lisa aliduwaa na kukaa kimya. Hata kama alikuwa ameshaujua ukweli huo, kusikia hivyo kutoka kwenye kinywa cha mtu mwingine kuliufanya moyo wake udunde haraka sana kiasi kwamba alihisi kukosa hewa.

Hapo awali, alidhani Alvin alimtetea Thomas Njau kwa sababu ya pesa.
Kisha, alipojua kwamba alikuwa mtu tajiri zaidi nchini, alifikiri kwamba alikuwa amefanya hivyo kwa sababu ya kiburi cha uwezo wake na utukufu wa kuwa juu. Kumbe, ilikuwa tu kwa sababu ya mpenzi wake wa zamani.
Sara alikuwa muhimu kiasi gani kwake, kweli?

Kelvin alisema kwa sauti ya huzuni, “Ulikuwa karibu kufa wakati huo. Kwanini mimi na wewe tuingie matatizoni kwa sababu ya matendo mabaya aliyoyafanya Alvin kwa ajili ya mpenzi wake wa zamani?”

"Kelvi, nimesema inatosha!" Lisa alitamani kulia. Alihisi kwamba angepoteza akili ikiwa angeendelea kusikiliza zaidi.

“Lisa, nakuambia haya tu kwa matumaini kwamba utabaki kuwa na akili timamu. Usiache kila kitu kwa ajili yake, ikiwa ni pamoja na moyo wako. Hana afya, na hawezi kujitolea kwako isipokuwa wewe tu ndiye mtu unayempenda. Lakini nakuapia, hutaweza kuchukua nafasi ya mtu aliyekufa."

“Nitaweza. Asante.” Lisa alisema kwa hasira kabla ya kuutoa mkono wa Kelvin uliokuwa umemshika. "Nataka nibaki peke yangu kwa muda."

“Hakika…” Kelvin aliweka nywele za Lisa nyuma ya sikio lake.

Hatimaye, Lisa alipotoka kwenye mgahawa huo wa Stears alionekana kukata tamaa. Mapenzi machoni pake yalibadilishwa mara moja na dhamira hatari.
•••
Wakati huo huo, huko Mombasa katika jumba la Alvin la ufukweni mwa bahari, Alvin alipokea picha kadhaa kutoka kwa paparazi aliyemfahamu vyema.

Kulikuwa na picha chache za Lisa na Kelvin wakila aiskrimu pamoja kwenye mgahawa wa Stears, pamoja na ile aliyomshika mkono. Ingawa ilichukuliwa kutoka upande, mapenzi machoni pa mwanaume huyo na sura yake ya huzuni ilijidhihirisha wazi kwenye picha. Ni mkutano mzuri ulioje wa wapenzi wa zamani.

Hasira ambayo alikuwa ameivumilia hapo awali hatimaye ililipuka kama volkano. Alvin aliinuka na kufagia kila kitu kwenye meza ya chakula hadi sakafuni.



Shangazi Yasmine aliruka kwa hofu kumuona Alvin akivunja kila kitu kwenye chumba cha kulia chakula mithili ya mwendawazimu huku damu zikimtoka mikononi mwake. Hapo hapo akapiga simu kwa Lisa, lakini hakupata jibu.

Alipoona Alvin akizidi kupagawa zaidi kila sekunde iliyokuwa ikipita, hakuwa na jinsi zaidi ya kumpigia Maurine. Alikumbuka Maurine alikuwa akimhudumia vyema siku za karibuni.
•••
Baada ya kutoka Stears, Lisa aliendelea kutembea kando ya barabara akiwa kachanganyikiwa. Alisahau hata gari lake. Alitembea kwa muda mrefu akiwa hajui hata anapokwenda. Kufikia wakati anajikumbuka, aligundua kuwa alikuwa kwenye mlango wa Sarah Wonderland Park.

Fataki za kupendeza zililipuka juu ya ngome. Alikuwa akiitazama bila kujielewa wakati wanandoa fulani walipompita.

"Fataki ni nzuri."

"Ndio. Je, unajua ni kwa nini inafyatuliwa kwa wakati huu kila wiki?”

“Saa ngapi sasa? Ngoja nione. Saa mbili na nusu siku ya Ijumaa…”

“Ndiyo, ilikuwa ni siku kama hii na muda kama huu ambapo tajiri aliyejenga bustani hii ya burudani kwa ajili mpenzi wake alimvisha pete ya uchumba. Fataki hii ni kumbukumbu ya uchumba wao. Fataki hazikusimama usiku mzima. Fataki zililipuka angani na kuunda neno UPENDO. Tangu wakati huo, bila kujali hali ya hewa, huwa kuna maonyesho ya fataki hapa kila Ijumaa usiku. Kuna hata imani kwamba wanandoa ambao watatazama mlipuko huo wa fataki pamoja watakuwa na furaha milele.”

“Namhusudu sana huyo tajiri na mpenzi wake. Lazima wawe na furaha pamoja sasa.”

“Nafikiri hivyo pia.” Sauti ya mazungumzo yao ilififia kwa mbali.
Lisa alikuwa akipatwa na huzuni wakati aliporudi kwenye fahamu zake.

Ilikuwa nii hadithi nzuri kama nini. Akilinganisha na Mkufu wa Malkia aliomnunulia kwenye kwa pesa chafu huko Dar es Salaam, haukuwa chocote mbele ya bustani hiyo.

Ilikuwa ni aibu kwamba tajiri huyo aliishia kuoa mwanamke wa kutisha baada ya penzi lake la kweli kufa. Kwa wakati huu, alijiona kama mjinga.
Alijutia yote. Labda hakutakiwa kumwona kabisa maishani mwake Alvin na asingeishia kupata maumivu hayo ya kuvunja moyo.

Lisa alipanda ndege ya saa nne kurudi Mombasa, Shangazi Yasmine, ambaye alikuwa amesinzia kwenye kochi, aliruka kwa furaha alipomwona akirudi.

“Bibi mdogo, umerudi nyumbani?”

“Hmm.” Lisa aliburuta miguu yake mzito kwa uchovu kupanda ngazi.

"Bibi mdogo, mbona umechelewa sana kurudi?" Aunty Yasmine alimsogelea ghafla na kumuuliza huku akitabasamu. "Umekula? Una njaa? Ngoja nikuandalie chakula.”

"Sina njaa." Alizunguka kwa mkato na kumpita Aunty Yasmine.

“Unataka maziwa? Ninaweza kukutengenezea glasi sasa hivi.” Aunty Yasmini aliharakisha kwenda kumzuia kwenye ngazi.

Lisa alimtazama mwanamke huyo kwa sekunde chache kabla ya kuangaza kwenye ghorofa ya pili. “Anti Yasmine, kunanini huko juu? Kwanini unanizuia?”

Shangazi Yasmine alikuna kichwa kwa kusitasita. “Sikuwa…”

Bila kusikiliza maelezo yake, Lisa alimsukuma na ghafla nguvu zikamjia za kukimbilia ghorofani. Harufu ya kike ambayo haikuwa yake ilisikika hadi puani alipofungua mlango wa chumba cha kulala.


Lisa aligundua Alvin alikuwa amelala fofofo kwenye kitanda kikubwa. Hata hivyo, Maurine alikuwa amelala karibu naye huku mikono yao ikiwa imeshikana kwa pamoja.

Maurine alinyanyuka kutoka kitandani baada ya kusikia mlango ukifunguliwa. Sura ya wasiwasi ikamtoka alipomwona Lisa.

“Bibi mdogo, tafadhali usinielewe vibaya…”

Lisa alimkimbilia na kumpiga kofi usoni. “Nilikuwa na hisia mbaya na wewe tangu siku ya kwanza. Umeajiriwa kama nesi, na kazi hiyo haijumuishi kulala naye kwenye kitanda chetu.”

“Sikufanya hivyo,” Maurine alisema bila msaada.

“Hukufanya hivyo?” Lisa alikasirika sana hivi kwamba alishindwa kujizuia. “Nilikufukuza jana, lakini umerudi. Unajifanya wewe ndiye mama wa nyumba hii? Wazazi wako hawakukufunza adabu? Hivi una hata chembe ya aibu kweli?"

“Punguza kelele!” Alvin aliamka ghafla na kuketi kitandani huku akionekana kuishiwa nguvu. Aliuona uso wa Maurine ukiwa na michirizi ya machozi, na kulikuwa na alama ya kofi kwenye shavu lake. Kwa upande mwingine, uso wa Lisa ulikuwa ukipiga kelele za hasira. Ilikuwa dhahiri kwamba alikuwa amempiga Maurine.

"Lisa, unafanya nini?" Alvin alimtazama kwa hasira. "Unawezaje kumalizia hasira zako kwa mtu asiye na hatia mara tu unapofika nyumbani, nimekuwa nikikudekeza sana, si ndiyo?"

Lisa alishtuka. Kwa mantiki hiyo ilibidi afumbie macho kumuona mwanamke mwingine amelala kitanda kimoja na mumewe wakiwa wameshikana mikono?

“Kwanini amerudi?” Lisa alimnyooshea kidole Maurine na kumhoji kwa huzuni. "Si ulisema umemfukuza jana?"

"Naweza kumfukuza kazi na kumwajiri tena wakati wowote ninaotaka." Macho ya Alvin yalikuwa mekundu kwa hasira. Alikuwa amemfukuza Maurine kwa matakwa yake, lakini vipi kuhusu yeye? Alikwenda kwenye kulishana aiskrimu na Kelvin badala ya kuwahi nyumbani kumtunza mumewe. Alifikiri kuhusu hisia zake alipokuwa na akishikana na mwanamume mwingine hadharani?

“Sawa, nimeelewa.” Moyo wa Lisa ulivunjika vipande milioni. Kisha akatembea kuelekea chumba cha kubadilishia nguo na kuanza kubeba vitu vyake.

Kwa kweli, hakuwa na vitu vingi vya kusema. Hata kama angeondoka bila kitu chochote haikuwa na shida. Alifungasha tu vitu vyake kama kutoa ujumbe kwa njia ya vitendo kuwa alikuwa anaondoka. Aliingiza nguo zake chache kwenye sanduku na kutoka nje.

"Unafanya nini?" Alvin akamkazia macho kwa kutoamini.

Lisa aliinua kichwa kuzuia machozi yasimtiririke. “Hakuna sababu ya mimi kukaa hapa. Nawatakia maisha mema. Nitaondoka sasa hivi.” Baada ya hapo akageuka na kuelekea mlangoni.

Alvin alishika koti lake na kulitupa chini huku akimfokea kwa hasira, “Unaniacha kwa sababu ya Kelvin? Alikuambia nini? Lisa Jones, umesahau ahadi yako? Kwamba utakaa na mimi hadi nitakapopona? Kwamba utakaa nami milele hata kama ugonjwa wangu hautaisha?” Hatimaye, machozi yalitiririka kutoka kwa macho yake ya mviringo kama mto uliofurika.

Lisa allikuwa karibu kulegeza msimamo wake lakini alichefukwa ghafla aliposikia Maurine akisema kwa unyonge, “Ni kweli, Bibi Mdogo. Bwana Kimaro anakuhitaji sana. Tafadhali acha kumuumiza.”

“Kumuumiza?” Lisa alicheka. “Nani anamuumiza nani? Yuko na mimi, lakini bado anafikiria kupata mwingine zaidi. Sina muda na ujinga kama huu. Acha Maurine atibu ugonjwa wako. Hata hivyo mimi si daktari.” Lisa alitoka nje ya chumba cha kulala, akiburuta sanduku lake nyuma.

“Sitakuruhusu kuondoka.” Alvin alikimbilia mbele yake na kumshika mkono. Macho yake yalionekana kama mnyama wa porini. “Lisa, unaniacha kwa sababu mimi ni mgonjwa? Nakuambia hutakaa uondoke kwenye nyumba hii labda uwe marehemu."

"Unataka nini toka kwangu?" Lisa aliogopa hata kumwona.

"Utaelewa tu." Alvin alimtupa begani na kwenda kumfungia kwenye chumba cha upweke.

"Alvin, huwezi kufanya hivi." Mara moja Lisa alitambua nia yake na haraka akakimbia nje, akipanga kutoroka. Hata hivyo, Alvin hakumpa nafasi hiyo. Badala yake, alifunga mlango kwa nguvu na kuufunga kwa nje.

“Alvin, nakuchukia. Nimekukosea nini? Familia yako ya Kimaro ilinitenga kwenye jela yao, na sasa unafanya vivyo hivyo. Wewe ni shetani!” Lisa alipiga ngumi kwenye mlango.

“Wewe ni Ibilisi… Ibilisi…”

Sura ya: 243

Maneno hayo ya chuki yalijirudia katika ubongo wa Alvin. Mara akaziba masikio yake kwa mikono ili asisikie. Hakutaka kusikia mwanamke aliyempenda akimwita majina hayo. Alijijua ni mgonjwa, na hakutaka kumwumiza Lisa.

Akiwa amechanganyikiwa na hali hiyo, Aunty Yasmine alinyanyuka na kushika mikono yake. “Bwana Mkubwa, huwezi kumtendea hivi Bi. Mdogo. Hakusema maneno hayo kwa makusudi. Ni kwa sababu tu ana wivu kukuona ukiwa karibu na Maurine…”

Hata hivyo, Alvin alikuwa kama mwendawazimu kwa wakati huo. Sio tu kwamba hakumsikiliza, lakini hata alimsukuma Aunty Yasmine kwa nguvu. Mwanamke yule aligonga kichwa chake chini na kuzimia.

Maurine haraka akaanza kumpepea. Aunty Yasmine alilala kimya akiwa amepoteza fahamu. Sebule ilikuwa kimya ghafla. Kelele pekee zilikuwa za Lisa akiomba msaada kutoka kwenye chumba cha upweke.

Maurine alitabasamu kwa kejeli huku macho yake yakidhihirisha chuki kali, akajiwazia. ‘Lisa Jones, bila shaka hukutegemea hili kutokea’

Ndani ya chumba cha upweke, Lisa alipiga kelele hadi sauti yake ikakauka, lakini hakuna mtu aliyekuja kumsaidia. Kwa bahati nzuri, ingawa chumba hakikuwa na madirisha, kilikuwa na taa, kitanda na hali ya usafi.
Alikuwa amechoka baada ya siku ndefu. Hakutarajia kujikuta akiwa hana umuhimu kwa Alvin. Alijisikia vibaya kuona kuwa mtu aliyekufa alikuwa na nguvu sana moyoni mwake kuliko yeye aliye hai.

Hakika alipoteza ujasiri wake wote wa kumpigania mwanaume huyo. Labda hakuna kitu kizuri alichothamini ndani yake hata baada ya mateso yote aliyopata kwa ajili yake. Alilala na kupitiwa na usingizi mzito.

Kulipokucha, Lisa hakuwa tayari kuendelea kufungiwa kwenye chumba hicho cha upweke. Kwa wakati huo, alichotaka ni kutoroka humo ndani. Alipoenda kujaribu kufungua mlango muda fulani baadaye, alishangaa kuona ukifunguka bila tatizo.

Hilo lilimshangaza. Alitoka sebuleni kwa tahadhari na kugundua kuwa tayari ilikuwa ni saa tatu asubuhi. Sebule ilikuwa kimya sana. Mwanzoni, alitaka kuondoka mara moja. Hata hivyo, alikuwa na wasiwasi kwamba huenda kuna kitu kilimtokea Alvin baada ya kukumbuka hali yake ya hasira jana yake usiku. Mwishowe, aliamua kunyata kuelekea chumbani.

Alisukuma mlango uliokuwa umefunguka kidogo na kumuona Alvin akiwa amejilaza kitandani bila nguo yoyote. Maurine, ambaye alikuwa amevaa nguo nyepesi ya kulalia, alikuwa ameketi juu yake, akimpa massage ya upole mgongoni.

"Bwana Kimaro, unajisikiaje?" Sauti ya Maurine ya kubembeleza ilijaa chumbani.

Lisa alihisi kuumwa kwa kuona hivyo. Aliondoka mahali hapo bila kuangalia nyuma. Alikuwa mjinga kiasi gani kuhangaikia hali yake baada ya kumfungia kwenye chumba cha upweke usiku kucha wakati yeye alikuwa kazama katika faraja ya Maurine?

Alipowawazia wawili hao wakifanya jambo la faragha kama lile kitandani mwake, Lisa alihisi kichefuchefu. Aliamua kuachana na mtu huyo kwa muda usiojulikana.

Pamoja na hayo, kuna kitu hakujua. Baada ya kuondoka, Maurine alitoka kwenye mwili wa Alvin na kumtazama mwanaume huyo. Bado alikuwa amepoteza fahamu. Alivaa na kumpigia Rodney simu.

Takriban nusu saa baadaye, Rodney na Chester walifika wakiwa na wasiwasi mwingi. Maurine aliwaambia marafiki hao wa Alvin waliokuwa na wasiwasi mwingi. “Nilirudi jana usiku baada ya kupigiwa simu na Aunty Yasmine. Nilimpatia dawa na hatimaye akatulia. Lisa aliporudi nyumbani alinipiga bila hata ya kunisikiliza. Alvin aliamka katikati ya ghasia na kuanza kufokeana naye.”

“Alvin alipoteza udhibiti wa hasira zake baada ya hapo, na Lisa akasema angeondoka. Alimfungia ndani ya chumba peke yake na kumjeruhi kwa bahati mbaya Aunty Yasmine. Niliita gari la wagonjwa usiku huohuo ili kumpeleka Aunty Yasmine hospitali. Sasa, sijui nini kingine cha kufanya,” Maurine alisema kwa maelezo marefu.

Alama ya kofi la Lisa kwenye shavu lake bado ilikuwa ikionekana na alikuwa amevimba. Rodney alipiga ukuta kwa ngumi aliposikia hivyo. “Lisa anaumwa kabisa. Nitamfundisha somo…”

“Tulia.” Chester alimshika rafiki yake mkono.

“Angalia alichomfanyia Alvin. Anajua kwamba akili yake haijatulia, lakini bado anamkasirisha kimakusudi. Nadhani anajaribu kumfanya apoteze akili ili aweze kurithi utajiri wake.”

Maurine alisema kwa unyonge, “Nilifungua mlango wa chumba alichofungiwa kwa siri asubuhi ya leo ili kumruhusu atoke. Nafikiri… Si wazo zuri kumfungia mtu hivyo. Unafikiri nini kitatokea ikiwa Alvin ataamka na kumkuta hayupo?”

Chester alimpongeza, “Umefanya jambo sahihi. Alvin amekosea sana kumfungia.”

“Lakini ninahofia atakasirika akimkuta Lisa ameondoka…” Mwonekano wa wasiwasi ukauwasha uso wake.

“Tutamwambia kwamba sisi ndio tuliomwacha aende zake,” Chester alimtoa wasiwasi.

"Asante."

Muda si mrefu Alvin alizinduka. Alishika kichwa chake kwa mikono yote miwili ili kupunguza maumivu ya kichwa.

“Unajisikia vizuri?” Rodney aliuliza kwa umakini.

Alvin aliinua kichwa chake kuwatazama kwa kukunja uso. “Mbona wote mko hapa? Lisa yuko wapi? Alirudi nyumbani jana usiku?"

Wote wakamtazama kwa mshangao. Rodney na Chester wakatazamana. Sekunde chache baadaye, Chester aliuliza, “Alvin, hukumbuki kilichotokea jana usiku?”

"Nini kimetokea? Si nimelala usiku kucha?” Alisikika kama kachanganyikiwa. “Niligombana naye juzi na jana nikasubiri hadi usiku sana bila kumuona. Niliingia kitandani nikiwa nimechanganyikiwa na kwa namna fulani nililala tu.”

Rodney alishtuka kweli. Chester alimpiga bega rafiki yake. “Kusema ukweli, uligombana na Lisa tena usiku wa juzi na akaondoka kwenye nyumba hii. Kwa bahati nzuri, Shangazi Yasmine alimpigia simu Maurine jana usiku. Jana tena Lisa alirudi usiku mkagombana tena. Ulimuumiza Aunty Yasmine katika harakati hizo, akapelekwa hospitali…”

Uso wa Alvin ukabadilika mara moja. "Hiyo haiwezekani. Sikumbuki lolote kati ya hayo.”

"Inaonekana hali yako imekuwa mbaya zaidi kuliko tulivyotarajia. Unaonyesha hata dalili za kuweweseka na kupata maluweluwe. Hali yako ni tata sana.” Chester akakunja uso ake.

Alvin alikunja ngumi kwenye blanketi. "Hapana. Nimekuwa nikijisikia vizuri zaidi hivi karibuni.”

“Lazima ni kwa sababu Maurine anakuhudumia vizuri.” Rodney alisema kisha akaongeza kwa hasira, “lakini Lisa anaendelea kukuchokoza. Nadhani ni bora ukiacha kuonana naye kwa wakati huu. Acha Maurine aendelee kukutunza. Ni kwa manufaa yako mwenyewe.”

“Nakubaliana na Rodney wakati huu. Ni bora ukijiweka mbali na Lisa. Nina hakika hutaki kumdhuru, sivyo?” Chester alisita. “Hivi majuzi nilisikia kuhusu huyu mtaalamu wa saikolojia, Nyasia kutoka nje ya nchi. Inavyoonekana, anaweza kuponya mgonjwa yeyote. Lakini yeye ni mtu mwenye kazi nyingi, kwa hivyo inachukua muda mwingi na bidii kuwasiliana naye.”

"Wasiliana na mtu huyu kwa njia yoyote ile." Alvin alihimiza.

Ingawa Lisa alikuwa amemwacha kwa usiku mmoja tu, hakuweza kuzuia msukumo wa kwenda kumtafuta. Hata hivyo, alihitaji kujizuia ili asimdhuru tena.
•••
Lisa alikaa hotelini baada ya kuondoka kwa Alvin. Siku iliyofuata, alishirikiana na Pamela kutafuta nyumba. Wakati huo, alikuwa ameamua kununua nyumba ili awe na mahali pake mwenyewe huko Nairobi.

“Hivi kweli haurudi nyuma? Usibadili mawazo yako tena Alvin atakapokuja kukutafuta siku chache zijazo.” Pamela hakuweza kujizuia kumtania rafiki yake.

“Wawili hao walikuwa wamelala kwenye kitanda changu. Unafikiri bado ninaweza kurudi huko?" Lisa alihisi kana kwamba moyo wake ulikuwa umechomwa kisu alipokumbuka tukio lile. "Akili na mwili wangu havitaki kabisa kumsikia Maurine. Uhusiano wetu ulikuwa umeanza kuimarika lakini baada ya kuja Maurine kila kitu kimesambaratika tena.”

“Uko sahihi. Inachukiza sana. Kwa kuwa hawezi kumsahau Sarah Njau, kaamua kukaa na binamu yake ili ajisikie vizuri. Kwanini bado anataka kukuweka karibu?” Pamela akamshika mkono. “Twende tukanunue nyumba. Ninajua mahali pazuri.".....ITAENDELEA....

Unafikiri nini kitafuata hapo, maana simulizi inazidi kuwa tamu kila siku lakini sina budi kuhitimisha kipande hiki ila niwasihi tukutane katika episode zijazo ili kujua nini kitafuata kwenye mkasa huu wa kusisimua na kuelimisha unaokwenda kwa jina la LISA.