JINA LA SIMULIZI............................LISA

AUTHOR...........................JOMBA WAJO
SPONSORED BY......SIMULIZI ZA DULLY
WHATSAPP...........................0628924768
SEHEMU YA................................151-152

Sura ya: 151

Hatimaye wakati wa chakula cha jioni ulipofika, Lisa alisema kwa uwazi, “Kama binti haramu, sina haki ya kula na Bwana Kimaro. Nitakula chakula changu cha jioni jikoni.” Alipomaliza kuongea mara moja alinyanyuka kuelekea jikoni kabla ya mtu yeyote kuzungumza.

Alvin aliishiwa pozi ghafla huku Melanie akisema kwa majivuno, “Ni vizuri kwamba anajitambua.”

Ingawa Joel hakupendezwa na maneno hayo, hakutaka kusema neno lolote.

Mpishi alikuwa ametumia siku nzima kuandaa chakula cha jioni kama alivyoagizwa na Nina. Hata hivyo, Alvin aliacha kula baada ya kuchota vijiko viwili tu vya chakula. Tangu alipoachana na Lisa, hakuwa na mlo mnono kabisa. Siku zote alijikuta ana njaa tu.

"Bwana Kimaro, chakula hiki sio kitamu vya kutosha kutosheleza hamu yako?" Nina aliuliza kwa tahadhari. “Mbona umeonja tu na kuacha?”

“Nimeshiba kwani nilikula matunda na karanga muda si mrefu. Nyie endeleeni tu, mimi naenda chooni mara moja.” Alipomaliza kuongea, alinyanyuka kuelekea chooni.

Ilikuwa lazima kupita jikoni ili kuelekea chooni. Alipoingia jikoni, alimuona Lisa akifurahia chakula chake kwenye meza ndogo. Kwa kweli aliweza kula sana licha ya kumuona akiwa na mwanamke mwingine. Alvin kwa namna fulani alihisi hasira ikichemka ndani yake. Kwanini Lisa asiwe na wivu naye hata kidogo? Alimsogelea bila kujali na kumtania, “Nina hakika hukuwahi kupata mlo mzuri namna hii huko Dares Salaam tangu nilipoondoka. Jiangalie mwenyewe. Inaonekana kana kwamba umelala njaa maisha yako yote.”
Lisa aliinua kichwa chake na kumtazama kwa uso uliokereka. Alihisi uvimbe wa hasira kwenye koo lake ukitaka kupasuka. "Ndio, nimekuwa na njaa maisha yangu yote, kwa hiyo wewe unatakaje?" Alipokuwa akiongea, alimtemea wali usoni kwa makusudi.

"Lisa, unajiombea kifo?" Uso wa Alvin ulijawa na hasira. Mate na wali vilikuwa vimemtapakaa usoni na mwilini. Haraka akaitumia mikono yake kujifuta kwa sura ya kuchukia.

“Samahani. Kwa vile mimi ni mshamba wa kijijini na sina ustaarabu. Wazazi wangu hawakuwahi kunifundisha adabu.” Lisa alitabasamu. “Bwana Kimaro, samahani sana. Kutokana na hadhi yako ya juu, natumai hutakwazika na mapungufu yangu, sivyo?”

Alvin alipandwa na hasira. "Lisa, unapata raha sana kutokana na uigizaji wako, eeh? Ninakuonya sasa, ondoka Nairobi mara moja. La sivyo usinilaumu kwa kitakachokutokea.”

Kadri Alvin alivyozidi kuchukia ndivyo Lisa alivyozidi kutabasamu. “Ninasikitika huna haki ya kuamua hili, Bwana Kimaro. Wewe si Rais wa nchi hii.”

"Unafikiri kwamba sifahamiani na Rais?" Alvin alicheka sana. "Hata hivyo, ni kazi rahisi tu kukuondoa. Muda si mrefu utaichukia kabisa Kenya."

Lisa alipigwa na butwaa kwa muda na uso wake ukakunjamana. “Kwa nini niondoke? Kwani uwepo wangu hapa unakupa karaha? Nimekuja kimpango wangu na nitaondoka kimpango wangu, hebu niache mimi nifurahie chakula changu.”Jinsi Alvin alivyochukia alitamani kuuchanachana uso wake kwa makucha.

“Bwana Kimaro, hujaenda chooni bado? Mnafanya nini hapa?” Melanie aliingia ghafla baada ya kumaliza chakula chake kwa haraka. Aliwaona Alvin na Lisa wakizungumza kama watu wanaojuana muda mrefu. Kwa vile wote wawili walikuwa wamevalia nguo za kijivu, walionekana kama wanandoa katika mavazi yao yanayofanana.

Harakaharaka Melanie akamshika mkono Alvin, huku akionekana kuhofia mtu wake kunyang'anywa. Alvin aliinua kichwa chake, macho yake yakaangaza kwa huzuni. Kisha akatoa tabasamu la uongo na kweli. "Nilitaka kwenda chooni lakini Lisa alinizuia na kujaribu kunitongoza."

"Nini?" Melanie alikasirika sana hivi kwamba macho yake yalikaribia kuchomoka kwenye soketi zake.

Lisa alimtazama Alvin bila kuamini, na kumkuta akitabasamu. Muda si muda alijifanya kuwa na sura ya huzuni huku akisubiri kutazama tamthilia hiyo aliyoianzisha. Lisa aliuma meno kwa hasira. Alvin alikuwa mtu mbaya sana!
Melanie akawaka kwa hasira. "Lisa, huna aibu kama mama yako!"

“Samahani, ninakuzidi miezi michache kiumri, kwa hiyo ni wazi kwamba mama yangu alikutana na baba yangu mapema zaidi ya mama yako. Kwa mantiki hiyo mama yako alikuwa ni hawara tu wa baba yangu, yeye ndiyo aliyekosa aibu. Chunga mdomo wako. Pia, sikumtongoza Alvin.” Lisa alimpa vipande vyake.
"Hah, kwa hiyo unamaanisha kuwa Bwana Kimaro anakusingizia?" Melanie alimkosoa Lisa kwa uchungu. “Angalia tu hadhi ya Bwana Kimaro. Yeye ni mtu maarufu wakati wewe ni mtu wa hali ya chini. Akusingizie wewe kwa lipi hasa?”
Lisa aliinamisha macho yake chini, mapigo ya moyo wake yakitikisika kwa nguvu kifua chake. Alvin alikunja uso. Alikasirika ghafla japokuwa yeye ndiye alitaka kumchonganisha Lisa. Tangu mwanzo hakuwa na hisia zozote na Melanie. Licha ya kujilazimisha kumkubali, alizidi tu kukerwa na Melanie aliyekosa adabu. Tabia yake mbovu ilimfanya aonekane kama binti aliyelelewa na familia isiyo na maadili na si binti aliyetoka kwenye moja ya familia mashuhuri hata kidogo.
“Nyie mnabishana kuhusu nini?” Joel na Nina waliingia jikoni baada ya kusikia mtafaruku huo.
“Baba, Mama, mmekuja kwa wakati muafaka. Kwa kweli Lisa alikuwa akijaribu kumtongoza Bwana Kimaro” Melanie akalalamika mara moja, “Mama, hata alikudhihaki kwa kukuita wewe ni hawara tu wa baba.”
Uso wa Nina ulibadilika mara moja. “Sababu iliyomfanya Joel anioe enzi hizo ni jambo lisilo kuhusu kabisa we binti, unasikia? Umeenda mbali sana Lisa. Nimekuwa nikikutendea vizuri kabisa tangu ulipofika jana. Nilikununulia hata nguo nzuri umevaa umependeza. Badala ya kushukuru, unapandisha kiburi hata kumtongoza mchumba wa dada yako na kunitusi mimi mbele yake? Huku ni kukosa shukrani na heshima.”
Joel naye akakunja uso na kuingilia kati. "Kunaweza kuwa na kutokuelewana tu..."
“Kutokuelewana gani?” Melanie alimkatisha bila subira. “Bwana Kimaro alisema mwenyewe kuwa Lisa alikuwa akimtongoza. Licha ya kuwa na mchumba, bado ana tabia chafu. Hana aibu hata kidogo!”
“Mchumba?” Alvin aliuliza huku akitabasamu. Ni wale tu waliomfahamu vyema ndio walioweza kuhisi hasira kali katika macho yake yaliyoanza kubadilika ghafla.
“Ndio. Ana mchumba huko Dar es Salaam," Nina akaongeza haraka, "Hata hivyo, mwanamume mwenyewe ni mmiliki wa kampuni ndogo tu, hana lolote. Yeye ni kapuku tu ukilinganisha na wewe."
“Kweli?” Alvin akatabasamu kwa unyonge. Alikuwa ameondoka Dar es Salaam kwa siku chache tu, lakini tayari Lisa alikuwa na mchumba. Bila kujisumbua kufikiria sana, alikuwa na hakika kwamba mtu huyo alikuwa Kelvin Mushi. Alipokumbuka masinema yote aliyomchezea kuhusu Kelvin, ghafla alijiona mjinga sana. Mwanamke huyo alikuwa mjanja kuliko vile alivyofikiria.
"Wanasema familia ya Ngosha imetulia, lakini kilichotokea usiku wa leo kinanifungua macho." Alvin alikoroma. Baada ya kumaliza kuongea, alielekea mlangoni. Alipompita Joel, alinyamaza kwa muda kabla ya kusema, “Uncle Ngosha, nitaondoka kwanza. Leo sina hamu ya kukaa hapa tena.” Kwa hayo, akatoka nje ya nyumba.
"Nisubiri Bwana Kimaro." Melanie alimfuata Alvin.
Mwale wa mwanga wa joto uliangaza uso wa Lisa alipokuwa amesimama jikoni, ukimulika uso wake uliojaa hofu. Lisa ndiyo kwanza alikuwa amefika nyumbani kwa baba yake na alikuwa bado hajatulia katika familia hiyo. Hata hivyo, maneno ya Alvin yalikuwa yamemsukumia ndani ya shimo.
“Angalia ulichofanya!” Nina alikuwa akitetemeka kwa hasira. “Joel wewe ndio ulitaka kumleta nyumbani, lakini kufika tu hapa anataka kuiba mpenzi wa dada yake. Nani anajua ni matatizo gani atatusababishia huko mbeleni? Sasa kwa kuwa tumemkosea Bwana Kimaro, nakushauri umwondoe haraka. Hatupaswi kuichukiza familia ya Kimaro na kuwafanya washindwe kushirikiana nasi.”

Sura ya: 152

Lisa ni binti yangu, na nimekuwa na deni naye kwa zaidi ya miaka 20. Hii ni nyumba yangu na pia familia yangu. Anaweza kukaa hapa muda wowote anaotaka. Ikiwa nyinyi wawili hamfurahii, mnaweza kuhama,” Joel alijibu bila huruma.

Uso wa Nina ulijawa na hasira. Mwishowe, alimtazama Lisa kwa macho makali kabla ya kuondoka. “Sawa. Ikiwa kuna mabadiliko yoyote katika mipango ya ndoa ya Melanie, Lisa atawajabikia kwa kukosa kwake heshima.” Nina alipomaliza kuongea tu aliondoka huku akihema.

“Baba, sikumtongoza Bwana Kimaro,” Lisa alisema kwa uzito. Hakujali jinsi wengine walivyomwona, lakini ikiwa Joel angeamini yale ambayo wengine walisema, angevunjika moyo sana na kupoteza imani naye.

Joel akashusha pumzi na kusema taratibu. "Nakuamini. Bwana Kimaro pengine alikwazika kwa kusikia kuwa wewe ni mtoto wa nje ya ndoa, ndiyo maana ana chuki dhidi yako.”

“Kwanini akwazike, kwani inamhusu nini?” Lisa alipigwa na butwaa kidogo.

Joel kisha akamweleza Lisa historia fupi ya Alvin, “Malezi ya Bwana Kimaro ni ya kusikitisha sana. Mama yake, Lea Kimaro, alikuwa msichana mzuri mwenye akili nyingi tangu umri mdogo, kama wewe tu vile. Ndio maana aliweza kujitokeza hata kama mwanamke mwenye uwezo wa kurithi KIM International.”

Joel akaendelea wakati Lisa akisikiliza kwa makini. “Wakati huo, walikuwa wakiishi Tanzania, wanaume wengi matajiri walitaka kumwoa Lea, lakini bwana mmoja aitwaye Mike Tikisa alipanga njama dhidi yake kwa kulala naye baada ya kumlewesha madawa na punde akampa mimba. Kwa hilo, hakuwa na chaguo ila kuolewa naye.”

Lisa alishtuka. Haishangazi Alvin alikasirika sana wakati alipomwekea madawa ya nguvu za kiume kwenye chakula hapo awali. Alikuwa ameguswa hasa kwa jambo hili kutokana na ukweli kwamba alizaliwa kwa njia hiyo pia!

Joel aliendelea, “Kuwasili kwa Bwana Kimaro duniani kulikuwa tukio lisilokubalika kwa Lea. Lea pia hakumpenda sana Alvin kwa sababu alimchukia baba yake sana. Muda mfupi baadaye, alitalikiana na Mike Tikisa na kuolewa na mpenzi wake wa zamani, Bwana Mason Campos ambaye alikutana naye chuoni. Kisha, akajifungua mtoto mwingine wa kiume anayeitwa Jack Kimaro.”

"Ndiyo sababu kwamba amekuwa na huzuni tangu utoto?" Lisa alinong'ona kwa hisia zinazopingana.

“Ndio. Baada ya talaka, Mike Tikisa alikuwa mtu wa kulewa tu kila siku. Lea, kwa upande mwingine, akaunda familia mpya. Anamjali Jack kwa mapenzi mazito. Kwa macho ya Alvin, anawachukulia Jack na baba yake kama wavamizi kwani waliharibu familia yake na kusababisha baba yake awe mlevi tu. Ndio maana naye anakuchukia kwa kuwa ni mtoto wa nje.” Joel aligusa kichwa chake kwa hisia. “Samahani, Lisa. Nisamehe kwa kukufanya uteseke…”

“Sio kosa lako, baba.” Licha ya maelezo ya Joel, Lisa alijuwa yeye ndiye alikuwa chanzo cha chuki ya Alvin, hivyo akashauri. “Baba, nadhani niondoke kwanza. Vinginevyo, Aunty Nina na Melanie bila shaka wataanzisha vita na mimi.”

Hapo awali Lisa alipanga kubaki hapo ili kupambana na Nina uso kwa uso. Hata hivyo, kwa kweli hakutaka kumuona mpenzi wake wa zamani akiishi kwa ukaribu na dada yake wa kambo.

"Hapana. Sasa kwa kuwa hatimaye umerudi, sina budi kukutunza na kukuweka chini ya ulinzi wangu.” Joel alikuwa na wasiwasi kwamba asingeweza kumtunza Lisa vizuri ikiwa angeishi peke yake. Kisha akaongeza, “Hili ni suala letu la kibinafsi la familia. Huwezi kuondoka hapa kwa sababu tu ya uchumba wa Melanie na Bwana Kimaro. Kama haitawezekana tutaghairi mpango wa ndoa na familia ya Kimaro.”

Lisa aliguswa na kujawa na faraja moyoni mwake. Alijisikia vizuri sana kuwa na baba ambaye alimwamini bila masharti.

Asubuhi iliyofuata. Lisa akijua hakukaribishwa vyema kwenye familia hiyo, aliamka mapema kwa makusudi. Baada ya kuoga alijiandaa kuelekea ofisini. Alipokaribia kutoka nje ya nyumba hiyo, aliwaona Melanie na Alvin wakiingia nyumbani wakati wa jua la asubuhi wakiwa wameshikana mikono.

Wachumba hao wenye sura nzuri walionekana kama wanaendana vizuri. Lisa alihisi kuwa macho yake yanauma. Ina maana walikuwa tayari wamependana sana hadi watafutane asubuhi na kupata kifungua kinywa pamoja? Lisa aliinamisha kichwa chake akijifanya hajawaona na kuongeza mwendo wa kasi kuelekea eneo ambalo dereva aliegesha gari.

"Simama hapo, Bi. Jones. Baada ya tukio la jana usiku, bado hujajifunza kuwa na adabu, huh?” Alvin alimzuia, uso wake ukionyesha dhihaka kama kawaida.

Lisa alipokumbuka alichoambiwa na Joel kuhusu historia ya Alvin, hakujishughulisha na kubishana naye, ila tu akamwambia kwa utulivu. “Nafikiri mtu wa hali ya chini kama mimi hastahili kukusalimia. Zaidi ya hayo, najiandaa kuelekea ofisini.”

“Ofisini?” Macho ya Melanie yalitetemeka, akauliza, "Unaenda kufanya kazi katika kampuni yetu?"

"Hapana. Usihofu. Sitaingia katika kampuni ya Ngosha. Mama yangu aliniachia kampuni kubwa huko Tanzania, ina ofisi yake ndogo hapa Nairobi ndiyo naenda kuikagua.” Lisa alitoa tabasamu la kukosha. Macho yake angavu na makali yalionekana kuweza kuona mawazo potofu ya Melanie.

Melanie alikoroma kwa aibu, “Bila shaka, nina wasiwasi. Hujui lolote. Ninaohofia tu kwamba utafanya kazi huko hovyohovyo uharibu kampuni yetu.”

“Nilifikiri ulikuwa na wasiwasi kwamba ningechukua urithi wa familia ya Ngosha.” Lisa alitabasamu kwa unyonge.

"Wewe ni mshamba tu wa kijijini." Melanie alionekana kama amesikia utani. Alimgeukia Alvin na kusema, “Bwana Kimaro, unamwona jinsi alivyo na ndoto za abunuwasi? Sijawahi kumtilia maanani kabisa. Sio tu kwamba hajasoma, lakini pia ni mshamba wa kijijini ambaye hajui jinsi ulimwengu ulivyo.”

Alvin akampa jicho la pembeni. Ikiwa hakumjua Lisa, angekubaliana na maneno ya Melanie, lakini Lisa alikuwa mhitimu kutoka katika moja ya taasisi bora zaidi nje ya nchi. Alishinda hata tuzo katika usanifu na muundo wa mambo ya ndani. Alikuwa bora zaidi kuliko Melanie, binti mpendwa wa familia ya Ngosha ambaye alipoteza pesa za wazazi wake kwa kusoma nje ya nchi na akarudi na felia. Lakini Melanie hakugundua kuwa akilinganishwa na Lisa, alionekana tu mtu asiye na akili na mjinga.

Lisa alikuwa amevaa koti la kawaida la rangi ya zambarau siku hiyo. Akiwa na macho yake angavu, meno meupe, na sura safi, Alvin alikiri moyoni mwake kwamba ilikuwa ni sawa na ardhi na mbingu kumlinganisha Melanie na Lisa.

“Ndiyo, mimi ni mtu wa kijijini tu, huku wewe ni mwezi mkali unaoning’inia angani. Nisingethubutu kujilinganisha na wewe.” Tabasamu la Lisa lilikuwa shwari na lisilojali, kama maua lili meupe.

"Ni vizuri unajua hilo." Melanie alitabasamu kwa kiburi.

“Inatosha, ingia...” Alvin aliona ujinga tu kusikia dada wale wawili wakirumbana, akamsukuma Melanie kuingia ndani. Melanie alitangulia haraka. Hapo ndipo Lisa alitoka na kuingia kwenye gari.

Katika ukumbi wa kulia chakula, kulikuwa na meza iliyojaa vyakula vitamu. Melanie aliweka chakula kwenye sahani ya Alvin kwa makini, lakini kadri Alvin alivyokuwa akimwangalia ndivyo alivyozidi kukereka. Mwishowe Alvin akainuka na kusema, “Sina hamu ya kula, naondoka.”

“Bwana kimaro…” Melanie alishindwa kumwelewa. “Kuna kitu nimekukosea?”

"Kwani ni lazima unikosee ndipo niondoke? Usinifuate,” Alvin alifoka kwa kejeli na kugeuka nyuma bila kujali. Melanie alitazama umbo lake refu na lililo wima likiondoka. Alikosa raha kiasi kwamba machozi yakamtoka.

"Nini kimetokea?" Nina akamfuata haraka.

“Mama, hata mimi sijui.” Melanie alifikiria kabla ya kusimulia jinsi alivyokutana na Lisa mlangoni hapo awali na maneno yote ya dhihaki aliyomtusi.

“Mjinga wewe!” Nina alimkaripia, “Lisa alifuzu kujiunga katika chuo kikuu maarufu duniani alipokuwa na umri wa miaka 16 tu, na miaka yote alipata alama za juu. Alishinda tuzo kadhaa za kifahari katika usanifu na muundo wa mambo ya ndani. Alikuwa mwanafunzi bora katika mtihani wa taifa wa shule ya sekondari na aliongoza kwenye mtihani wa taifa wa kidato cha sita wa mwaka wake. Yeye ni tofauti kabisa na mtu kama wewe ambaye ulitumia pesa kununua diploma yako.”

Melanie alipigwa na butwaa kabisa. Akifikiria nyuma yale aliyokuwa amesema hapo awali, alihisi kufedheheshwa sana sasa. "Lakini Bwana Kimaro hafahamu yote hayo, si ndiyo?"

"Nani anajua? Bwana Kimaro ana habari za kutosha. Labda tayari amechunguza kila kitu kuhusu familia yetu kabla ya kukutana na wewe.” Nina alionekana mwenye huzuni. "Pia niligundua kuwa Lisa sio mtu rahisi sana kushughulika naye. Ni miezi miwili tu imepita tangu achukue mikoba ya Mawenzi Investiments, lakini tayari amewanyoosha wafanyakazi wote kwenye mstari wake.”

“Kwa hiyo nifanye nini?” Melanie alikuwa mpole ghafla.

“Jiepushe na mambo yake. Niachie mimi nitamshughulikia mwenyewe. Ni lazima tu utekeleze wajibu wako kama binti aliyelelewa vizuri kutoka kwa familia yenye hadhi.” Nina alikuwa anaumwa na kichwa. Ilikuwa ni kosa lake kutomsomesha bintiye vyema. Melanie hakuwa na hata nusu ya ujuzi aliokuwa nao yeye alipokuwa mdogo.....ITAENDELEA.....

Unafikiri nini kitafuata hapo maana mambo ni moto mambo ni fire, lakini sina cha kusema nikuombe tuungane pamoja katika sehemu inayofuata ya mkasa huu wa kusisimua unaokwenda kwa jina la LISA.