JINA LA SIMULIZI............................LISA
AUTHOR...........................JOMBA WAJO
SPONSORED BY......SIMULIZI ZA DULLY
WHATSAPP..........................0628924768
SEHEMU YA................................238-239
Sura ya: 238
“Kwanini umzuie…”
Kabla hata Chester hajamalizia sentensi yake, zogo kubwa lilisikika kati ya walinzi waliokuwa wakimzuia binti mmoja aliyekuwa akilazimisha kuingia ndani.
“Samahani, Bibiye. Huwezi kuingia.” Sauti ya mlinzi ilisikika. “Hujakaribishwa mahali hapa, kuwa mstaarabu sivyo utaumizwa bure.”
“Hao wanaume wote wananifahamu, kama hamuniamini hebu niachieni muone kama watanifukuza?” Yule binti alijitetea huku akifurukuta katikati ya mikono ya walinzi.
Lisa alipogeuza kichwa chake na kutazama upande ule, mara moja akamkumbuka kuwa ni yule binti ambaye alimkuta barabarani gari lake likiwa limezama kwenye matope.
"Charity, ni nani aliyekuruhusu kuja hapa?" Rodney alisimama ghafla. Uso wake ulijawa na karaha na chuki. “Potea sasa hivi kabla mashetani yangu hayajapanda.”
"Nimekuja kumtafuta Alvin Kimaro." Macho ya Charity yalilegea, lakini aliendelea kumtazama Alvin kwa nguvu. “Bwana Kimaro, ningependa kuzungumza na wewe kuhusu New Era Advertisings…”
“Unafikiri Alvin atakusikiliza?” Rodney alidhihaki, “Familia ya Njau imemkosea sana Alvin. Hulifahamu hilo? Hebu walinzi mburuteni mumtoe nje, haraka.”
Kundi la walinzi wa nyumba hiyo walimzunguka Charity mara moja na kumshika mabega yake pande zote mbili.
"Subirini." Lisa aliinuka ghafla. "Yeye ni mwanamke tu. Msimnyanyase kiasi hicho!”
"Hujui chochote kuhusu huyu mwanamke, wewe ni wakuja tu hapa Kenya, bora ungeacha kuingilia mambo yasiyo kuhusu!" Rodney alifoka. "Lisa, tafadhari usinipe wakati mgumu sana usiku wa leo, unasikia?"
"Rodney, kwa kweli tabia yako si nzuri." Uso wa Lisa ulionesha chuki waziwazi. "Tangu nilipoingia hapa unaniandama tu, kwanini?"
Rodney hakutaka kumsikiliza Lisa, akamgeukia Alvin. " Alvin, mdhibiti mkeo!"
“Lisa! Njoo huku.” Kwa mshangao, Alvin alizungumza kwa sauti ya kina wakati huu, "Usijisumbue juu ya jambo hili."
“Jambo gani? Ina maana huoni jinsi Rodney alivyokuwa mkali kwangu tangu niingie mahali hapa?” Lisa aliuliza kwa hasira.
“Simzungumzii Rodney, namaanisha Charity. Achana naye…” Alvin alionya.
Lisa aliitazama sura ya binti huyo huku akiwa amekata tamaa. "Nimeonana naye njiani wakati nakuja hapa, yeye ni rafiki yangu, bila shaka mtamruhusu aingie."
Lisa aliona kwamba wanaume wote watatu walikuwa wakimtazama kwa sura zisizo za kawaida. Aliweza kuhisi kwamba macho yao hayakuwa ya kirafiki, lakini hakujali. Alichojali tu ni kumsaidia yule binti.
Macho ya Alvin yalitoa ishara ya onyo kali alipomtazama Lisa. Ilikuwa ni muda tangu alipomtazama kwa jicho kama hilo kwa mara mwisho. “Lisa, ni afadhali usifike mbali sana. Charity hastahili kuwa rafiki yako. Kaa mbali naye.”
“Nisipofanya hivyo?” Lisa alishupaza uso wake na kumwangalia Alvin machoni.
Alvin aliinua midomo yake kwa hasira, lakini Rodney hakuweza tena kuvumilia tabia yake. "Lisa, umeshamaliza? Acha ujinga. Kuna kikomo cha uvumilivu. Alvin anaweza kukuvumilia ikiwa utathubutu kumsogelea mwanamke huyu, lakini hakika mimi sitaweza.” Lisa alibaki kimya huku macho yakimtazama Alvin.
Hata hivyo, Alvin aliweka uso mkavu bila kusema neno lolote. Hali ilikuwa ya wasiwasi kwa muda. Wakati huo, Charity alitabasamu ghafla. "Ni sawa, Bi Jones. Ukisisitiza kuwa rafiki yangu, Bwana Kimaro anaweza kukupa talaka.”
Lisa alimtazama binti huyo kwa mshangao. Mwanzo alimwita kama Bi. Kimaro walipokutana kwa mara ya kwanza, lakini kwa wakati huo akamwita Miss Jones tena, ilimshangaza sana. Ilionekana alikuwa anamfahamu, japo kwa kiasi.
Ilimshangaza pia kwanini Alvin na marafiki zake walimchukia sana Charity. Hakuona kama Charity kama ni mtu mbaya. Badala yake, alihisi kwamba Charity alikuwa wazi na mwaminifu.
“Sawa Bi. Jones, naona hapa ni wewe peke yako ndiye mwenye moyo wenye kujali angalau. Niache tu nipambane na hali yangu nisije nikakuingiza matatizoni.” Charity alisema kwa sauti ya kugusa moyo.
“Achana na Lisa, Charity,” Alvin alionya kwa sauti ya huzuni.
“Nimekosea? Kwa kuwa ni mke wako, unatakiwa kumlinda wakati wote, hasa marafiki zako wanapokuwa karibu.” Charity alikoroma kwa kejeli. "Unawaacha tu marafiki zako wamfokee wanavyoisikia, hivi, umewahi kufikiria hisia za mke wako, Bwana Kimaro?”
Koo kavu la Lisa lilijisikia vizuri kidogo. Kinyume na matarajio yake, mtu wa kwanza kuzifikiria hisia zake hakuwa Alvin bali ni mgeni ambaye alikutana naye mara mbili tu.
“Inatosha, Charity. Acha kuwachonganisha Alvin na mkewe.” Chester, ambaye alisimama kando ya jiko la kuchomea nyama, hatimaye alizungumza. Alikuwa amevaa nguo zilizompendeza sana. Hata hivyo, sura yake ilionyesha chuki kali. "Bado una ulimi mkali kama zamani. Unaudhi kama nini!”
Maneno yake yalimchoma moyo Charity. Chester alionekana kuwa mzuri zaidi, lakini chuki yake kwake ilikuwa bado ile ile. Charity alitabasamu kwa uchungu na kusema. “Nimekuwa nikijaribu kuwakwepa kwa miaka hii yote. Kwa kadiri ninavyokumbuka, sidhani kama nimefanya jambo lolote lile lililowakera. Lakini kwanini mnaifanyia hivi kampuni ya New Era Advertisings? Bwana Kimaro, Alvinarah Media Network Group ni muhimu sana kwetu. Bila mtandao wa vyombo vya habari, matangazo yetu tutauzia wapi? Alvin nakuomba pleasee…”
“Ina uhusiano gani na mimi?” Alvin alidhihirisha kiburi chake.
Uso mzuri wa Charity ulizidi kufifia. “Bwana Kimaro, kama kuna tofauti zozote kati yetu, tunaweza kuziweka kando ya biashara na kuzungumza kibinafsi? Ukinikatia mtandao wako wa vyombo vya habari bila shaka utakuwa umekata nusu ya mapato ya kampuni yangu kwa mwaka. Sawa, pengine utakuwa umenipa somo mimi, lakini vipi kuhusu mamia ya wafanyakazi wanaotegemea kuendesha maisha yao kutokana na ajira zao kwenye kampuni ya New Era Advertisings?”
Kuona jinsi Charity alivyokuwa hoi ilimkumbusha Lisa hali yake ya zamani.
"Bwana Kimaro, labda utazingatia ombi langu nikikuomba nikiwa nimepiga magoti?" Charity alimkazia macho Alvin usoni kwa kufadhaika.
Rodney alisema kikatili, “Kuomba radhi hakusaidii, Charity. Hili ni somo kwako. Rudi nyuma na ujitafakari. Kuwa binadamu mwenye heshima. Nani anajua, tunaweza kufikiria kuipa familia ya Njau nafasi ya kuishi wakati ujao.”
“Nyie watu hamjabadilika hata kidogo. Hata sijajua nimefanya nini kilichowaudhi,” Charity alitabasamu kwa kujidharau. Alipogeuka tu na kuwa tayari kuondoka, alipigwa na butwaa baada ya kuuona uso wa Maurine.
Maurine aliingia katika hofu na kujificha nyuma ya Alvin. Alvin alipoona hivyo alizidi kuchukia. "Charity, potea mara moja."
Charity akakoroma kwa mara nyingine. Macho yake yaliwakodolea wanaume wale watatu kwa zamu kabla hajamtazama Lisa kwa huruma. "Wanaume watatu wanamdanganya na kumlaghai mwanamke mkarimu asiye na hatia. Je, hiyo ni haki?”
Kichwa cha Lisa kiligonga. Alikuwa amechanganyikiwa na maumivu. Hakuweza kuelewa ni nini Charity alikuwa akimaanisha, wala hakuelewa ni kwanini watu hao watatu walibadilika sana baada ya kusikia maneno yake.
“Toka nje.” Chester alipiga hatua kuelekea kwa Charity. Akamshika mikono na kumtoa nje. Alimkokota hadi kwenye geti na kumtupa nje.
Charity, ambaye alikuwa amevaa viatu virefu, aliangukia magoti. Nywele zake pia zilichafuka. Hata hivyo, alijikakamua na punde si punde akasimama. Hakuwa jeuri wala mnyenyekevu tena. Macho yake yalikuwa makavu na makali.
"Charity, ikiwa bado una matumaini kwa kampuni yako kupata nafasi Alivinarah, bora ufunge mdomo wako," Chester alimwonya kwa kumkodolea macho makali.
"Kwa kuwa mlikuwa na ujasiri wa kumleta Maurine hapa, kwa nini mnaogopa kumjulisha binti wa watu ukweli?" Uso uliopoa wa Charity ulizidiwa na ukaidi. “Nyinyi watu hamwezi hata kumsahau mwanamke ambaye amekufa kwa miaka mingi. Ni nini kizuri kuhusu Sarah? Yeye…”
Maneno yake yalimfanya aambulie makofi. Chester alishusha makofi kadhaa usoni kwa Charity. "Nyamaza."
Charity alijaribu kupepesa machozi. “Usijali. Sitamwambia Lisa kuhusu hilo. Ni mwanamke mzuri ambaye hastahili kuumizwa. Mtu mwenye matatizo kama Alvin hafanani naye.”
"Inaonekana kama hujajifunza somo lako." Chester akamshika tena na kumkaba koo. Hata baada ya kumuacha kwa miaka mingi, mwanamke huyo aliifanya damu yake kuchemsha.
“Nimekosea kusema hivyo?” Charity alijibu huku akinyong’onyea, “Licha ya kuwa ameoa, Alvin ameamua kumweka ndugu wa mpenzi wake wa zamani kama muuguzi wake. Anajaribu kumlaghai Lisa ambaye hajawahi kumuona Sarah kwa sababu yeye sio mwenyeji wa hapa, huh? Anahisi Lisa hatoshi? Kwa vile hawezi kumshinda Sarah, kwanini aliamua kumuoa Lisa? Ili kumdanganya? Nyinyi nyote ni wababaishaji.”
"Funga mdomo wako. Hujui lolote.” Chester alimvuta moja kwa moja na kumtupa kwenye dimbwi liliyokuwa kando yake. Maji ya baridi yalipofunika mwili wake mzima, karibu ashindwe kupumia.
"Tena ushukuru kwamba mimi ndiye niliyekutoa nje. Angekuwa Rodney au Alvin, matokeo ambayo ungekutana nayo sasa yangekuwa mabaya zaidi.” Chester alimtazama Charity ambaye alikuwa katika hali mbaya. Kisha, akageuka na kuondoka bila kuangalia nyuma.
Sura ya: 239
Kimya cha kutisha kilitawala baada ya Charity kuondoka. Ni sauti ya mkaa unaowaka tu ndio ilisikika katikati ya ukimya. Muda kidogo Alvin akachukua koti lake kisha akaweka mkono wake kiunoni mwa Lisa. “Sijisikii kula tena. Twende chumbani kwangu.”
“Nataka kurudi nyumbani,” Lisa alisema ghafla.
Rodney alikasirika sana. “Alvin, si uliahidi tutaenda kuvua samaki baharini kesho asubuhi? Unaweza kumwomba Hans ampeleke Lisa nyumbani. Ni mara chache sana sisi huwa huru kujumuika pamoja na kujiburudisha.”
“We baki na marafiki zako, Shani atanirudisha nyumbani.” Lisa alimsukuma Alvin na kuanza kuondoka.
"Sitabaki." Alvin alimfuata Lisa kwa hatua kubwa. Maurine naye alikusanya vitu vyake kwa haraka na kuwafuata pia.
Rodney alikasirika mpaka akapiga teke jiko la kuchomea nyama likaanguka chini.
•••
Wakiwa njiani kuelekea nyumbani, Hans aliwaendesha Lisa na Alvin waliokuwa wamekaa kwenye viti vya nyuma, pamoja na Maurine aliyekuwa ameketi kwenye siti ya abiria. Shani akaendsha peke yake gari la Lisa.
Baada ya muda, Maurine kwa uangalifu aliwapa Lisa na Alvin kipande cha keki. "Bwana Kimaro, Bibi Mdogo, chukueni kipande hiki cha keki ili kutuliza matumbo yenu kwani nyie hamkula chochote jioni hii."
Lisa alibaki kimya na kumtazama Maurine hadi uso wake ukahisi kupauka.
Akiwa amekunja uso, Alvin akanyoosha mkono wake kuchukua keki. Kisha, akaiweka mbele ya Lisa. “Itatuchukua angalau saa nyingine kufika nyumbani. Kula tu kidogo.”
"Hakuna haja. Sijisikii kula.” Lisa aliinamisha kichwa chini na kuchezea simu yake.
Safari nzima ilikuwa katika hali ya wasiwasi. Maurine aliposhuka kwenye gari baada ya kufika nyumbani, macho yake yalikuwa mekundu, alimwamngalia Lisa kwa huzuni na wasiwasi.
Lisa alimkazia macho na kumtazama. "Nini tatizo? Kwanini unainagalia kwa wasiwasi hivyo?”
“Bibi Mdogo…Samahani.”” Maurine alikuwa mwisho wa akili yake. Ilionekana kana kwamba machozi katika macho yake yangetiririka wakati wowote.
“Samahani kwa lipi?” Lisa alijitahidi kusafisha hisia za hasira usoni mwake. “Acha kuigiza kama umeudhika na kutishwa. Ndiyo maana unawafanya watu wengine wafikiri kwamba nakunyanyasa.”
Alvin akakunja sura na kujaribu kusema. “Lisa…”
“Ninasema tu kile kilicho moyoni mwangu.” Baada ya kuongea, Lisa aliingia ndani ya jumba mara moja.
Maurine aliuma mdomo. “Bwana Kimaro, mkeo haonekani kunipenda sana. Kwa kweli sijui la kufanya.”
"Nenda ukapumzike kwa sasa." Alvin alimwambia. Akageuka na kumfuata Lisa chumbani.
"Sasa kwa kuwa umeonyesha hasira yako, unajisikia vizuri?"
"Hapana.” Lisa aliinua kichwa chake na kuutazama uso mzuri wa Alvin ukiwa umekakamaa kwa hasira. “Nikisisitiza kuwa rafiki wa Charity, utanitaliki?”
"Acha upuuzi. Umechukulia kwa uzito maneno ya Charity.” Alvin aliuliza kwa kuchukizwa.
“Unaweza kujibu swali langu?” Lisa alimtazama kwa nguvu.
Alama ya kukosa subira ilitanda kwenye paji la uso la Alvin. “Sitakutaliki, lakini pia sitakuruhusu kuwa rafiki yake. Humjui Charity. Ni mwanamke mmbaya sana, hafai.”
“Ni mambo gani mabaya yasiyosameheka ambayo amefanya? Unaweza kunipa mfano?” Lisa aliuliza kwa shauku ya kutaka kujua.
Macho ya Alvin yalizidi kukolea hasira, akatazama pembeni asije kumkwaza Lisa. “Amefanya mambo mengi sana mabaya siku za nyuma. Ninakuonya kwa manufaa yako mwenyewe.”
“Ni mabaya gani hayo ambayo huwezi kuyataja? Alimuumiza mpenzi wako wa zamani?" Lisa alishindwa kujizuia kumtania Alvin.
Mwili wa Alvin ulisisimka. Aligeuka na kumtazama Lisa. “Acha kuwaza upuuzi, unasikia? Unataka tu uanze kubishana nami juu ya mwanamke ambaye hata humjui, huh? Kuna faida gani?”
“Ninabishana na wewe?” Lisa alivaa tabasamu licha ya kuwa na hali ya huzuni kali. "Ninakuuliza tu maswali ya kawaida, lakini wewe ndiye hutaki kujibu maswali yangu."
“Sipendi kubishana na wewe Lisa. Nina njaa. Nataka kula kitu.” Alvin alielekea mlangoni.
“Unaweza kujibu swali langu la mwisho? Ni kitu gani wewe na marafiki zako mnajaribu kunihadaa na kunidanganya?” Lisa alimtamkia kila neno kama alivyosikia kutoka kwa Charity, huku akimkazia macho.
Alvin alitazama nyuma tena na kuyakazia macho yake ambayo sasa yalikuwa yamejawa na hasira. “Ni lazima nirudie mara ngapi? Maneno ya Charity si ya kweli. Ni wazi kwamba anajaribu kututenganisha. Acha kuuliza maswali ya kipuuzi, la sivyo nitapoteza imani na wewe.”
Lisa alijihisi mnyonge mbele ya shutuma za Alvin. Hakuwa na maana ya kutilia shaka. Hata hivyo, hakusahau sura ya huruma aliyopewa na Charity baada ya kumwona Maurine. “Sawa. Tuache mabishano kuhusu Charity. Mwambie Maurine aondoke na utafute muuguzi mwingine, basi. Simpendi.”
Alvin alikunja uso wake kwa hasira na mshangao. “Umekuwa ukisema mengi na kuvuta uso mrefu usiku kucha kwa sababu tu humpendi Maurine na huna imani na mimi? Ulitakiwa kusema hivyo moja kwa moja kuliko kuanzisha madrama mengi. Kwanini uzungukezunguke?”
Lisa alishtuka. Ilikuwa ni muda tangu aliposikia maneno ya kijeuri kutoka kwake. Maneno hayo yalionekana kama kofi usoni mwake. “Ukiendelea kunifikiria hivi, hakuna ninachoweza kufanya. Hata hivyo, siwezi kukaa pamoja na Maurine hapa nyumbani.” Lisa alisema kwa uwazi, “Maurine sio muuguzi pekee hospitalini. Kuna wauguzi wengine pia."
“Smash!” Mlio wa glasi ikivunjika sakafuni ulisikika ghafla mlangoni.
Wote wawili waligeuza macho yao kuelekea upande huo, wakishangaa ni saa ngapi Maurine alikuwa amefika kwenye mlango wa chumba chao. Uso wake ulikuwa na wasiwasi, macho yake yalikuwa mekundu, aliyatumbulia macho maziwa yaliyomwagika pale chini na vipande vya glasi vilivyotawanyika sakafuni.
Muda mfupi baadaye, Maurine alitabasamu kwa uchungu huku machozi yakimtoka. "Bwana kimaro, kwa kuwa mke wako hanipendi, itabidi kutafuta muuguzi mwingine."
Alvin akakunja uso wake kwa hasira na hakusema chochote.
Maurine alishusha pumzi na kulazimisha tabasamu. “Huwezi kuharibu uhusiano wako na mke wako kwa sababu yangu. Naweza kuelewa hilo. Nimekuwa nikijaribu kuepuka hali ya aina hii, lakini Bi. Kimaro nahisi ananifikiria vibaya.”
Alvin aliinua kichwa chake. Sura ya kutisha ikatanda usoni mwake.
"Nitapakia na kuondoka sasa hivi." Akiwa ameduwaa, Maurine akainama ili kuokota vipande vya glasi, lakini kwa bahati mbaya alijikata kidole chake. Damu zilianza kuchuruzika sakafuni. Aliifuta damu kwa nguvu. Hata hivyo, kadri alivyozidi kuipangusa ndivyo damu inavyozidi kumwagika. Wakati huo huo machozi zaidi yalikuwa yakimwagika usoni mwake.
“Ni sawa. Viache tu, Shangazi Yasmine atasafisha baadaye.” Alvin alimvuta Maurine na kushuka naye kwenye ngazi.
Lisa alishuka pia kwenye ngazi, ambapo alimuona Alvin akipiga kelele sebuleni, “Anti Yasmine, kifaa cha huduma ya kwanza kiko wapi? Unaweza kumsaidia Maurine kufunga kidole chake?”
Shangazi Yasmine alifika kwa haraka na kumsaidia Maurine kufunga kidole chake kwa bandeji akisaidiwa na Alvin. Kulitazama tukio hilo mubashara, wasiwasi ulizidi kumjaa Lisa. Mtu kiburi kama Alvin angewezaje kuwa na wasiwasi na mgeni kama Maurine hata akamshika mkono? Je, Maurine alikuwa muuguzi tu?
Kwa bahati nzuri, maneno ya Charity yalimkumbusha. Kulikuwa na jambo linaloendela ambalo yeye hakulifahamu. Ikiwa Maurine angeendelea kukaa pale, Alvin angeweza kuishia kumjali zaidi. Lisa akahisi wivu ukimzidia kiasi cha kushindwa kuvumilia.....ITAENDELEA.....
Unafikiri nini kitafuata hapo, maana simulizi inazidi kuwa tamu kila siku lakini sina budi kuhitimisha kipande hiki ila niwasihi tukutane katika episode zijazo ili kujua nini kitafuata kwenye mkasa huu wa kusisimua na kuelimisha unaokwenda kwa jina la LISA.
