JINA LA SIMULIZI............................LISA
AUTHOR...........................JOMBA WAJO
SPONSORED BY......SIMULIZI ZA DULLY
WHATSAPP..........................0628924768
SEHEMU YA................................224-225
Sura ya: 224
Jioni, Alvin alikuwa bado hajarudi Lisa alipofika nyumbani. Shangazi Yasmini alikuwa tayari ametayarisha mboga. Lisa alitazama mboga kwenye ubao na kusema, “Hukukata nyama ya kutosha, na mboga pia hazitoshi.”
"Lakini hii tayari ni nyingi." Shangazi Yasmine alishangaa. "tukiongeza itakosa walaji na kuharibika..."
"Mimi nilikuwa nikimchomea kilo mbili za nyama, na Alvin anamaliza yote." Lisa akatoa nyama nyingine kutoka kwenye friji.
Shangazi Yasmine alikuwa na hamu ya kujua. "Je, hii inaweza kuwa nguvu ya upendo? Nimemuona Alvin akikua tangu akiwa mdogo. Hajawahi kuwa mlaji mzuri. Ni kana kwamba hapendi kula chochote na alishiba hata kama alikula sahani ndogo tu ya wali.”
Kusema kweli, kama Lisa asingekuwa na muda na Alvin jijini Nairobi, asingeweza kuamini maneno ya Aunty Yasmine. Alvin alikuwa akipenda sana mapishi ya Lisa walipokuwa Dar es Salaam. Ilikuwa tu ni vile kwamba Alvin hakuwahi kusema mawazo yake waziwazi kwamba mapishi yake yalimvutia. Kwa kuwa kulikuwa na mtu ambaye alipenda chakula alichotengeneza. Hilo lilimfanya Lisa awe na shauku zaidi ya kupika.
"Baadaye, utagundua jinsi Alvin alivyo mlaji mzuri." Lisa alianza kukata nyama ya nguruwe.
Kuandaa nyama ya nguruwe choma kulihitaji muda mwingi. Wakati anasubiri, alianza kupitia habari za mitandaoni kwenye simu yake.
Hata hivyo, alipoona habari iliyoshika hatamu kwenye mitandao kadhaa, Lisa alishikwa na bumbuwazi. Mtandao wa Niambie.co.ke ukaandika: [Bwana Alvin Kimaro Ni chizi. Aliwahi kuua Mtu Hapo Zamani.]
Mtandao wa Ghafla.co.ke ukaandika: [Rangi za Kweli za Tajiri mkubwa nchini Kenya; Bwana Alvin Kimaro ana historia ya ugonjwa mbaya wa akili. Alipelekwa katika hospitali ya magonjwa ya akili baada ya kujaribu kumuua yaya wake. Inatisha. Kuna picha kama ushahidi.]
Moyo wa Lisa ulitetemeka. Aligonga kwenye picha.
Kulikuwa na picha chache za kijana mdogo. Sifa na sura ya mvulana huyo ndivyo Alvin alivyoonekana alipokuwa mdogo. Picha moja ilimuonyesha akiwa ameshika kisu chenye damu mikononi mwake. Macho yake yalikuwa na mng'aro mkali, na uso wake mchanga ulionekana kukunjamana na kutisha. Kulikuwa na picha nyingine mbili. Moja alimwonyesha akikamatwa na polisi huku nyingine akiwa amevalia shati jeupe baada ya kulazwa katika hospitali ya magonjwa ya akili.
Maoni ya watu yakaanza kutiririka: [Nilisikia juu ya ugonjwa huu hapo awali. Katika mtaa wetu, kulikuwa na mgonjwa wa akili ambaye aliua mtu. Watu wa aina hii wanatisha kweli kweli.]
[Ee bwana wangu, hiyo inatisha sana. Hata alitaka kumuua yaya wake aliyemtunza? Huyu ni kichaa kamili! Mbona aliruhusiwa kutoka hospitali ya magonjwa ya akili? Je, ikiwa ataumiza mtu? Nilisikia ugonjwa huu unahitaji dawa za muda mrefu. Kama sivyo, utajirudia.]
[Nilisikia kwamba yeye ndiye mwanzilishi wa Alvinarah Company. Je, mtu mwenye ugonjwa kama huu bado anaweza kuendesha kampuni?]
Kulikuwa na maoni zaidi ya 10,000 mtandaoni. Kichwa cha Lisa kilikaribia kumlipuka. Alikumbuka tukio ambalo Alvin alimpiga na kumuumiza mara ya mwisho. Baada ya hapo, wakati mwingine alipomkasirisha, macho yake yalikuwa yanatisha sana. Kuna wakati mkono wake pia ulikuwa umeumia kwa njia ya ajabu.
Alifikiria jinsi Alvin alivyokuwa na hasira na mkali kila wakati, alijua ni tabia yake ya kawaida. Hakuwahi hata siku moja kufikiria kwamba angekuwa mgonjwa wa akili. Baada ya yote, alionekana kawaida sana.
Lisa alikimbia ghorofani na kugundua chupa chache za dawa kutoka kwenye droo kwenye meza yake ya maktaba. Alitafuta majina ya dawa hizo kwenye simu, na dawa mbili kati ya hizo zilikuwa za kutuliza hasira na dawa nyingine ni za kuzuia magonjwa ya akili.
Kwa hiyo habari hiyo ilikuwa ni kweli? Hapo awali alitaka kumuua yaya aliyemtunza, na sasa, alikuwa amemdhuru. Baadaye ingekuwaje? Akafikiria…Alihisi ubaridi ukishuka chini ya uti wa mgongo wake na hakuthubutu kushuka chini.
“Bibi Mdogo, Bwana Kimaro hajarudi. Unataka kumpigia simu?” Shangazi Yasmine alitokea mlangoni. Alipoziona dawa alizokuwa ameshika Lisa, sura yake ikasisimka. “Dawa hizi…”
“Shangazi Yasmine, ulisema umemwona Alvin akikua tangu mdogo. Kwa hiyo unapaswa kujua ... kwamba yeye ni mgonjwa wa akili, sivyo?" Uso wa Lisa ulikuwa umepauka, na midomo yake ilikuwa ikitetemeka.
Shangazi Yasmine alishindwa aseme nini. Aliifuta mikono yake kwenye apron yake na kuuliza. “Ulisikia wapi? Hili haliwezekani…
“Habari Ipo kwenye mtandao.” Lisa alimuonyesha picha hizo. “Shangazi Yasmine, yote haya ni kweli?”
Aunty Yasmine alishtuka baada ya kuziona zile picha. “Nani alichapisha mambo hayo? Hizi ni picha za siku nyingi sana… Bibi mdogo, lazima umwamini Bwana Kimaro. Ni mtu mzuri.”
"Lakini tabia yake ya kawaida kwa kweli ni mtu mkali mkali tu na ana hasira zilizokithiri. Dawa hizi pia ni uthibitisho wa hilo.” Lisa alishikilia chupa za dawa kwa nguvu na kunung'unika, "Shangazi Yasmine, mimi huwa namuogopa pia. Aliwahi kunipiga vibaya sana na kuniumiza hapo awali, na lilikuwa tukio la kutisha. Nataka tu kujua ukweli.”
“Sawa, nitakuambia. Natumai hutamuelewa vibaya kama watu wa nje.”
Shangazi Yasmine akashusha pumzi ndefu. “Bwana Kimaro alianza kuonyesha dalili za ugonjwa huu alipokuwa na umri wa miaka minane. Wakati huo, wazazi wake walikuwa tayari wameachana na mama yake hakumjali hata kidogo. Katika familia ya Kimaro, Mzee Kimaro alikuwa mtu busy aliyejikita tu kwenye kazi zake. Bibi Kimaro alimpenda Alvin, lakini alikuwa na watoto na wajukuu wengi. Alihitaji kujumuika nao pia, kwa hiyo hakuwa na wakati wa kumtunza. Hakuna mtu aliyegundua kwamba yaya wake alikuwa akimnyanyasa Alvin kwa sababu hawakumjali.”
“Kumnyanyasa?” Lisa alishtuka.
“Ndiyo. Wakati Alvin alipokuwa mdogo, alijihisi kutojiamini na kulia mara kwa mara. Bila shaka, hiyo ilikuwa mbinu tu ya mtoto ili kupata upendo wa wazazi wake. Lakini yaya wake alifikiri kwamba alikuwa akideka, hivyo mara nyingi alimfungia kwa siri ndani ya chumba na kumshindisha njaa. Wakati wa majira ya baridi kali, alimvua nguo zake na kumwacha akipigwa na baridi na njaa.”
Lisa alihisi kifua kinamuuma kwa uchungu. Alikuwa amepitia hisia hiyo ya baridi na njaa hapo awali, lakini Alvin alikuwa mtoto tu wakati huo. Mtu anawezaje kuwa mkatili kiasi hicho kwa mtoto?
“Alvin alilalamika kuhusu hilo hapo awali, lakini hakuwa ameumia sehemu yoyote mwilini. Kwa hiyo, kila mtu alifikiri alikuwa akimsingizia tu yaya kimakusudi.”
Aunty Yasmine aliendelea kusema, “Babake hakumjali pia. Alikuja amelewa kila siku. Kisha, Alvin alipokuwa na umri wa miaka minane, baba yake alienda ng'ambo na mwanamke mwingine. Alipotoka alikata mahusiano yote na Alvin na kumwambia asimtafute tena kwani kumwangalia kulimkumbusha siku za nyuma zisizo na furaha. Kuondoka kwake ndio lilikuwa jiwe la mwisho ambalo lilimponda Alvin…”
Lisa aliona vigumu kuongea. “Kwa hiyo…?!”
“Ndipo Alvin alipoingia kwenye mfadhaiko. Hakuzungumza wala kula. Hata alimchoma kisu yaya wake aliposhindwa kustahimili kunyanyaswa tena. Bibi Kimaro alipokagua kamera za ulinzi, tuligundua kuwa ni kweli yule yaya alimnyanyasa sana Alvin, lakini alikuwa amechelewa. Alvin alikuwa tayari kapelekwa hospitali ya wagonjwa wa akili ambapo alipata matibabu kwa miaka mitatu. Baada ya kurejea, alirejesha usikivu wa familia ya Kimaro kupitia bidii yake na kuwa hivi alivyo leo.”
Macho ya shangazi Yasmine yalikuwa mekundu. “Bibi mdogo, ni kawaida kumuogopa Bwana Kimaro. Lakini natumai hutamdharau wala kumuacha. Anatia huruma kweli. Akikupoteza, atapoteza kila kitu na hata tumaini la kuishi tena.”
“Sawa, sitathubutu.” Lisa akaitikia kwa kichwa. Moyo wake bado ulihisi dalili za maumivu.
Ni nani angeweza kufikiria kwamba mwanamume mwenye kiburi na mashuhuri kama yeye alikuwa akificha maisha ya utotoni yenye huzuni na maumivu? Ghafla alijisikia kumkumbatia kwa nguvu. Alitaka kumwambia kwamba angempa furaha ya familia ambayo alikuwa ameipoteza maisha yake yote.
Hata kama watu wengine wangemwogopa, yeye asingemugopa tena.
Alikumbuka kitu ghafla. Alihisi Alvin angejisikia vibaya baada ya kuona hizo picha. Alimpigia simu, lakini hakuna aliyepokea. Aliweza tu kumpata Hans kwenye simu. “Hans, Alvin yuko wapi? Niliona habari fulani kuhusu yeye. Yuko wapi sasa hivi?”
Sura ya: 225
“Bibi Mdogo, Bwana Kimaro…” Hans alisikika akiwa na wasiwasi, lakini hakujua aanzie wapi.
“Nimesikia kila kitu kutoka kwa Shangazi Yasmine. Sijali ugonjwa wake, we niambie tu alipo.” Lisa alijua anachofikiria.
“Baada ya Bwana Kimaro kuona habari hiyo, aliendesha gari peke yake. Hatujui alikokwenda na tunamtafuta kila mahali. Nadhani kuna kitu hakiko sawa na hisia zake. Ugonjwa wake unaweza kujirudia, na ninashuku kwamba ataenda kumtafuta Mama yake.
“Lea?”
“Ndiyo. Alipoona habari hiyo sasa hivi, nilimsikia akinong'ona kuwa hiyo lazima iwe kazi ya Lea. Kama Lea anahusika, atapoteza udhibiti wa hisia zake na ninahisi atamfanyia kitu kibaya." Hans alisema kwa wasiwasi, "niko njiani kumtafuta Lea sasa hivi."
“Nitumie anwani ya sehemu ulipo pia. Nitakupitia sasa hivi.” Lisa alichukua funguo ya gari na kutoka nje haraka.
•••
Katika jumba lake binafsi, Lea alipoona habari kuhusu ugonjwa wa akili wa Alvin kwenye mtandao, alimpigia simu Valerie mara moja. “Wewe ndiye uliyevujisha hizo picha?”
"Kwanini unanishuku mimi?" Valeria aliuliza kwa wasiwasi.
"Watu wa familia ya Kimaro pekee ndio wenye picha hizi. Kando na wewe, ni nani katika familia ya Kimaro…” Lea alikuwa bado hajamaliza kuzungumza wakati sauti za mapigano ziliposikika kutoka nje. Alifungua mlango na walinzi wote walikuwa wamelala chini. Alvin alisimama mlangoni akiwa na sura mbaya.
“Wewe…”
“Nifuate.” Alvin alimpiga mama yake kwa nguvu na kumvuta kuelekea juu ya paa. lilikuwa ni paa la flati la ghorofa. Simu yake ilidondoka chini. Sauti ya Valerie yenye wasiwasi ilitoka kwenye simu, lakini hakuna aliyejali kuhusu hilo.
Akiwa juu ya paa, Lea alionekana kufadhaika huku akiburutwa huku na kule. “Alvin, unajaribu kufanya nini…. Ah!” Nusu ya mwili wake ilisukumwa kutoka kwenye ukingo wa paa, akikaribia kuangushwa chini kutokea juu.
“Nilikuonya hapo awali usijaribu kutumia ugonjwa wangu wa zamani kunidhalilisha, lakini ulifanya nini? Kwanini nina mama kama wewe?" Alvin alimshika shingo kwa nguvu huku akipiga kelele. Alikuwa amevunjika moyo kabisa.
Lea alitoa macho kwa mshtuko huku uso wake ukiwa umekunjamana. “Siyo mimi…”
“Ni nani mwingine zaidi yako?” Macho ya Alvin yalikuwa yakiwaka kwa hasira. "Unajali tu kuhusu Jack tangu akiwa mtoto. Ulinizaa wa nini? Wakati huu wote, umekuwa ukimsaidia Jack kwa sababu ulitaka kunitoa kwenye nafasi yangu ya uenyekiti katika kampuni. Unanidharau tangu uliponizaa. Mimi sikujali hayo, lakini kwanini uliamua kueneza picha zangu? Nilikuambia kwamba nitakufanya ulipe kwa hili."
Tangu utotoni, Alvin hakuwahi kuhisi upendo wa kifamilia na uchangamfu kutoka kwa familia ya Kimaro. Sasa, hatimaye alipata tena mwanamke ambaye alimpenda, alitaka tu kuwa na maisha ya furaha, ya kawaida pamoja naye. Lakini, watu wa karibu wa familia yake walikuwa wametumia njia ya kikatili kufunua maisha yake ya aibu.
Mtandao ulikuwa umejaa maoni makali na mabaya kuhusu yeye. Kila mtu alimuogopa na hakuna aliyekuwa na hamu ya kumsogelea. Aliamini Lisa angeweza pia kuwa na hofu. Tayari alikuwa akimuogopa hapo awali. Joto na furaha yake iliyobaki ilikuwa imetoweka kama mapovu.
“Alvin, tulia. Mimi ni mama yako,” Lea alisema kwa sauti ya kutetemeka, “Unachofanya sasa ni kitendo cha jinai. Utatupwa jela utengwe na ulimwengu wote.”
“Ha! Kwani hivi sasa sijatengwa na kila mtu? Kwanini umenizaa? Wewe ndiye mwanamke mbaya zaidi ulimwenguni. Unanichukiza!” Alvin alipiga kelele kwa nguvu zake zote. Nusu ya mwili wa Lea ulining'inia hewani, na alikuwa karibu kuanguka.
“Utaniua kweli mwendawazimu wewe!” Lea alilalamika kwa hofu.
“Mimi ni mwendawazimu kweli, na wewe ndiye uliyenipeleka hadi kwenye ukichaa." Alvin alikasirishwa naye zaidi.
Alipokaribia kushindwa kudhibiti akili yake, alisikia kelele za Lisa nyuma yake. "Alvin, hapana!"
Mwili wa Alvin ulitetemeka, na uso wake mzuri ukabadilika kuwa wa kutisha zaidi. Hakuthubutu kugeuka na kumwangalia. Aliogopa kwamba angeona uso wake uliojaa hasira na ukatili. Alihisi kwamba ugonjwa wake ulikuwa mbaya zaidi kila mara tangu ulipojirudia. Kifua chake kilijawa na uadui. Hapo awali, angeweza kujizuia asimdhuru Lea. Lakini siku hiyo, hakuweza kujizuia tena. Hakutaka mtu yoyote kumsogelea kwa sababu hakuwa tayari kufungiwa tena katika hospitali ya watu wenye matatizo ya kiakili. Kulikuwa na pande nne tu za kuta huko. Hakuna mtu ambaye angemjali au kuwa na wasiwasi juu yake.
"Alvlisa, njoo hapa." Lisa alishusha pumzi na kumsogelea hatua kwa hatua.
“Imetosha, usisogee tena!” Alvin alimfokea kwa hasira. Uso wake mzuri ulijaa uchungu. "Mimi ni mgonjwa. Nitakuumiza. Unajua hilo?"
Lisa aliona upande huo wa Alvin uliojificha kwa miaka mingi. Moyo ulimuuma huku machozi yakimtoka. "Siogopi. Hakuna aliyezaliwa kuwa hivi. Huna hatia. Waliokudhulumu ni wale walio katika udhalimu.”
“Acha kuongea, sikuamini.” Alvin alitikisa kichwa bila kusita. "Mama yangu alinidanganya vivyo hivyo siku za nyuma, na alinipeleka kwenye hospitali ya magonjwa ya akili mara tu nilipogeuka."
Lea alidakia na kusema. “Kwa hali yako wakati huo, kama singekupeleka kwa matibabu—”
“Nyamaza!” Alvin alimkatisha ghafla. “Wewe ndiwe uliyesababisha ugonjwa wangu. Ulikuwa wapi nilipofungiwa chumbani kwa siku tatu mchana na usiku? Ulikuwa wapi nilipovuliwa nguo wakati wa baridi kali na karibu kufa kutokana na njaa na baridi?” Alizidi kuhamaki huku akiendelea kuongea, akawa anaelekea kushindwa kujizuia tena.
Lisa alishindwa kabisa afanye nini. Wakati huo Chester alikuja pembeni yake akiwa na sindano mkononi. “Ninaogopa kuwa wewe ndiye mtu pekee ambaye unaweza kumkaribia sasa. Mchome sindano hii mkononi na atazimia.”
"Lakini sijawahi kudunga sindano hapo awali ..." Lisa aliogopa.
"Unaweza kufanya hivi." Chester alimtazama bila kuyumbayumba na kumuelekeza. "Jitahidi. Usiruhusu Alvin kupita hatua ambayo tutashindwa kumrudisha."
"Sawa." Lisa akashusha pumzi ndefu na kuificha ile sindano kwa siri. Alimsogelea Alvin taratibu.
“Nilikuambia usije. Hunielewi?” Alvin aligundua kuwa Lisa alikuwa karibu naye na akamfokea.
"Siwezi kusimama karibu na kukuona ukiingia kwenye matatizo!" Lisa alizidi kumfokea Alvin kwa macho mekundu. “Alvin, huwezi kuwa mbinafsi kiasi hicho. Uso wangu uliharibika kwa sababu yako. Popote ninapoenda, watu hunidhihaki kwa kuwa na sura mbaya. Ulisema kwamba hutanionea aibu. Uliahidi kunipa furaha na kwamba ungetumia maisha yote kunithibitishia. Je! hivi ndivyo unavyothibitisha?”
Alvin aliutazama uso wake mdogo wenye michirizi ya machozi. Ghafla, alikuwa amepotea kama mtoto. “Mimi…”
“Bado huelewi? Siku zote nimekupenda. Bado nitakupenda haijalishi utakuwaje. Sitakuogopa kwa sababu ya maisha yako ya nyuma. Ni kinyume kabisa. Nitasikia maumivu tu kwa ajili yako, na ninataka kukupa joto kwa maisha yako yote. Wewe ni mgonjwa, na mimi ni mgonjwa pia, tutariwadhana. Hiyo ni sawa. Naweza kuwa kando yako. Ikiwa huwezi kupona, bado nitakuwa nawe maisha yote.”
Lisa akamsogelea hatua kwa hatua, na koo lake likamkaba. "Vivyo hivyo, ikiwa mimi ndiye mgonjwa, hutaniacha, sivyo?" Alvin alishikwa na mshangao, na macho yake makali yakaanza kupoa na ule moto wa hasira ukaanza kuzima taratibu.
Lisa alichukua nafasi hiyo na kumchoma mkono. Alvin akageuza kichwa chake na kumtazama. Hakuweka upinzani wowote, na macho yake polepole yakapoteza mwelekeo. Mkono wake uliomshika Lea ukalegea, akaanguka chini taratibu!......ITAENDELEA.....
Unafikiri nini kitafuata hapo, maana simulizi inazidi kuwa tamu kila siku lakini sina budi kuhitimisha kipande hiki ila niwasihi tukutane katika episode zijazo ili kujua nini kitafuata kwenye mkasa huu wa kusisimua na kuelimisha unaokwenda kwa jina la LISA
