JINA LA SIMULIZI............................LISA
AUTHOR...........................JOMBA WAJO
SPONSORED BY......SIMULIZI ZA DULLY
WHATSAPP..........................0628924768
SEHEMU YA................................222-223

Sura ya: 222

Lisa alishangaa sana. Maongezi yao yaliruka kutoka mada moja hadi nyingine haraka sana. Kama ingekuwa kipindi wako Dar es Salaam, Lisa angejibu kwamba anampenda bila kusita. Hata hivyo, kwa muda huo hakuwa na uhakika na hisia zake…
Kusita-sita kwake kuliufanya moyo wa Alvin kuzama. "Je! ni ngumu sana kwako kujibu swali hili?"
"Hubby, unapaswa kwenda kazini sasa." Lisa alimsukuma na kuanza kuondoka. Alvin alitazama jinsi anavyoondoka na macho yake yakawa na huzuni.
•••
Baada ya kufika kwenye kampuni, Alvin alifungua kompyuta na kuuliza kwenye Google swali hili kwa hasira:
[Kwanini mwanamke hamuonei wivu mume wake?]
Jibu 1: [Mwanamke huyu anajitegemea kihisia. Anajiamini na anajizuia kujionyesha hata kama anampenda sana mumewe.]
Jibu 2: [Mwanamke huyu ana moyo dhabiti. Ana imani thabiti na mume wake na ana uelewa kamili kwake.]
Jibu 3: [Hampendi vya kutosha.]
Cha kushangaza, jibu la tatu ndilo lililomkaa zaidi kichwani Alvin. Kwa hasira akaitupa huko laptop yake na kukivunjavunja kikombe cha kahawa alichokuwa amekishika palepale.
Hans aliyesikia mshindo huo akaingia na kumtazama kwa wasiwasi. Ni yeye pekee ndiye aliyeshuhudia jinsi hasira za Alvin zilivyozidi kuwa mbaya siku hadi siku. Hakuweza kuelewa. Alvin alikuwa akipendana na Lisa, lakini nini kilikuwa kikimkasirisha papo hapo? Hans alikuwa na wasiwasi. Ugonjwa wa Alvin ulionekana kuzidi kuwa mbaya zaidi.
Kwa upande mwingine, Lisa akiwa hospitali, alipokea simu kutoka kwa Pamela “Otea niko wapi?”
"Siwezi kuotea." Sauti ya Lisa haikuwa na furaha hata kidogo.
“Sawa. Nimefika nje ya ofisi za kampuni yako. Nilihisi utakuwa katika hali mbaya tangu baba yako alipopata ajali. Kama rafiki yako, nilinunua chakula kitamu na kukuletea hapa kukupa pole.” Pamela alicheka. “Siamini kwamba Alvin yuko makini kivile na kukumbuka kukuletea chakula. Hmph.”
Lisa alipigwa na butwaa kwa muda kisha akasema kwa haraka, “Usiingie ofisini. Geuka, ingia ndani ya gari na uondoke."
“Lisa, unamaanisha nini?” Pamela alishangaa kufuatia jibu la Lisa. “Nimepoteza muda wangu kuendesha gari kutoka mbali ili kuja kukufariji. Nilikwama hata kwenye msongamano wa magari kwa muda wa saa moja, na hivi ndivyo unavyonijibu?…”
Pamela alipokuwa akipandwa na hasira, mara aliona umbo la mtu aliyemfahamu likijongea kwake kwa hatua ndefu. Macho yake yakawa yamemtoka! Mtu huyo katika kumbukumbu zake ambaye alijaribu sana kumsahau ghafla alionekana mbele ya macho yake. Alihisi kukosa pumzi. Ni kana kwamba kuna kitu kilimlipuka ndani ya kichwa chake. Alikuwa na wasiwasi, fadhaa, na katika hali ya mfadhaiko.
“Pamela…” Patrick akaenda moja kwa moja mbele yake.
Pamela alikuwa bado katika hali ya mshangao. Baada ya kutengana na Patrick kwa miezi zaidi ya mitatu, hakutarajia kumuona mapema au baadaye, achilia mbali ndani ya jiji la Nairobi.
Pamela alikuwa kapendeza kiasi chake japo si sana. Alikuwa na nywele zilizojipinda zenye rangi ya asali zilizolegea. Alikuwa amevalia suruali ya jeans brand ya ‘cardigan’ nyekundu chini ya fulana ndefu nyeupe na jozi ya viatu vya ‘Dk. Martens’. Alikuwa amejipodoa kidogo lakini alivutia.
Hapo awali, Pamela angekonda kidogo kila walipotengana baada ya kuachana na Patrick. Lakini, kwa wakati huo alionekana kung'aa na kunawiri kana kwamba alikuwa amezaliwa upya. Kwa mara ya kwanza, Patrick alikuwa na hisia kwamba asingeweza kumpata tena.
Pamela aliduwaa mpaka akasahau kwamba simu ya Lisa ilikuwa hewani. “Sawa, inaonekana umeshakutana na Patrick.” Upande wa pili wa simu, Lisa alicheka kwa uchungu. “Alikuja na kunitafuta jana. Hebu kaeni chini mzungumzie tofauti zenu.”
",..sawa." Pamela akatulia taratibu. Aliinua kichwa na kumtazama mpenzi wake wa zamani.
“Pamela, kwanini hukuniambia kuwa unakuja Nairobi kufanya kazi?” Patrick alitabasamu kwa uchungu. “Ulizuia simu zangu zote na jumbe zangu za WhatsApp. Bado una hasira tu hata baada ya kunichunia kwa muda mrefu hivyo?”
“Kukuchunia?” Moyo wa Pamela ukaduwaa. Baada ya muda wote huo, bado alifikiri kwamba alikuwa akimpenda tu kama kawaida na kwamba yote yangepita mradi tu ambembeleze?

“Sawa, ninakubali kwamba nilikuwa na makosa wakati huo. Nimetafakari makosa yangu, naomba unisamehe. Tukirudi Dar, nitakutana na wazazi wako nyumbani kwenu ili kuwaomba msamaha. Tunaweza kufunga ndoa mara moja.” Patrick alimshika mkono.

Patrick alikiri kwamba hakuwahi kumthamini ipasavyo siku za nyuma na alimchukulia kawaida sana, akifikiri kwamba angebaki karibu naye siku zote. Kwa hivyo, aliishia kumpuuza sana. Aliapa asingefanya hivyo tena.
"Sitarudi nyuma." Pamela alibaki na msimamo wake. "Ninafanya kazi katika kampuni ya vipodozi ya Osher kwa sasa, na maendeleo yangu ya baadaye ya kazi ni mazuri hapa. Nilishasahau kero zako zote ulizokuwa ukinifanyia."
Patrick alishikwa na butwaa. "Kwa hiyo, kazi yako ya awali huko Dar es Salaam haikuenda vizuri?"
"Patrick Jackson, nilikaa Dar es Salaam kwa ajili yako tu, hata nikaghairi karibu mara tatu kuja kufanya kazi Nairobi nikisubiri ahadi yako ya kunioa. Lakini ulifanya nini? Uliniabisha mimi na wazazi wangu na kaka yangu pia kwa kutuweka mgahawani tukikusubiri masaa mawili, hukutokea wala kutoa taarifa, matokeo yake ukakimbilia kwa Linda. Nimeelewa kila kitu sasa. Bado mimi ni binti mdogo na mrembo, kwa hivyo ninataka kutembea na kujionea mengi ya ulimwengu huu. Sitaki kuolewa tena kwa sasa. Kwanini niingie kwenye kaburi la ndoa mapema hii?”
“Acha kujipoteza akili.” Patrick alimwambia kwa dharau. “Si wewe uliyekuwa ukililia kuolewa nami zamani?—”
Pamela akamkatisha. “Ilikuwa zamani, kwa hiyo ulidhani zamani ingebaki milele hata kama hukuithamini? Sitaki sasa. Patrick, nilishakuambia wazi kabisa tulipoachana mwaka jana. Tumemalizana. Sifanyi mzaha, usije kunitafuta tena.” Aligeuka ili kuondoka.
Patrick alipigwa na butwaa. Alimfuata na kumshika mkono. “Pamela, siamini. Tumekuwa pamoja kwa muda mrefu sana na tuliachana na kurudiana mara nyingi. Unawezaje kusema tu kwamba tumemalizana kirahisi rahisi hivi? Ninaapa, simpendi kabisa Linda—
“Basi unaweza kuniahidi kutowasiliana naye milele zaidi ya kwenda kwenye mazishi yake atakapokufa? Kama upo tayari mpigie simu sasa hivi na umwambie. Ninakupa nafasi ya mwisho.” Pamela alimkazia macho.
Patrick alikuwa haamini. “Tusiende mbali kiasi hicho. Kwa uchache zaidi, ninakuahidi kupunguza mahusiano yangu na Linda. Pia nitamwambia atafute mpenzi haraka iwezekanavyo—”
“Inatosha. Unasemaga hivi kila mara. Sitaki tena kusikiliza upuuzi wako.” Pamela alikasirika sana. "Kwanini unilazimishe?"
Patrick aliendelea kumshika na kukataa kumuachia. “Pamela, inatosha sasa. Unajua nimeacha kazi ngapi katika kampuni yangu kwa siku hizi mbili ili kukusubiri nje ya ofisi za Lisa?"
“Nyamaza kama hujui kuongea.” Pamela alikasirika baada ya kusikia maneno yake ya kijinga. “Unanibembeleza au unaniamrisha?”
“Hukuwa hivi hapo awali. Unapumbazwa na Lisa, huh? Kwanini huwa unamsikiliza? Alikuja Nairobi na wewe ukamfuata. Mwenzio sasa ameolewa, utaendelea kumfuata milele?” Patrick alifoka kwa jazba.
Pamela nusura afe kutokana na hasira. Ikiwa wasingekuwa hadharani, angevua viatu vyake na kumpiga navyo.
Kwa bahati mbaya au nzuri, Rodney alikuwa akitshuka kutoka ghorofani alipokwenda kwenye ofisi za Mawenzi kumtafuta Lisa akiwa na nia ya kumpendekezea vipodozi kadhaa kwa ajili ya uso wake ambavyo vilitengenezwa mahususi na kampuni yake. Alishangaa kumuona Pamela akibishana na mwanamume hadharani.
Tangu alipofokeana naye kwenye wodi ya Lisa kule hospitali, Rodney alikuwa na fikra kwamba Pamela hakuwa msichana aliyetulia. Sasa, hata alikuwa akirumbana na mwanamume mwingine hadharani, na ni wazi kwamba mwanamume huyo alikuwa mpenzi wake.
Alipokumbuka jinsi alivyomdhalilisha hapo awali, alipata hamu ya kulipiza kisasi. Alitaka kumharibia kabisa Pamela kwa mpenzi wake huyo. Alitabasamu kwa dharau na kuwasogelea kwa hatua ndefu. "Hey, babe, ni nani huyo?"

Sura ya: 223

Pamela akiwa katikati ya hasira yake alishtuka aliposikia sauti ya mwanaume aliyemfahamu. Aligeuka nyuma na kumwona Rodney, yule kijana wa kujionyesha, akimsogelea huku akimuwashia tabasamu la upendo.
“Babe, ni jana tu ulisema unanipenda mimi peke yangu, na leo nakufumania na jamaa mwingine. Unacheza na moyo wangu eti eeh?" Maneno ya utata ya Rodney yalikaribia kumfanya Pamela alowe na jasho mwili mzima.
“Huyu ni nani? Una uhusiano gani naye?" Uso mzuri wa Patrick ulitiwa giza baada ya kumuona yule jamaa ambaye alitokea ghafla.
Ikiwa Rodney asingekuwa bora kuliko Patrick katika kila nyanja, Pamela angehisi kufedheheshwa kidogo. Hata hivyo, Rodney alikuwa mzuri, mtanashati na mwenye mwonekano wa kitajiri zaidi kuliko Patrick. Mwili wake wote ulitoa haiba isiyozuilika, ya kutisha na kuvutia kwa wakati mmoja. Hakika hakuwa mtu wa kawaida.
Pamela akalegeza macho yake ghafla na kuachia tabasamu kana kwamba moyo wake umefunguka kwa Rodney. Alikutanisha kiganja chake cha mkono wa kulia na kiganja cha mkono wa kushoto wa Rodney na kusema, “Nilisahau kukuambia. Tayari nina mpenzi mpya, anaitwa Rodney.”
Mwili wa Rodney ukasisimka ghafla. Kwanini hali ilikuwa tofauti na alivyotarajia? Kwa hiyo walikuwa wameshaachana? Yeye alienda tu kuwachokoza ili waachane, lakini kwa kutokujua kumbe alikuwa akimsaidia Pamela badala yake.
“Haiwezekani.” Uso wa Patrick ulikunjamana kwa kutokuamini na kumpungia mkono Pamela. “Unatumia njia hii kunizuga? Pamela, nakubali kwamba unajua kuigiza. Twende nyumbani.”
“Unataka nikwambie mara ngapi kuwa sikutaki? Tulishaachana zamani.” Pamela aligeuza uso kwa Rodney kumuonyesha Patrick. “Angalia jinsi alivyo mzuri. Anaonekana kama Tony Montana wa kutoka kwenye muvi ya Scarface. Ana uwezo wa kutimiza ndoto yangu kwani ana sura nzuri, umbo maridadi, pesa na ushawishi. Patrick, ulimwengu wangu ulikuwa wewe tu hapo awali, kwa hivyo sikugundua mtu mwingine yeyote. Lakini baada ya kuja Nairobi, niligundua kuwa kuna watu wengine bora kuliko wewe. Hufai tena kuishi kwenye moyo wangu.”
Rodney hakujua kilichokuwa kikiendelea. Alivamia vita isiyomhusu na yeye akaishia kuwa mateka, mateka wa huba!
Ghafla akakumbuka kejeli zote ambazo Pamela alimtupia kule hospitali. Nii nani aliyesema kule hospitali kwamba alikuwa kipande cha takataka? Ni nani aliyesema kuwa yeye ni mrembo tu? Ni nani aliyesema kuwa hafanani na mwanaume?
“Unadhani kusema hivyo kutanifanya nikuamini?” Patrick akatikisa kichwa kwa huzuni. Hakutaka kuamini hata kidogo. “Bado una hasira na mimi na Linda. Unataka tu kunitia wivu…”
“Sisemi uwongo. Nampenda sana. Ngoja nikuthibitishie kama huniamini.” Bila neno lingine, Pamela aliikamata shingo ya Rodney na kuishusha chini. Kisha kukutanisha vichwa vyao, akapenyeza ulimi wake kwenye mdomo wa Rodney na kumpiga denda kwa nguvu.
Kadiri Rodney asiyejua lolote alivyozidi kupinga, ndivyo Pamela alivyozidi kumwongezea manjonjo. Alijisahau hata akanogewa kabisa. Rodney alibusuwa kwa lazima na mwanamke kwa mara ya kwanza katika maisha yake yote. Alitaka kumsukuma, lakini Pamela alimkandamiza kisogoni na kusema kwa sauti ambayo ni wao wawili tu ndio walikuwa wakisikia, “Si ulikataa kuwa wewe si mwanamke? Sasa ni wakati wa kuthibitisha hilo.”

Hiyo ilimaanisha kwamba asingeweza kujithibitisha kuwa mwanamume ikiwa angemsukuma Pamela. Rodney alikiri kwamba alikuwa amechanganyikiwa. Rodney alimkumbatia mgongoni na kurudisha busu lake kwa nguvu.
Patrick aliweza kuwatazama wawili hao akiwa hoi. Macho yake yalikuwa mekundu kutokana na mshtuko. Je, huo ulikuwa ni 'upendo' ambao alikuwa ameungama kwake siku za nyuma?
Alimtongoza kwa muda mrefu, lakini alipotaka sana kumtendea mema, alichagua kumuumiza hivyo.
“Pamela, nimekatishwa tamaa kabisa na wewe. Sitakutafuta tena.” Patrick alishindwa kuendelea kutazama tamthilia ile ya mahaba, akaondoka zake kwa hasira na kwa jazba.

Hakuona muda huohuo alipogeuka, tone la chozi lilidondoka kwenye jicho la Pamela. Matone ya machozi yakatua kwenye midomo ya Pamela na Rodney na Rodney akaonja kitu cha chumvi. Alipigwa na butwaa kwa muda, muda uliofuata akajikuta anasukumwa na Pamela.
Yule mwanamke aliyembusu hapo awali alikuwa akijifuta uso na mdomo kwa nguvu kana kwamba alikuwa ameramba kitu kichafu.
“Pamela Masanja…” Rodney alikasirika sana.
"Je, unahitaji tishu?" Pamela alichukua kipande cha tishu na kumpa. Macho yake mazito bado yalikuwa yakimeta kwa machozi, kama paka asiye na hatia.
Rodney alichukua kipande cha tishu kwa hasira na kuufuta mdomo wake kwa nguvu. “Mhh! Nahisi kichefuchefu hadi natamani kutapika!” Rodney akatema mate mfululizo.
“Nahisi hivyohivyo pia.” Pamela aliitikia kwa kichwa huku akifanya hivyohivyo. "Kumbusu mtu ambaye simpendi ni kinyaa sana."
Rodney alihisi kwamba kejeli yake ilikuwa ikipuuzwa, na moyo wake ulikuwa karibu na maumivu kutokana na hasira. “Unalia nini? Unajilazimisha kumuacha jamaa wakati bado unampenda, lhuku kwa ndani inakuuma. Je, huoni kwamba wewe ni mnafiki?”
“Hakika huna rafiki wa kike,” Pamela alicheka ghafla, “hukuwa na ujuzi katika busu hilo sasa hivi. Inawezekana kuwa busu lako la kwanza, sivyo?
“Bullsh*t...Ujuzi upi katika kujilazimisha kumbusu mwanamke nisiyempenda?” Rodney alikuwa na aibu sana kwamba Pamela alikuwa amemgundua ukweli. Hakuweza kujizuia kutema maneno machafu.
"Inaonekana nimepatia eeh?" Kuangalia sura yake ambayo ilikuwa karibu kulipuka kutokana na hasira, Pamela alipunguza jazba na kuongea kwa utulivu. “Si unajua kuwa wanawake wanapenda kujishaua? Wanaume wanaodharau mashauzi ya wanawake hawatapata wapenzi kamwe. Jifunze kitu.”
Rodney aliuma meno. "Pamela, nilikusaidia sasa hivi, kwa hiyo hivi ndivyo unavyonilipa fadhili zangu?”
“Nilikuomba unisaidie?” Pamela alimshushua. “Si ni wewe ndiye uliyekimbia hapa kwa hiari na kuniita 'babe'. Umesema hata mambo ya kutuchonganisha? Usifikiri kuwa nilikuwa sijui nia yako.” Pamela alicheka na kuondoka zake. Rodney alitoa sauti kubwa ya kusonya na kuondoka akionekana kuchukizwa.
Pamela akamuona Lisa ambaye alikuwa anakuja kwake. Lisa alisimama baada ya kumuona Rodney aliyekuwa nyuma ya Pamela. “Nyinyi wawili…” Lisa alikosa la kusema. Alipikicha macho yake kuona kama yalikuwa na ukungu uliomzuia kuona vizuri. Kwanini Rodney alionekana kuwa mpole sana wakati huo?
“Kwanini yuko hapa? Mmegombana tena? Patrick yuko wapi?” Maswali dabodabo yalimtoka Lisa.
"Patrick ameondoka. Tumeachana rasmi safari hii. Alisema hatanitafuta tena.” Pamela alitazama juu na kutabasamu, lakini macho yake yalikuwa na machozi.
"Usifikirie sana, ni hatua nzuri. Tunahitaji kuangalia mbele. Kuna wanaume wengi wazuri jijini Nairobi.” Lisa alimshika mkono na kuelekea ndani ya kampuni pamoja.
“Sijali. Nina huzuni leo. Inabidi unitowe usiku wa leo ukaniweke sawa.” Pamela alijidekeza.
“Siwezi kutoka usiku wa leo. Niliahidi kwenda nyumbani kumpikia Alvin.” Lisa akamkaribisha, akisema, “Kwanini usije kula nyumbani kwangu?”
“Usijali, sina hamu ya kuiona sura ya Alvin,” Pamela alisema kwa hasira, “Kwa kuwa sasa umeolewa, huna muda wa kutoka na mimi, ghafla najihisi mpweke sana.”
"Ndiyo sababu unapaswa kutafuta mpenzi wa kukuriwadha." Lisa akashusha pumzi ndefu na kusema. "Niangalie. Baada ya kuolewa, siwezi hata kwenda kula chakula na watu wa jinsia tofauti. Hata nikitoka na wasichana wenzangu, bado nahitaji kuripoti kwake. Nahitaji kurudi nyumbani mara baada ya kazi kwani Alvin atakuwa hana furaha nikichelewa kurudi nyumbani.”
"Kama ndo hivyo basi nadhani sitaweza kuolewa." Pamela aliingiwa na hofu baada ya kumsikiliza Lisa......ITAENDELEA....

Unafikiri nini kitafuata hapo, maana simulizi inazidi kuwa tamu kila siku lakini sina budi kuhitimisha kipande hiki ila niwasihi tukutane katika episode zijazo ili kujua nini kitafuata kwenye mkasa huu wa kusisimua na kuelimisha unaokwenda kwa jina la LISA