JINA LA SIMULIZI............................LISA
AUTHOR...........................JOMBA WAJO
SPONSORED BY......SIMULIZI ZA DULLY
WHATSAPP..........................0628924768
SEHEMU YA................................214-215

Sura ya: 214

“Lisa…” sauti ya upole ya Kelvin ilisikika ghafla masikioni mwake. Aliinua macho yake kutazama chanzo cha sauti hiyo. Alikuwa ni Kelvin Mushi. Alionekana kupendeza sana katika suti yake ya bluu. Macho yake yalitiririka kwa mshtuko na huruma alipomtazama. Akapiga hatua mbele na kuunyanyua mkono wake na kuubembeleza usoni mwake. Mkono mwingine ukamshika begani.

Alvin aliinuka na kumkumbatia Lisa karibu yake. "Kuna nini? Mbona unakosa adabu, yaani unamshika mke wangu hadharani mbele yangu?”

“Alvin Kimaro, wewe si yule uliyekuwa hapo awali, na ninakuhakikishia kuwa nitamchukua Lisa muda si mrefu. Hustahili kuwa naye.” Baada ya onyo hilo, alimgeukia Lisa na kusema kwa upole. “Nipe muda kidogo.”

“Kelvin, sikutarajia kukuona hapa leo.” Lisa, ambaye alikuwa amekwama katikati ya wanaume wale wawili, alijaribu kuongoza mada ya mazungumzo.

"Nimekuwa nikifanya kazi pamoja na Campos Ltd. hivi karibuni." Kelvin alisema, akimaanisha kuwa alikuwa mshirika wa Jerome Campos.

Sauti yake ilipopungua, katibu wa Jerome alikuja na kumsalimia kwa shauku, “Bwana Mushi, tumekuandalia kiti huko mbele. Ni watu wa hadhi ya chini tu ndio wanaopata viti vya nyuma.

"Ndio hivyo? Lakini huyu ni Alvin Kimaro..." Kelvin, ambaye kila mara alikuwa akimhofia Alvin, hatimaye akapata nafasi ya kumdhihaki.

“Alvin Kimaro ndiyo nani? Hastahili hata kukaa meza moja na Bwana Campos.” Sekretari wa Jerome alikoroma kabla ya kumuongoza Kelvin.

“Lisa unataka kujiunga na mimi?” Kelvin alimnyooshea mkono Lisa ghafla.

Kila mtu aligeuka na kuwatazama kwa ajabu. Wanawake walikuwa na wivu kuwa wanaume wawili wa sura zao walikuwa wakimgombania mwanamke aliyeharibika sura. Hali ya aibu ikamtanda Lisa.

“Kelvin Mushi, mara ngapi ninahitaji kukukumbusha kwamba yeye ni mke wangu?” Sura ya kupendeza ya Alvin sasa ilikuwa imekunjamana, na sauti yake ilisikika kwa vitisho.

“Unataka Lisa akae na wewe huku kwenye mkia wa ukumbi?” Kelvin aliuliza kwa upole ingawa macho yake yalionyesha nia ya dhihaka. “Hujamsikia katibu alivyosema? Ni watu wenye hadhi ya chini tu ndiyo wanastahili kukaa huku. Lisa ana hadhi ya juu kuliko wewe hivi sasa”

Kelvin hakujizuia kwa maneno yale ya kihuni. Wengine waliokaa meza hizo za nyuma hawakuthubutu hata kusema neno lolote kwani wengi wao walikuwa wamezamia tu na wengine hata kuhonga pesa ili kuingia kwenye sherehe hiyo ya uchumba ya kitajiri waweze kufahamiana na watu wengi zaidi kutoka familia zenye uwezo. Walishukuru kupata nafasi za kuketi ambazo wengine walisema ni za watu wa chini kama Alvin na Lisa.

Alvin alitabasamu.“Kelvin ulikerwa sana nilivyokudhalilisha kwenye sherehe ya kuzaliwa ya Mzee Ngosha mara ya mwisho kwa hiyo unalipiza kisasi?”

Kelvin aligoma kujibu. Hata hivyo, ni yeye pekee aliyefahamu jinsi alivyokuwa akifurahia wakati huo.

Alvin akalegeza midomo yake kwa tabasamu.“Unajionyesha kuwa ni mtu mstaarabu na mwenye adabu lakini inavyoonekana umejaa udhaifu mtupu na kutojiamini ndani yako. Kama mimi nipo wa hadhi ya chini, unawezaje kupambana na mtu ambaye tayari ameanguka?"

lilimshangaza sana Lisa. Alielewa kuwa Kelvin alikuwa anamchukia Alvin, lakini hakuwahi kumdhihaki hata siku moja. Lakini baada ya kusikia hivyo alimdharau sana Kelvin. Kweli Kelvin alionekana kuwa mtu tofauti siku hiyo. Hata aliuona unafiki uliomo ndani yake.

Alvin aligeuka na kumpigapiga Lisa kwenye uso wake. "Wanaume wengine ni wanafiki wazuri sana, tazama, mimi sijaribu kuficha kuwa ni mtu mbaya, tofauti na wengine wanaojionyesha kuwa watu wazuri lakini wana roho mbaya sana kwa ndani."

"Inatosha, Alvin Kimaro! Unadhani ninaweza kuzungumza nawe kwa utulivu baada ya kuiba mchumba wangu?" Kelvin aliripuka. Uso wake sasa ulikuwa umetanda kwa hasira. “Lisa njoo twende mama, nina uwezo wa kukuhudumia sasa hivi.”

“Pole, Kelvin, nadhani nitakaa hapa.” Lisa alimtazama huku uso wake ukiwa na huzuni, “Tafadhali nenda, siendani na wewe na sura yangu ya kutisha.”

“Umesikia hayo?” Alvin alimkumbatia Lisa kwa mahaba na kumwambia kwa upole, “keti mpenzi, tafadhari, nitaendelea kukunywesha wine taratibu.”

Kuna kitu kilipita machoni mwa Kelvin huku akimwangalia Lisa aliyekuwa ameegemeza kichwa chake kwenye kifua cha Alvin. Kelvin alizuia hasira zake za ndani na kugeuka ili kuondoka. Lisa alihema kwa ndani huku akiinua macho yake kumtazama akiondoka. Alitamani sana Kelvin aondoke haraka. Kwa kuwa alikuwa ameamua kurejea upande wa Alvin, alijua kwamba haiwezekani wawe pamoja tena.
Ilikuwa ni vigumu zaidi kwa kuwa bado alikuwa ameolewa na Alvin.

"Kula snacks zako na uache kuwafikiria wanaume wengine." Alvin alimgutusha ghafla kutoka kwenye fikra zake.

Lisa akageuza uso wake na kusema. “Kelvin huyu si kama yule niliyekuwa namjua…”

“Si kila mtu anaweza kuhudhuria sherehe hii ya uchumba. Yeye si mwenyeji wa Nairobi na hana watu wengi anaofahamiana nao hapa, hata hivyo alifanikiwa kufika hapa leo. Isitoshe amewekewa kiti kwenye meza nne za mbele. Unafikiri haya yote yametokea kwa bahati tu?” Alvin alimuuliza.

Lisa hakuwa na neno la kusema. Hakika, alihisi kama Kelvin alikuwa na mwenendo usio wa kawaida siku hiyo.


Baada ya sherehe. Familia ya Campos iliwaalika wageni wao kwenye bustani kwa ajili ya picha na burudani nyingine. Kundi la watu likaanza kutembea kuelekea mlangoni. Lisa alikuwa ananyanyuka tu pale alipohisi mtu akimpiga kwa nguvu. Mara, mwanamume mnene akageuza kichwa chake ili kumnyooshea kidole. "Kwanini unanigusa makalio yangu?!"

Lisa alimtambua mtu huyo papo hapo. Alikuwa ni Mkurugenzi Majuto ambaye alikuwa amejaribu kumsumbua kwenye chakula cha jioni cha hisani cha KIM International.

"Nini? Unathubutuje kumshika makalio mume wangu?! Mwanamke mwenye sura ya kutisha namna hii unataka kumtongoza mume wangu? Amini nikisema nitakupiga hadi ufe." Mwanamke mnene karibu na Mkurugenzi Majuto akasogea mbele haraka kwa nia ya kumpiga Lisa makofi,

"Bi Majuto, unataka kupoteza mkono?" Macho ya Alvin yalimtoka kwa hofu huku akishika mkono wa mwanamke huyo.

“Msaada, Bwana Kimaro anataka kunivunja mkono!” Bi Majuto alipiga kelele za kishindo ghafla.

Wageni waliokuwa wakielekea bustanini waligeuza vichwa vyao kuelekea chanzo cha zogo hilo. “Mkurugenzi Majuto na Bi Majuto, kuna nini?” Jerome akawasogelea huku akionekana kuwa na wasiwasi,

“Asante sana kwa kuwahi kufika hapa, nilikuwa napita tu pale mwanamke huyu aliponishika vibaya, mke wangu ana hasira na alipokuwa anamkaripia ghafla Bwana Kimaro alitishia kumvunja mkono mke wangu. ” Majuto alisema akifanya ana hasira.

"Haya, Lisa, haujaridhika kwamba Alvin si mwenyekiti tena wa KIM International, kwa hivyo unatarajia kutafuta bosi mwingine kwa nguvu?" Valeria aliziba mdomo wake kwa mkono ghafla.

"Unachukiza sana. Mwanamke usiye na haya!"

“Fanya haraka muombe msamaha Mkurugenzi Majuto na mkewe.” Wageni waliomzunguka wakaanza kumkemea Lisa.

Papo hapo, Bi Majuto alifumba macho ghafla na kuanza kulia kwa kwikwi. "Bwana Kimaro pia alivunja mkono wa mume wangu..."

"Tazama, mkono wangu bado unauma..." Mkurugenzi Majuto alizuga kukasirika.

Uso wa Mzee Kimaro ulikuwa umetanda hasira, “Unavuka kikomo, Alvin muombe msamaha Mkurugenzi Majuto haraka.”

Jack alipumua na kusema kwa majonzi. "Ndugu, Mkurugenzi Majuto ni mshirika muhimu wa biashara wa KIM International. Yeye pekee ana uwezo wa kununua tani milioni mia moja za simenti kwa mwaka. Umevuka mipaka kwa kweli wakati huu."

"Ndio hivyo?" Alvin alilegeza tie ya shingo huku akiwa na tabasamu lisilojali usoni mwake.“Basi Mkurugenzi Majuto nikuombeje msamaha ili unisamehe?”

Sura ya: 215

Mkurugenzi Majuto alikagua kwa macho yake eneo zima ili kuhakikisha hakuna mtu kutoka kwa familia ya Kimaro ambaye alikuwa na nia ya kumsaidia Alvin.
“Mimi si mtu asiye na akili. Kwa kuwa uliniumiza mkono wangu siku ile, basi leo nitarudisha kisasi kwa kukuvunja mkono wako. Isitoshe mke wangu amedhalilishwa na mkeo kwa kunishika makalio yangu. Lakini tunaweza kusawazisha hili ikiwa utamruhusu mke wangu kumpiga mke wako kofi usoni.”
Lisa alicheka baada ya kusikia hivyo. “Una uthibitisho kwamba ni kweli nilikushika makalio yako? Nina hakika kuna kamera za usalama kila mahali. Hebu tuangalie picha tuone kama kweli nilikuwekea mkono wangu...”
Mkurugenzi Majuto akaruka kwa hamaki. "Unamaanisha nini? Kwanini nimsingizie mwanamke mbaya kama wewe?"
"Mkurugenzi mashuhuri Majuto hawezi kukusingizia. Mambo yamefikia pabaya sana lakini bado unakataa kukiri kosa lako. Nadhani kofi moja usoni haitoshi hata kidogo.” Bwana Thompson alionekana kujaribu kufanya mambo kuwa mabaya zaidi.
Melanie alipendekeza zaidi, “Lisa, omba msamaha haraka kwa mwanamume huyo na umuahidi hutarudia tena.”
Lisa alitabasamu tu kwa kejeli na kusema, “Naona mmedhamiria haswa kwa kila njia kutudhalilisha sisi wawili siku ya leo. Ukweli hata haujalishi, kwanini tusichunguze kwanza kama ni kweli ndipo niombe msamaha?"
"Hatuna muda wa kupoteza, Bi Jones, mtu mzima na hadhi yake kama Mkurugenzi Majuto hawezi kamwe kukusingizia uwongo." Jerome alisema kwa sauti ya chini. "Hata hivyo, mtu anapaswa kuvuna matokeo ya matendo yake. Unasemaje, Bwana Alvin Kimaro?"
Kila mtu akahamishia macho yake kwenye sura ya Alvin iliyokuwa imefura kwa hasira. Si muda mrefu uliopita, mtu huyu alikuwa juu ya uongozi. Sasa akiwa ameanguka kutoka juu, kila mtu alishindwa kujizuia kutaka kumuona akiteseka.
Chini ya macho ya umma, macho ya Alvin yaligeuka kuwatazama watu wa familia ya Kimaro. “Babu, Bibi, Mama, mnakubali pendekezo lao? Mko tayari kweli Mkurugenzi Majuto anivunje mkono na kumchapa kibao cha uso mke wangu?” Kwa maoni ya wanafamilia, alikuwa akitafuta msaada.
Bibi Kimaro alitingisha midomo yake. “Nafikiri—”
“Nadhani ni wakati wa nyie wawili kupata adhabu,” Mzee Kimaro alimshika mke wake kwa bega huku akimkatiza. "Tulishindwa kukuelimisha, lakini kwa bahati mbaya tukakugeuza kuwa mtu mwenye kiburi na dhalimu."
Valeria alikuwa akitabasamu kutoka sikio hadi sikio. “Alvin, naamini hukuliona hili likija. Hivi umesahau jinsi ulivyonifanyia mara ya mwisho? Lakini sasa unaona umuhimu wetu? Endelea kuota."
"Mama, unaonaje?" Alvin alimkazia macho Lea. Mwanamke yule akakwepesha macho yake.
Alvin akainamisha macho yake kwa masikitiko. Lisa hakuweza kujizuia kumuonea huruma mwanaume wake, akamshika mkono wake kwa nguvu. Alielewa uchungu wa kuachwa na familia yake mwenyewe. Alitazama juu ya bega lake kukutana na macho yake.
Mkurugenzi Majuto akafurahi sana kusikia familia nzima ya Kimaro ilimuunga mkono. “Umesikia hivyo? Nyoosha mkono wako sasa hivi. Hmm, nadhani tunapaswa kwenda na mkono wako wa kulia."
Alvin alipoinua kichwa chake tena kutazama chumba chote, midomo yake maridadi ilijikunja na kuwa tabasamu hafifu. "Kwa kweli, ghafla nilikumbuka kitu. Kwa kuwa karibu familia zote tajiri za Nairobi ziko hapa leo, naomba mniruhusu nijitambulishe tena.”
Alichukua kadi ya jina la dhahabu kutoka mfukoni mwake na kuionyesha huku akiongea kwa madaha. "Mimi ndiye mwanzilishi, mkurugenzi, na mwenyekiti wa kampuni ya Alvinarah, Alvinarah Corporation…”

Kila mtu aliifahamu kampuni hiyo, lakini hawakumjua mmiliki wake hadi alipojitambulisha. Ilikuwa ni kampuni kubwa, haswa ikiwa imejikita katika kuzalisha na kusambaza vifaa vya ujenzi katika nchi za Kenya, Uganda Somalia na Sudani Kusini. Ilikuwa na sehemu ndogo ya soko lake nchi Tanzania pia. Ingawa ilianzishwa chini ya miaka mitano iliyopita, kampuni hiyo ilikuwa imekua kwa kiasi kikubwa. Huko Kenya, sasa ilikuwa kampuni ya pili katika kuzalisha vifaa vya ujenzi baada ya KIM International. Anvinarah pia ilimiliki kundi la vyombo kadhaa vya habari nchini Kenya na Tanzania kwa mwavuli wa Alinarah Media Network ama kwa kifupi AMEN Group.
Wanafamilia ya Kimaro, haswa, walikuwa wakimtazama Alvin kwa macho ya kutokuamini. "Nini? Wewe ndiye mwanzilishi wa Kampuni ya Alvinarah?" Mzee Kimaro alikasirika.
"Alvin, unawaza nini?" Lea aliona ni vigumu kuamini pia. "Wewe ulikuwa mwenyekiti wa KIM International lakini ulikuwa unajenga kampuni ya Alvinarah kwa siri pia? Unawezaje kusaliti familia ya Kimaro?!"
"Mwanaharamu wewe, kosa langu kubwa maishani ni kukuruhusu uchukue KIM International!" Mzee Kimaro alitamani angeweza kushusha nyundo kwenye kichwa cha mjukuu wake muda huo.
“Baba usiwe na wazimu. Sio jambo kubwa. Kampuni ndogo kama Alvinarah haiwezi kushindana na biashara ya familia yetu,” Valeria alisema kwa huzuni.
"Hiyo ni sawa. Kimaro Cement ndio chapa bora zaidi ya simenti Afrika Mashariki. Kampuni ya Alvinarah ni takataka ukilinganisha na sisi,” Queenie aliunga mkono huku akitabasamu.
Vipengele vya wasiwasi kwenye uso wa Mzee Kimaro hatimaye vilipungua kidogo. “Alvin, wewe si sehemu ya familia ya Kimaro kuanzia leo. KIM International itafanya kila kitu kuifilisi Alvinarah. Jack, nakuamuru uiharibu kampuni ya Alvinarah katika muda wa miezi mitatu na itoweke kabisa Kenya.”
"Babu, nitafanya." Jack alijaribu kuzuia wasiwasi wake.
Alvin alitabasamu baada ya kuona sura zao zikitapatapa. “Jack, hujawaambia kuwa timu ya uhandisi ya Simon Mbugui iliyokuwa KIM International imejiuzulu? Sawa, nilisahau kutaja kwamba Timu ya Simon tayari imejiunga na Alvinarah. Tunafanya mkutano wa kimataifa ili kutangaza kutolewa kwa brand mpya ya Oceanic Cement saa 11:00 asubuhi Ijumaa ijayo.”
Kila mtu hakuamini masikio yake. KIM International ndiyo ilitakiwa kutangaza kuachiwa kwa brand mpya ya Oceanic Cement. Sasa iliangukiaje mikononi mwa Alvinarah?
Jack alicheka kwa kejeli. “Alvin, bado unaota? KIM International ilitumia miaka mitatu kufanya kazi na timu ya uhandisi ya Simon Mbugui kuvumbua Oceanic Cement. Kwanini Simon ajiunge Alvinarah na data zote muhimu? Kwa hakika ninaweza kurejesha umiliki wa uvumbuzi huo. Wakati huo huo, nitawashtaki pia Simon na Alvinarah kwa wizi wa hatimiliki.”
“Jack, wewe ni kituko sana, na sijui utawezaje kuiongoza KIM International kwa akili za matope kama hizi” Alvin alijibu huku akitabasamu, “Umewahi kusoma mkataba wa kazi wa Simon? Tangu mwanzo, hajawahi kusaini mkataba na KIM International bali alisaini na mimi binafsi. Mtaji wote uliowekezwa katika maendeleo ya mradi huo wa Oceanic Cement pia ulitoka kwangu peke yangu. Nyaraka zote za hakimiliki zimeandikwa kwa jina langu, si la kampuni. Kwa hali hiyo una haki gani kumshtaki Simon?”
Hakika chezea mtu mwingine lakini si mwanasheria, hasa mwanasheria mwenyewe akiwa ni msomi na mahiri kama Alvin. Jack aliufyata mkia, Alvin akazidi kutamba.
"Kinyume chake ..." Alvin alikaza macho yake. "Mimi na Simon tuna haki ya kurejesha umiliki wa bidhaa zote tulizozivumbua tukiwa na KIM International hapo awali. Jack, kaa tu na usubiri barua yangu ya kisheria.”
Rangi zote zilitoka kwenye uso wa kila mtu wa familia ya Kimaro waliposikia hivyo. Uso wa Jack ulikuwa umepauka kama karatasi huku Mzee Kimaro akitetemeka kwa hasira.
"Alvin, utalaaniwa kwa kifo kibaya!" Mzee Kimaro alimnyooshea mjukuu wake kwa kidole kinachotetemeka. "Familia ya Kimaro ilikulea miaka hii yote na hivi ndivyo unavyotulipa?"
“Alvin, huwezi kufanya hivyo. Uamuzi wako utatuharibia.” Moyo wa Bibi Kimaro ulikuwa kwenye maumivu makali sana.

“Babu, Bibi, nimewapa nafasi. Dakika chache zilizopita, niliuliza kuhusu maoni yenu lakini nyote mlinidhalilisha zaidi. Je, kuna mtu yeyote kutoka kwa familia ya Kimaro aliyenionyesha heshima yoyote?” Uso wa Alvin ulikuwa umetulia kama maji. Lisa pekee ndiye aliyejua jinsi mkono wake ulivyokuwa ukitetemeka. Mwanamume huyo hakukata tamaa tu bali alikasirika.
“Jack amechangia nini kwenye KIM International?” Alvin aliendelea. “Kampuni zingine zote chini ya KIM International hazijafanya vizuri katika miaka ya hivi karibuni. Ni mimi niliyeleta Kimaro Cement kwenye nafasi yake ya juu ili kuwa biashara yenye faida zaidi ya kampuni. Nilianzisha kampuni ya Alvinarah kama njia ya kupunguza ushindani wa nje. Ikiwa ningefanikiwa kurithi hisa kwa KIM International, bila shaka ningeunganisha makampuni yote mawili kuwa kampuni moja kubwa sana. Lakini, kwa kuwa familia imekata tamaa juu yangu, basi nitaendelea kuiongoza Alvinarah kama mpinazani wa KIM International.”
Hakujaribu kuficha dhamira na tamaa machoni pake. "Siwezi kamwe kujitolea kwa ajili ya wengine bila kupata manufaa yoyote."
"Kuiangusha KIM International? Unaweza kuendelea na ndoto yako nzuri!” Jack alimfokea kwa sauti kubwa.
“Tusubiri tuone basi. Lakini utawaelezaje washirika wakati huwezi kukabidhi mradi wa uzinduzi wa chapa mpya ya Cement kama ulivyoahidi?" Alvin alihoji kabla ya kuelekeza macho yake kwa Mkurugenzi Majuto na Bwana Thompson. “Na nyie mabosi, mmoja wenu ni mkandarasi wa barabara huku mwingine ni mkandarasi wa majengo. Ikiwa hamtoweza kupata Cement yenye teknolojia mpya na ya kipekee kama Oceanic Cement, ni suala la muda tu kabla hamjatupwa na kampuni zingine kwenye sekta yenu.”.....ITAENDELEA....

Unafikiri nini kitafuata hapo maana mambo ni moto mambo ni fire, lakini sina cha kusema nikuombe tuungane pamoja katika sehemu inayofuata ya mkasa huu wa kusisimua unaokwenda kwa jina la LISA.