JINA LA SIMULIZI............................LISA
AUTHOR...........................JOMBA WAJO
SPONSORED BY......SIMULIZI ZA DULLY
WHATSAPP...........................0628924768
SEHEMU YA................................159-160

Sura ya: 159

Baada ya kuondoka kwenye makazi ya Alvin, alikwenda moja kwa moja kwenye tawi la Mawenzi Investiments huko Nairobi, Barabara ya Moi. Ilichukua siku moja kwake kuelewa hali ya hapo. Maendeleo ya Mawenzi katika maeneo mengine yalikuwa mazuri, lakini hayakuwa mazuri katika mji mkuu, Nairobi.

"Ardhi ya Nairobi ni ghali sana na ni vigumu kuipata," meneja mkuu alimweleza. "Ingawa tuna pesa za kutosha, ni ngumu sana kupata ardhi bila kujuana na watu wazito katika jiji hili. Kuna familia nyingi sana zenye ushawishi hapa ambazo zinajihusisha na umiliki wa ardhi.

Lisa aliitikia kwa kichwa. "Itabidi tujaribu tuwezavyo kutafuta shamba zuri ili tuweze kupata eneo thabiti hapa Nairobi."

"Kuna shamba katika ukanda wa mashariki ambako mji mkuu unaendelezwa. Ni vizuri sana tukipata ardhi kwenye eneo hilo.” Meneja aliifunua ramani na kumuonyesha.

Lisa alikariri eneo hilo na kumuuliza Joel baadaye usiku kama alikuwa na wazo lolote. Baada ya yote, kwa kuwa sasa alikuwa na baba hapo Nairobi, angekuwa mjinga kufanya mambo peke yake bila kumwomba msaada.

Joel alitabasamu na kusema, “Hilo ni jambo dogo. Nitazungumza na idara husika kesho.”

Joel alipanga kumpeleka Lisa kwenye makazi ya ukoo wa Ngosha kwenda kuwasalimia Babu na Bibi yake. Ukoo ya Ngosha ulilowea huko Kenya miaka mingi baada ya kuhamia ikitokea Mwanza kwa hiyo Baba na mama yake Joel Ngosha waliishi huko. Joel Ngosha mwenyewe amekuwa kirudi Tanzania mara kwa mara kwa ajili ya biashara zake.

Lisa akampa baba yake zawadi aliyoiandaa. Alikuwa amemnululia suti. “Nilikununulia siku moja nilipoenda dukani na rafiki yangu. Ilinivutia nikaona nikununulie, na nadhani kitambaa chake ni kizuri pia."

“Binti yangu ana jicho zuri. Imenikaa vizuri. Nitaivaa kesho wakati wa safari.” Joel alitabasamu kutoka sikio hadi sikio.

“Pia nilinunua seti mbili kwa ajili ya Babu na Bibi, lakini sijui kama wangeweza—”

“Usihofu, hawatajali sana, zawadi ni zawadi tu. Cha msingi ni kwamba unawafikiria ndiyo maana umeweza kuwakumbuka kwa zawadi” Joel alisema huku akitabasamu.

Makazi ya zamani ya Ngosha pia yalikuwa karibu na Mlima wa Sherman. Wawili hao hawakubadilishana maneno njiani wakati wa kwenda huko. Wakati wanakaribia kufika kwenye makazi, sauti ya helikopta ilisikika. Lisa alichungulia dirishani kutazama, na hatimaye Joel akapata mada ya kuzungumza na binti yake.

"Matajiri wengi hapa katika mji mkuu wana helikopta zao binafsi. Ile sasa hivi inapaswa kuwa ya familia ya Shangwe."

"Rodney Shangwe?" Lisa aliuliza kwa mshangao. Kwa kweli hakumpenda jamaa huyo hata kidogo. Kwa Alvin kuwa na urafiki na mtu kama huyo, ni lazima walikuwa wakifanana kwa tabia.

"Unamjua Rodney Shangwe?" Joel alicheka. “Rodney ana uhusiano mzuri na Alvin, na helikopta walizonunua ni za aina moja ila rangi tofauti. Lakini, Alvin hapendi sana kutumia helkopta, huitumia kwa dharura sana. Nilisikia kwamba juzijuzi aliruka ghafla usiku wa manane. Kila mtu alisema kwamba kuna jambo la dharura lazima liwe limetokea katika familia ya Kimaro.”

Moyo wa Lisa uliganda. Ghafla alikumbuka wakati alipokuwa amelewa kwenye Yatch. Alihisi kama alikuwa kwenye helikopta, lakini alifikiri tu alikuwa akiota. "Baba, ilikuwa siku gani?"

“Aahm..Sina uhakika sana. Pengine ilikuwa Jumanne au Jumatano.” Joel alishangaa kwa Lisa kuuliza. “Kwanini unauliza siku?”

"Si chochote, nilikuwa na hamu tu ya kujua maana hata mimi nilisikia ikiunguruma nikiwa usingizini." Lisa alihisi kuchanganyikiwa. Jumatano ilikuwa ndiyo siku ambayo alifanyiwa tukio lile na Rodney. Ina maana Alvin alienda kwa helikopta kumchukua? Lakini kwanini alienda kwa haraka hivyo? Je! ni kwa sababu alitaka kumuona akijifanya ujinga, au alikuwa na wasiwasi naye ndiyo maana akawahi ili kumuokoa? Hakuwa na jibu sahihi la swali lake.

Lisa alishtuka baada ya wazo hilo kumtoka. Hilo lilikuwa haliwezekani. Angewezaje kuwa mkarimu hivyo? Alitaka kumdhalilisha zaidi ya Rodney.

Dakika 20 baadaye, waliingia kwenye makazi ya mzee Ngosha.
Kulikuwa na watu zaidi ya kumi waliokuwa ndani ya jumba la makazi ya ukoo huo, akiwemo Nina na bintiye. Kila mtu alikuwa akipiga soga na kucheka, lakini wote walielekeza macho yao kwake walipomuona akiingia.

Lisa akatazama kwa haraka macho ya kila mtu. Wote walikuwa wakimtazama kwa dharau na shauku. Ilionekana kana kwamba hawakumpenda sana.

Hatimaye, macho yake yalitua juu ya wale wazee wawili, babu na bibi yake. Bibi mzee alimtazama kwa sura laini, lakini bwana mzee alionekana kutojali.

“Baba, mama, kama nilivyokuambia, huyu ni Lisa. Ni binti wa Sheryl niliyezaa naye.” Joel alimtambulisha kwa wale wazee wawili.

Bibi Ngosha aliitikia kwa tabasamu. “Anaonekana mrembo. Kaa chini. Nilimsikia Joel akiongea kuhusu wewe hapo awali na nikaagiza vito vya thamani kwa ajili yako kama zawadi ya kuonana.”

Mjakazi alileta sanduku dogo la mbao. Lisa alisita kupokea lakini alikubali baada ya Joel kuitikia kwa kichwa. Akalifungua na kuchungulia ndani. Kweli kama alivyosema Bibi Ngosha, kulikuwa na mapambo yaliyotengenezwa na vito mbalimbali, na mtindo wake ulikuwa wa kizamani, lakini ulionekana kuwa ghali kabisa.

“Asante bibi. Nimevipenda sana.” Lisa alisema kwa furaha, “nitavithamini na kuvitunza sana.”

"Ni vizuri ikiwa umevipenda." Bibi Ngosha aliridhika. Ingawa hakuwa na mapenzi sana na mjukuu huyu, Lisa bado alikuwa binti wa mtoto wake. Siku zote hakufurahi kwa sababu Joel hakumpa wajukuu zaidi.

Wakati huo, Melanie aliinama na kutazama kabla ya kusema, “Bibi, na mimi nataka pia zawadi.”

Shangazi yake ambaye alikuwa amesimama kando alimtania, akisema, “Melanie, wewe sasa ni mpenzi wa Bwana Kimaro. Kwa nini bado unataka zawadi za thamani ya chini kutoka kwa bibi yako? Nilisikia kwa Kimaro kuna mapambo yenye vito vya gharama sana, unaweza kwenda kuzawadiwa zaidi ya hivi."

Melanie aliona aibu kidogo. Aliishia kula chakula na Alvin mara moja au mbili tu na hakutoka naye tena, lakini kila mtu alijua kuwa alikuwa ni mpenzi wake, kwa hivyo hakuweza kujiaibisha. "Bwana Kimaro alisema kwamba ningeweza kuchukua chochote ninachotaka, lakini ... bado hatujaoana, kwa hivyo sitajisikia vizuri kwenda kudai zawadi kabla ya ndoa.”

Mzee Ngosha aliitikia kwa kichwa kuridhika. "Hayo ni mawazo mazuri. Bwana Kimaro anatafuta mke kutoka kwa familia nzuri. Familia yetu ya Ngosha haina shida ya pesa wala vito, kwa hiyo msiwe kama wale wanawake duni ambao kazi yao ni kujikombakomba kwa matajiri.”

“Hiyo ni kweli, wewe si mtoto wa haramu hata hivyo, huhitaji kubemelezwa kwa vito vya thamani ili usijikie ni wa familia ya Ngosha." Shangazi alimpa Lisa jicho la pembeni lililojaa dhihaka. Umati ulicheka kwa dharau, na Joel mara moja akaonyesha kutofurahishwa kwake. Alikuwa karibu kuwakemea.

Hapohapo, Lisa alitabasamu na kusema, “Ndiyo, nimefurahi sana kupokea vito vya thamani kutoka kwa bibi yangu, lakini si kwa sababu ni vya gharama, ni kwa sababu nimepewa na Bibi. Ningeweza kuthamini chochote ambacho bibi angenipa hata kama ingekuwa ni kibuyu cha asali tu!” Lisa alinyamaza kidogo, na macho yake mazuri yenye majimaji ghafla yakawa mekundu.

"Nikiwa njiani kuja hapa, nilikuwa na wasiwasi. Mimi ni tofauti na Melanie na nililelewa na babu na bibi yangu upande wa mama tangu utotoni. Melanie ni mchangamfu na anapendeza, lakini hajui jinsi ya kuishi na wengine. Nililelewa na shangazi na mjomba wangu, na hakuna mtu aliyenifundisha jinsi ya kuishi pamoja na familia yangu. Niliogopa kwamba Bibi na Babu wasingenipenda, lakini kwa bahati nzuri… Kwa bahati nzuri, zawadi hii kutoka kwa Bibi imejulisha kwamba bado ana mimi moyoni mwake.” Alimtazama Bibi Ngosha alipomaliza kuongea huku akihisi kuguswa.

Mwanzoni, Bibi Ngosha alifurahi tu kwamba mwanawe alikuwa na binti wa ziada, lakini baada ya kusikia maneno ya Lisa, ghafla moyo wake ulimuuma kwa mjukuu huyo. Yeye pia alikuwa na aibu kidogo. Alikuwa amechagua tu vito hivyo bila mpangilio, lakini mjukuu wake alivipenda kwa moyo hadi akatokwa na machozi.

Bibi Ngosha akazidi kuomba msamaha na kumpungia Lisa mkono kwa haraka ili asogee kwake. “Njoo ukae kando ya Bibi. Wewe ni mjukuu wa familia ya Ngosha, lakini utakuwa umeteseka sana. Nilisikia mjomba na shangazi yako hawakukutendea vizuri, sivyo?”

“Hapo awali walikuwa wazuri kwangu, lakini baada ya kumrejeshea binti yao wenyewe, hawakunijali tena. Walinifungia hata kwenye jumba lenye ukiwa la ukoo na kunilazimisha kula chakula kibichi na kunywa maji machafu,” Lisa alisema huku machozi yakimtoka.

"Nilisikia kwamba familia ya Masawe iilikutendea vizuri. Unasema uwongo, sivyo?” Melanie alimuona Bibi Ngosha akimbembeleza Lisa mkono na akashindwa kuvumilia tena.

“Ndiyo hivyo,” shangazi yake naye akajibu mara moja. "Mjomba na shangazi yako walikulea tangu mtoto, kwa hivyo unawezaje kusema maneno kama haya?"

'Ni sawa kama huniamini. Unaweza kwenda kufuatilia mwenyewe. Hospitali ina rekodi zangu za matibabu." Lisa alitabasamu kwa huzuni.

"Funga mdomo wako ikiwa hujui kuchagua maneno yako!" Joel alikasirika na kumkemea Melanie. “Kila mtu huko Dar es Salaam anajua kwamba mjomba na shangazi yake hata walimuua mama yao. Watu waovu kama hao wangemtendeaje wema mpwa wao?”

"Nini? Inakuwaje bado kuweko watu wasio na huruma hivyo?” Bibi Ngosha alishtuka na kuushika mkono wa Lisa kwa nguvu. "Mjukuu mpendwa, lazima uwe umeteseka sana, pole."

“Kuna msemo unaosema, daima kuna upinde baada ya mvua. Tazama, sasa, nina baba, babu na bibi kando yangu." Lisa aliinamisha kichwa chake, na ilikuwa kana kwamba nyota nzuri zilikuwa zikimulika machoni pake.

"Msichana mzuri kama nini." Bibi Ngosha alimpenda zaidi na zaidi.

Hata sura ya Mzee Ngosha ililainika sana, akafungua mdomo kwa mara ya kwanza. “Kwa kuwa umerudi kwa Ngosha, wewe ni mzao wa familia ya Ngosha. Ikiwa mtu yeyote atathubutu kukuonea siku zijazo, unaweza kutuambia, lakini hakikisha usiharibu sifa ya familia.”

“Asante, babu.” Lisa alitabasamu kupitia machozi yake. Nyakati nyingine, tabasamu la machozi huwapendeza zaidi waliozeeka.

Sura ya: 160

Pembeni, Nina na Melanie nusura wawe wazimu kwa hasira. Walikuwa wameandaa mambo mengi mabaya ya kusema juu ya Lisa mapema, lakini hawakutarajia Lisa angeteka huruma za wazee wale na kukonga mioyo ya Bibi na Babu Ngosha. Uso wa Nina ulizidi kudhoofika kwa hasira. Lisa Jones hakuwa mtu rahisi.

Wakati wa chakula cha jioni, Bibi Ngosha aliendelea kuweka chakula kwenye sahani ya Lisa. "Kula zaidi, wewe ni mwembamba sana."

“Asante, bibi.” Lisa alikula chakula chote alichopewa na bibi yake na hakuwa mbaguzi.

Bibi mzee aliridhika sana na kumgeukia Melanie ambaye alikuwa mbaguzi sana wa vyakula. “Hujawahi kuteseka hapo awali ndiyo maana unabagua bagua sana vyakula. Unapaswa kujifunza kutoka kwa dada yako."

“Bibi…” Uso wa Melanie ukawa mbaya kwa hasira.

Aliyeketi kinyume alikuwa mdogo wake na Joel, Damien Ngosha. Alicheka na kuuliza, "Melanie, ni lini utachumbiwa na Bwana Kimaro?"

Melanie aliona umati ukimtazama kwa kijicho na haraka akasema kwa aibu, “Bibi Kimaro alisema harusi itafanyika mwaka huu au mwaka ujao. Hatutachumbiana na tutafunga ndoa moja kwa moja.”

"Inaonekana Bibi Kimaro ana wasiwasi sana." Shangazi akatabasamu. "Hivi karibuni itabidi tukuite Bibi Kimaro."

Mzee Ngosha aliitikia kwa kichwa kuridhika. “Mshikilie Bwana Kimaro vizuri. Familia ya Ngosha itakutegemea katika siku zijazo."

Melanie alifurahi sana. "Babu, sitakuangusha."

Akiwatazama watu wote wakimpongeza Melanie, Lisa hakujisikia raha. Macho yake yalikuwa kwa baba yake mdogo, Damien Ngosha. Mwanamume huyo alikuwa ameketi kwenye kiti cha magurudumu, akiwapa watu huzuni sana.

Mara Nina akaibuka na hoja.“ Joel, uliahidi kumpa kaka yangu shamba lililo kando ya barabara ya Nakuru hapo awali. Mbona nimesikia ghafla ukizungumza na idara ya ardhi ili kuipa Mawenzi badala yake?” Nina alijifanya kana kwamba alikuwa amefikiria swali ghafla.

Mikono ya Lisa ilikakamaa, Joel akakunja uso. "Mawenzi ni kampuni ya Lisa. Kaka yako tayari ametengeneza mali nyingi hapa Nairobi na amepata pesa nyingi, kwa hivyo hili nitampa Lisa badala yake apate nafasi katika mji mkuu.

“Hiyo si kweli. Kaka yangu alipoteza pesa katika mradi wa mwisho na anategemea kuchukua shamba hilo ili atumie kuchukua mkopo.” Nina alitabasamu kwa uchungu. “Hata amemaliza kutengeneza proposal. Joeli, tusaidie kwanza. Tutatafuta kiwanja kingine cha kumfidia Lisa baadaye.”

Shangazi akaitikia kwa kichwa. "Nadhani tunapaswa kusaidia familia ya Mahewa kwanza. Lisa bado ni mdogo sana, kwa hivyo hataweza kushughulikia watu walio chini yake. Ataishia kuwa makucha ya paka.”

Damien pia alimshauri, “Ikiwa Joel hataki, basi mwombeni Bwana Kimaro msaada, Melanie. Litakuwa jambo rahisi kwake.”

Mzee Ngosha alipiga meza mara moja. "Inatosha. Mpeni Farres tu hiyo ardhi." Lisa aliinamisha macho yake chini kwa mbwembwe hafifu za dhihaka. Ilionekana kana kwamba katika uso wa masilahi, kila mtu katika familia ya Ngosha alikuwa na mwenendo sawa.

Baada ya chakula cha jioni. Joel aliondoka kwenye makao hayo akiwa na uso wenye huzuni, akiongozana na Lisa, Nina, na Melanie pamoja naye.

Baada ya kurudi nyumbani, Nina na Melanie walivaa nguo za kulalia na kwenda ghorofani kulala. Joel ghafla akamwambia Lisa,

“Usijali, tayari nimeshashughulikia masuala ya shamba lililo kando ya barabara ya Nakuru. Utapewa wewe.”

Lisa alipigwa na butwaa.

Nina aligeuka na kusema kwa hasira, “Joel Ngosha, uliahidi kumpa kaka yangu kabla ya Lisa!”

“Niliahidi hilo lini? Ni kitu ambacho nyote mlijisemea tu." Joel alipinga.

“Sijali. Shamba hilo lazima apewe Farres. Iwapo hukubaliani, nitamwambia Melanie aende kwa Bwana Kimaro akamwombe msaada.” Nina alishinikiza.

"Watu wengine wanaweza wasijue hili, lakini kusema kweli, sidhani kama Bwana Kimaro anampenda Melanie." Joel alicheka na kurudi chumbani kwake.

Lisa naye alirudi haraka chumbani kwake kwani alikuwa amechoka baada ya vita ya akili.

Nina alikanyaga miguu yake kwa hasira na kumwambia Melanie, "Kesho, nenda kwa Bwana Kimaro na umwombe atusaidie."

Melanie alionekana mwenye wasiwasi na kunong'ona, “Mama, hasira ya Bwana Kimaro ni ya kupita kiasi. Sijui kama yeye—”

“Lazima uende. Ikiwa hatakubali, unaweza kwenda Bibi Kimaro. Ni wakati wa kuthibitisha msimamo wetu katika familia ya Ngosha.” Nina alimkumbusha.

Macho ya Melanie yakaangaza na akakubali kwa kichwa.

•••
Nyuma ya Mlima wa Sherman kulikuwa na uwanja mkubwa wa farasi ndani ya eneo kubwa la ardhi lililomilikiwa na familia ya Kimaro, Farasi mmoja alikuwa akikimbia kwa kasi kwenye nyasi. Yule mtu aliyempanda farasi huyo alishika mjeledi mrefu. Mavazi yake meusi maridadi ya kupandia farasi yalimfanya aonekane mzuri na mtukufu kana kwamba ni mwanamfalme wa kale. Mwili wake ulitoa haiba ya kiume ya kustaajabisha.

Punde, farasi alisimama na Alvin akaruka chini kutoka juu ya farasi huyo. Watendaji wa kampuni ya KIM International walikusanyika mbele yake kwa haraka.

"Bwana Kimaro, ujuzi wako wa kupanda farasi unazidi kuwa bora na juu zaidi."

"Bwana Kimaro, wewe ni mzuri sana, unaweza kushinda hata upepo."

Alvin akawatazama tu watendaji wale waliokuwa wakijipendekeza kwake kwa maneno mazuri na kuwaambia, “Nendeni kwenye point.”

Mtendaji mmoja alisisitiza ujasiri wake na kusema, "Bwana Kimaro utarudi lini KIM International? Umeondoka kwa muda usiozidi miezi minne tu lakini faida ya kampuni imekuwa ikishuka. Bwana Jack Kimaro hatusikilizi kabisa na anasisitiza kufanya mambo anavyotaka mwenyewe. Tafadhali rudi kwenye kampuni."

"Bwana Kimaro, tunakuhitaji." "Kampuni haiwezi kufanya vizuri bila wewe." Mwingine alisisitiza hoja hiyohiyo.

Alvin alichukua maji aliyokabidhiwa na Hans na kuinamisha kidevu chake huku akimeza funda kubwa. Macho yake yalikuwa hayajali.

“Sawa nimewasikia, tokeni mbele yangu. Nitarudi kwenye kampuni wiki ijayo." Alvin alisema huku akijiandaa kuondoka.

'Hapo sawa. Karibu tena, Bwana Kimaro! Tutatoka machoni pako mara moja." Watendaji wale wakaondoka kwa furaha.

Hans alicheka na kupunguza sauti yake na kusema, “Bwana Kimaro, wewe bado ni bora zaidi. Hata baada ya kuondoka kwa miezi minne, Jack Kimaro bado hawezi kukonga nyoyo za watendaji hao.”

"Jack Kimaro ni kama baba yake, kwa hivyo najua yeye ni mtu wa namna gani, lakini mama yangu ... hatafurahi." Alvin alicheka kwa upole.

"Bwana Kimaro." Kuna mtu alimwita ghafla. Akakunja uso na kugeuka. Melanie, akiwa amevalia sweta nyeupe alimkimbilia haraka. Uso wake mzuri ulijawa na mshangao wa kupendeza. "Bwana Kimaro, nilimsikia Bibi akisema kuwa ulikuwa ukikimbia na farasi."

“Niko busy ongea shida yako.” Alvin alimpanda farasi. Angependelea kukimbia mizunguko michache zaidi kuzunguka uwanja kuliko kumsikiliza Melanie.

Melanie akawa na wasiwasi na haraka akasimama mbele ya farasi. "Bwana Kimaro, nahitaji kuzungumza nawe."

Hasira ya kutokuwa na subira iliangaza machoni pa Alvin, lakini aliivumilia. “Ni nini?”

"Unamkumbuka dada yangu wa kambo, sivyo? Alimhimiza baba yangu kumpa shamba lililoko kando ya barabara ya Nakuru, lakini baba yangu alikuwa tayari amemuahidi kumpa mjomba wangu shamba hilo hapo awali…” Melanie alisema kwa wasiwasi. Alihisi kwamba Alvin alikuwa akimpa subira, lakini hakuwa na jinsi. Hakuweza kusimama na kumtazama Lisa akipanda juu ya Nina na yeye.

“Kwa hiyo…” Alvin alimtazama kwa dharau huku pembe za mdomo wake zikitanuka kwa tabasamu pana.

Melanie alimtazama kwa huzuni. “Unaweza kunisaidia tafadhali?”

Alvin aliketi juu ya farasi na kumtazama chini kwa utulivu kwa muda. Ghafla, alitabasamu na kusema. “Hakika.”.....ITAENDELEA...

Unafikiri nini kitafuata hapo maana mambo ni moto mambo ni fire, lakini sina cha kusema nikuombe tuungane pamoja katika sehemu inayofuata ya mkasa huu wa kusisimua unaokwenda kwa jina la LISA.