JINA LA SIMULIZI............................LISA
AUTHOR...........................JOMBA WAJO
SPONSORED BY......SIMULIZI ZA DULLY
WHATSAPP..........................0628924768
SEHEMU YA................................240-241

Sura ya: 240

Alijiuliza mambo mengi sana. Alvin alikuwa ameanza kumtenga kwa ajili ya marafiki zake na Maurine ndani ya muda mfupi tu. Je, mwaka mmoja au miwili baadaye ingekuweje? Lisa aligusa uso wake ulioharibika na akakosa matumaini. Je, Alvin bado angempenda kwa moyo wake wote? Aligeuka na kuelekea kwenye maktaba ili kujisahaulisha na mawazo hayo kwa kufanya kazi zake za ziada.

Muda mfupi baadaye, alisikia sauti ya gari ikiondoka. Alihisi pengine ni Maurine ambaye alikuwa akiondoka. Lakini, Lisa hakutoka nje ya maktaba.

Saa tano usiku, mlango wa maktaba ulisukumwa kwa nguvu. Alvin aliingia huku akiwa amekunja uso. “Lisa, unafanya nini? Angalia muda sasa, ni saa ngapi na bado haujalala, bado una hasira na Maurine, sivyo? Tayari ameondoka.”

“Unaweza kwenda kulala kwanza? Bado nina jambo la kushughulikia.” Lisa aligeuza macho yake baada ya kumtazama. Hakuweza kukubali ukweli kwamba alikuwa amebadilika kwa sababu ya mwanamke mwingine.

“Inatosha. Uvumilivu wangu una mipaka yake.” Alvin alimvuta kutoka kwenye kiti na kusema kwa jeuri, "Usiniangalie kwa sura ya kuchukiza, amka twende!"

"Usinishike kwa mkono uliotoka kumshika mwanamke mwingine." Lisa alimsukuma kwa hasira.

Alvin akapandisha hasira. "Unawaza nini Lisa? Mkono wake ulikuwa umekatwa na chupa, kwa hiyo nikamwomba Aunty Yasmine aufunge bandeji. Hilo nalo ni la kuonea wivu? Ina maana siwezi kumsaidia mwanamke yoyote kwa sababu nipo na wewe?”

Lisa alijaribu kuzuia uchungu moyoni mwake kisha akasema kwa sauti ya kwikwi, “Hujawahi kumjali hivi Hans wala Shani, lakini Maurine? Unambembeleza na kuongea naye kwa upole kuliko hata mimi, unafikiri nitajisikiaje?”

“Huna akili!” Alvin akauachia mkono wake. "Maurine ni muuguzi wangu, lazima ni mtii ili anihudumie vizuri. Suala la afya halihitaji mzaha.”

“Sijakukataza kuwa naye, ila ni lazima uchague moja, mimi au yeye” Lisa alimpa mtihani.

“Kwa kuwa unafurahia kukaa hapa, endelea kukaa na uchukue fursa hii kujitafakari. Unaweza kuwa na wivu, lakini kuna kikomo kwa hilo.” Alvin akaufunga mlango kwa nguvu na kuondoka huku akiwa amekunja uso.

Lisa alikaa kwenye kiti kimya bila kujua kuwa machozi yalikuwa yakimtoka. Usiku huo hakuingia chumbani hata kidogo.

Alvin alijirusha huku na kule kitandani peke yake kwani usingizi ulikuwa wa shida. Tangu Maurine aanze kumhudumia, hakuwa amepatwa na tatizo la kukosa usingizi. Usiku huo, alilala kwa saa moja tu. Alipoamka asubuhi iliyofuata, uso wake ulikuwa umekunjamana kwa kukosa usingizi wa kutosha. Hakutaka hata kuiona sura ya Lisa. Kwa hiyo, aliondoka nyumbani bila kupata kifungua kinywa.
•••
Baada ya kufika ofisini, Lisa alimpigia simu Hans. "Nenda kapeleleze kinachoendelea katika kampuni ya ‘New Era Advertisings’. Kisha uniletee taarifa."

Lisa alimpigia simu Pamela baadaye. "Nisaidie kitu kimoja shosti, najua kuwa una marafiki wengi zaidi hapa Nairobi kuliko mimi. Umewahi kusikia kuhusu Charity Njau anaye milikikampuni ya New Era Advertisings ?"

“Oooh! Charity Njau? Kweli,” Pamela alijibu kwa mzaha. "Nilisikia kwamba alikuwa mpenzi wa zamani wa Chester. Kuna nini kwani?"

“Sawa, nahitaji kujua zaidi ya hilo!”

Pamela aliongeza, “Nilivyosikia ni kwamba, Charity ana sifa mbaya. Uvumi umeenea kwamba yeye ni mkatili sana. Anaweza kufanya lolote bila kujali utu kwa ajili ya pesa na madaraka. Amefikia hata hatua ya kuwadhulumu ndugu zake ili kuwa mtendaji mkuu wa New Era Advertisings. Mama yake alikuwa ni sekretari tu wa Bwana Langa Njau, mwanzilishi wa kampuni hiyo ya New Era Advertisings na ndipo Charity akazaliwa. Ni baada tu ya mke halali wa Langa Njau kufariki ndipo mama yake Charity aliiteka familia ya Njau . Nilisikia mama yake pia ni katili.”

Lisa aliuliza kwa udadisi baada yakusikiliza maelezo marefu ya Pamela, "Mke wa zamani wa Langa ana waoto?"

“Swali lako linanitia wasiwasi,” Pamela alisema kwa kufadhaika. “Namfahamu mwanamume mmoja anaitwa Thomas Langa Njau. Nilihudhuria hafla moja siku chache zilizopita ambapo Thomas Njau alionyesha kuvutiwa nami, na tangu wakati huo, amekuwa akinisumbua sana.”

“Thomas Njau ?” Lisa alikunja uso. "Jina hili siyo geni kwangu."

Akiwa na mawazo, Lisa aliinuka na kusimama ghafla. “Nimekumbuka sasa. Unaikumbuka ile ishu ya Kelvin kuchomwa kisu na kupoteza figo hospitali? Enhee, basi mtu mmoja anayeitwa Zigi Kabwe alitaka kuniua. Lakini kwa bahati, Kelvin alikuja kuniokoa. Baadaye, nilisikia kutoka kwa polisi kwamba chanzo cha Zigi kutaka kuniua ni kulipiza kisasi kifo cha dada yake.”

Lisa akaweka kumbukumbu zake sawa na kuendelea.

“Thomas kutoka familia ya Njau ya hapa Nairobi alitaka kumbaka dada yake Zigi, Lily Kabwe. Lily alijiua kutokana na mfadhaiko. Familia ya Kabwe ilimshtaki Thomas, na alitakiwa kutumikia kifungo chake. Hata hivyo, Alvin alimtetea kwenye kesi na akashinda.”

“Ndiyo, nimekumbuka uliwahi kunisimulia kipindi Kelvin kalazwa hospitali.” Pamela alipigwa na butwaa. “Kwanini ameamua kunisumbua? Hataweza kunibaka kweli?”

"Kwani anajua unapoishi?" Lisa alikuwa na wasiwasi juu yake.

“Eeh! Anajua. Sijui hata alipajuaje. Nimewahi kumkuta mara mbili akinisubiri nje ya nyumba yangu ninapotoka kazini jioni.” Kadiri Pamela alivyozidi kufikiria juu yake, ndivyo alivyokuwa akiogopa zaidi. “Sidhani kama ana nia njema na mimi. Ana husiana vipi na Alvin? Kwanini alimsaidia kesi yake?”

“Bado sijajua.” Lisa alijibu. “Sidhani kama inafaa kuendelea kukaa hapo. Kaa hotelini kwa muda huu,” Lisa alimshauri kwa wasiwasi. "Nipigie simu mara moja ikiwa chochote kitatokea."

“Sawa. Nakubaliana na ushauri wako.”

Baada ya kumaliza kuongea na Pamela, Hans aliingia akiwa na habari za uchunguzi wa kampuni ya New Era advertisings.

“Bi. Jones, New Era Advertisings hujihusisha na matangazo ya redio, televisheni, magazetini, mtandaoni, mabango ya barabarani na promosheni ya bidhaa mbalimbali. Kwa muda mrefu imefanya kazi pamoja na mtandao wa vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kampuni ya Alvin, Alvinarah Media Network Group, au AMEN Group kwa kifupi, ambayo ni kampuni iliyo ndani ya Alvinarah Group of Compannies. Pia inashirikiana na KIM Outdoors iliyo chini ya KIM International kwa ajili ya mabango ya barabarani. Lakini, Charity Njau, bosi wa New Era Advertisings kwa namna fulani alimkasirisha Alvin Kimaro, na kusababisha Alvinarah na KIM International kughairi ushirikiano wao. Kwa hivyo sasa makampuni yanayojitangaza kupitia New Era Advertisings yanajitoa kwa sababu kampuni hiyo haina uwezo wa kuwafikia wateja wao tena.”

"Charity Njau kamchukiza Alvin Kimaro, kwa lipi?” Lisa aliuliza kwa kutilia mkazo neno la mwisho.

Hans akajibu. "Kwa kweli, Charity amekuwa akisimamia New Era Advertisings vizuri kabisa kwa miaka michache iliyopita, lakini kwa bahati mbaya..." Hans akashindwa kumalizia.

"Usijali." Lisa aliitikia kwa kichwa. “Unaweza kunipatia namba ya Charity? Ningependa kukutana naye.”

Kulikuwa na mashaka mengi akilini mwake ambayo alitaka kufafanuliwa.
Thomas Njau, Charity Njau, Alvin Kimaro, Rodney Shangwe, Chester Choka, Zigi Kabwe, Maurine Langa…Je, watu hawa walikuwa na uhusiano gani?

Ilimchukua Hans muda kupata namba ya simu ya Charity. Kisha, Lisa akampigia Charity simu.

"Huyu ni Charity Njau kutoka New Era Advertisings. Nikusaidie nini?” Mwanamke huyo alikohoa katikati ya maneno yake.

"Lisa Jones. Je, una homa, Bi. Njau ?” Lisa alipigwa na butwaa.

"Ndio, nina homa kidogo."

"Una muda tukutane kwa chakula cha jioni leo?" Lisa alikuwa na hakika kwamba Charity asingekataa ombi lake kwani alikuwa akihitaji msaada. Lakini kinyume na matarajio yake yote, Charity alimkataa. "Sidhani kama naweza, Bi Jones. Najua una mashaka mengi akilini mwako, lakini New Era Advertisings sasa iko kwenye changamoto kubwa. Nikikutana nawe, kampuni yangu itaishia katika hali mbaya zaidi. Huwezi kunisaidia.”

Sura ya: 241

“Ni sawa, kama unafikiria hivyo. Lakini unaweza kunasidia kitu kimoja, unaweza kuniambia Maurine Langa ni nani?”

“Bi. Jones, usitake kujua kuhusu hilo.” Charity alijibu kwa mkato.

"Inaonekana una wasiwasi na mimi." Lisa aliishika simu yake kwa nguvu. “Jana ulisema Alvin na marafiki zake wanadanganya na kunilaghai, unakumbuka? Nadhani ulikuwa unanionea huruma.”

“Haina maana tena. Maadamu wewe ni jasiri, huhitaji kujali wengine wanafikiri nini juu yako,” Charity alijibu kwa sauti ya chini.

Lisa alitabasamu kwa uchungu. “Sawa, sitakulazimisha. Hata hivyo, kuna jambo moja zaidi. Una kaka anayeitwa Thomas Njau? Unaweza kumwomba aache kumsumbua rafiki yangu Pamela? Mwambie kwamba yatampata makubwa kama ataendelea kumfuatilia.”

“Thomas Njau …” Sauti ya Charity ilijawa na papara. “Sawa, nitamwambia. Lakini ngoja nikukumbushe jambo pia, Bi Jones. Mwambie Maurine akae mbali na Alvin haraka iwezekanavyo.”

Moyo wa Lisa ulirukaruka. “Tayari nimemfukuza jana usiku.”

“Nina wasiwasi kwamba baadhi ya watu hawatakubali aondoke…”

Kabla Charity hajamalizia maneno yake, zogo likasikika nje ya ofisi ya Lisa. Rodney aliingia ndani ya ofisi huku akimburuta Shani nyuma yake.

"Samahani kidogo, kuna dharura imejitokeza nitakupigia baadaye." Lisa alimwambia Charity na kukata simu.

Baada ya kukata simu, Lisa alielekeza macho yake kwa Rodney ambaye alionekana kuhamaki. Ghafla, kitu kiliingia akilini mwake. Je, hiki ndicho Charity alichomaanisha kwamba baadhi ya watu hawatokubali Maurine kuondoka? Lisa alizidi kuchanganyikiwa.

"Bwana Shangwe, ni nini kimekuleta hapa ofisini kwangu?" Lisa aliinua kichwa chake na kuuliza kwa hasira.

“Acha kujifanya, Lisa. Ulimlazimisha Alvin kumfukuza Maurine?” Rodney aliweka mikono yake juu ya meza huku akiwa na hasira machoni pake. "Unawezaje kuwa na akili ndogo kiasi hicho? Nilikuwa nimeanza kukuheshimu lakini sasa unanifanya nikudharau.”

Lisa alimtazama bila kupepesa macho hata kidogo. "Sina uhusiano na wewe, kwa hivyo sijali jinsi unavyoniona."

“Mimi ni rafiki mkubwa wa Alvin na ninamuelewa. Unafikiri Alvin atakupenda mtu mwenye kuchukiza kama wewe?" Rodney alidhihaki, “Maurine alikuwa anakuheshimu, lakini unajifanya kana kwamba wewe ni wa matawi ya juu. Unafikiri unaweza kuwadharau watu wengine kwa sababu ya hadhi yako kama Bi. Kimaro? Kweli, kwa jinsi ulivyo, hakuna mwanaume ambaye atakupenda kama Alvin atakuacha.”

Maneno yake yalipenya moyoni mwa Lisa. “Tangu jana unamtetea Maurine. Wewe ni nani yake hasa, huh? Mshenga, au kuwadi wa Alvin? Unategemea kwamba atachukua nafasi yangu na kuwa shemeji yako mpya?”

Rodney alishindwa kujizuia. “Umerukwa na akili. Ninamchukulia Maurine kama dada yangu, na siwezi kuvumilia jinsi ulivyomnyanyasa.”

“Nilimnyanyasa?” Lisa alijihisi kukosewa adabu sana. "Maurine ndo kakuambia hivyo?"

“Maurine hakusema. Yeye ni mkarimu sana, lakini mimi si mpumbavu.” Rodney alimwonya vikali, “Lisa, ukithubutu kumnyanyasa tena, nitakufanya kitu kibaya hata Alvin hatakutetea.”

Rodney alipofika mlangoni wakati akiondoka, alitazama nyuma. “Nimemfahamu Alvin kwa zaidi ya miaka 20. Wewe umemjua kwa muda gani? Fikiri juu ya hilo.” Lisa alibaki ameduwaa.

Mpaka inafika usiku, Alvin hakumpigia simu kabisa. Kwa kuwa Shani alikuwa naye na alishuhudia yote, Lisa aliamini kwamba Alvin alikuwa anajua kilichotokea siku hiyo. Alijiuliza labda ni Alvin ndiye aliyemtuma Rodney kufanya aliyoyafanya. Kwa hasira, Lisa hakurudi Mombasa baada ya kazi siku hiyo. Alikula chakula cha jioni na kuanza kutembea kwenye mitaa ya katikati ya jiji la Nairobi peke yake.

Aliingia kwenye duka la Stears na kuagiza aiskrimu. Ghafla, sauti ya upole ya mwanaume, iliyozoeleka masikioni mwake ilisikika nyuma yake.
"Ice cream ni tamu eeh? Ninunulie moja basi.”

Lisa aligeuza kichwa chake nyuma na kumuona Kelvin akiwa amesimama nyuma yake akiwa amevalia suti ya kijivu. Alipendeza kiasi chake, na wanawake kadhaa walikuwa wakimtolea macho ya wivu.

Kelvin aliinamisha kichwa chake na kumtazama Lisa machoni. Macho yake yalijawa na hisia za mapenzi.

"Ni muda umepita tangu tukutane." Lisa alisema bila kujiamini.

"Ndio. Nilikuona wakati natoka kazini sasa hivi, kwa hiyo sikuweza kujizuia kukufuata hapa,” Kelvin alijibu kwa huzuni. "Umekuwaje? Huonekani kuwa na furaha sana sasa hivi…”

“Hapana. Nilikuwa nafikiria tu mambo ya kazini,” Lisa alikanusha kabisa.

"Nilidhani kwa kuwa uko na mwanaume unayempenda, ungekuwa unafurahi muda wote.” Kelvin alicheka kwa namna ya kujidharau.

“Pole, Kelvin…” Lisa alilemewa na hatia. “Sikukusudia kukuumiza.”

"Pole haijawahi kumponya mtu." Tabasamu la uchungu lilienea kwenye uso wa Kelvin. Alichukua ice cream kutoka kwa mhudumu kisha akamkabidhi moja Lisa.

"Kuna dharura imetokea. Kwaheri.” Lisa alitbofyabofya simu yake kwa uongo na kweli kisha akatoa kisingizio cha aibu kwani hakuthubutu kumkabili Kelvin.

“Hutaki hata kukaa nami kwa muda? Lisa, usinifanyie ukatili sana.” Kelvin aliongea kwa maneno ya kusihi. Lisa akawa mpole.

Baada ya wote wawili kuketi, alimsikiliza Kelvin akiongea kuhusu maisha yake na mambo yanayohusiana na kampuni yake. Hawakutambua kuwa kuna paparazi aliwapiga picha kwa siri. Nusu saa baadaye, Lisa alitoa tena udhuru wa kuondoka.

“Subiri…” Kelvin alimshika mkono ghafla. Lisa hakupenda kushikwa na Kelvin hivyo akajinasua haraka haraka.

"Hutaki hata nikikugusa tu?" Macho ya Kelvin yalijawa simanzi. Alihisi kama pigo kwake. "Tangu zamani hupendi nikuguse."

“Kelvin, lazima nikiri kwamba nina deni kubwa kwako. Nilifikiria kutumia maisha yangu yote na wewe ili kufidia hilo, lakini niligundua kuwa mahusiano hayawezi kulazimishwa. Ninaweza kutoa figo yangu na kukulipa kama hutajali,” Lisa alisema kwa uthabiti.

Kelvin alipigwa na butwaa. Muda mfupi baadaye, uso wake wa kupendeza ukaonekana wenye huzuni. “Lisa, unadhani mimi ni mtu wa aina gani? Ni kweli umenitupa, umechagua kuwa na Alvin, lakini nakupenda. Sihitaji unijibu hivi.”

Kelvin alinyanyuka taratibu na kutoa simu yake mfukoni. Alibofya na kufungua picha na kumwonyesha Lisa. Lisa aliipokea simu bila kujijua.

Picha hiyo ilikuwa ya msichana mwenye umri wa kati ya miaka 17 na 18. Alikuwa na uso mdogo, wenye umbo la mviringo na ngozi nzuri. Tabasamu lake lilikuwa tamu, na kulikuwa na vishimo viwili ‘dimpos’ mashavuni mwake. Alionekana mrembo, mzuri na mwenye kuvutia sana machoni. Lisa alishtuka kuona msichana huyo anafanana sana na Maurine. Lakini, macho ya Maurine hayakuwa mazuri na ya kupendeza kama ya msichana huyo.

“Huyu ni…”

“Mpenzi wa zamani wa Alvin, ambaye pia alikuwa mpenzi wake wa kwanza.” Kelvin alijibu kabla Lisa hajamaliza hata swali lake.

Lisa akajikuta anakosa la kusema. Ingawa alikuwa amebashiri jibu kwa kiasi fulani, alikataa kuamini. Hata hivyo, maneno ya Kelvin yalikuwa yamefichua ukweli, na yaliufanya moyo wake kubana sana kiasi cha kukosa hewa. Haishangazi Charity alisema kwamba Alvin na rafiki zake walikuwa wakimdanganya na kumlaghai. Si ajabu Charity alimtazama kwa huruma.

Aligundua ni kwanini Alvin alimuajiri Maurine kama muuguzi wake, ni kwa sababu alianana na mpenzi wake wa zamani. Ha! Alijisikiaje kumuona Maurine kila siku? Je, alimkumbuka mpenzi wake wa zamani?
Maurine alikuwa nani kwake, basi? Kwa hiyo yeye hakuwa moyoni mwa Alvin? Hivi ndivyo Alvin alimaanisha kwa upendo usiobadilika?

“Mbona unanionyesha picha hii?” Lisa alimwangalia Kelvin kwa hasira.

"Haijalishi utanichukuliaje, lakini nilihangaika sana kupata picha hii."
Kelvin aliongeza kwa uwazi, “Familia nyingi tajiri hapa Nairobi zinajua kuhusu ex-girlfriend wa Alvin. Huko nyuma, alimdekeza kama binti wa kifalme na kuambatana naye popote alipoenda. Hata alisisitiza kumuoa licha ya pingamizi la familia ya Kimaro. Kwa kuwa alikuwa binti mkubwa katika familia ya Njau , Alvin aliisaidia sana familia ya Njau kwa gharama yoyote, hata akamfungulia baba yake kampuni kubwa ya matangazo, New Era Advertisings kwa mtaji kutoka familia ya Kimaro. Sarah alipenda sana viwanja vya burudani, kwa hivyo Alvin alitumia pesa nyingi kujenga Sarah Wonderland Park kwa ajili yake.”......TAENDELEA.....

Unafikiri nini kitafuata hapo, maana simulizi inazidi kuwa tamu kila siku lakini sina budi kuhitimisha kipande hiki ila niwasihi tukutane katika episode zijazo ili kujua nini kitafuata kwenye mkasa huu wa kusisimua na kuelimisha unaokwenda kwa jina la LISA.