JINA LA SIMULIZI............................LISA
AUTHOR...........................JOMBA WAJO
SPONSORED BY......SIMULIZI ZA DULLY
WHATSAPP...........................0628924768
SEHEMU YA................................149-150
Sura ya 149
Usiku sana, akiwa amesimama kwenye kibaraza, Lisa aliweza kuona nyumba ya familia ya Kimaro kutoka mahali alipokuwa. Usiku huo, taa zote zilimulika. Aliweza kuhisi kwamba ndani ya jumba hilo kulikuwa na shughuli nyingi. Alishangaa pale kwa muda, akashusha pumzi taratibu kisha akarejea kujilaza tena kitandani. Hata hivyo, alikuwa na shida ya kupata usingizi.
Asubuhi, Lisa alishuka chini mapema sana baada ya kukosa usingizi usiku. Mazingira ya pale sebuleni yalikuwa tofauti kabisa.
Joel alitulia tuli kwenye kochi huku Melanie akikumbatia mkono wake na kusema kwa furaha, “Baba, hujui jinsi Bwana Kimaro alinitendea kwa shauku jana usiku. Miongoni mwa mabinti wote, alivutiwa na mimi kwa mtazamo wa kwanza na hata akanialika nicheze naye. Bibi Kimaro pia alikuwa na mazungumzo ya muda mrefu nami, akiniomba niwe mpenzi wake.”
Nina alitabasamu kutoka sikio hadi sikio. "Mungu ndiye mtoaji wa bahati nzuri. Nilijua Melanie angeweza kumpata mpenzi sahihi kwa uzuri na kipaji chake, lakini sikutarajia angeweza kuolewa na Bwana Kimaro. Familia ya Kimaro ni miongoni mwa familia tajiri zaidi hapa Nairobi. Mali zote za familia ya Kimaro zitakuwa zako katika siku zijazo.”
"Usisahau kuna Jack Kimaro pia katika familia." Akiwa amekunja uso, Joel aliwakumbusha Nina na Melanie baada ya kusikia maneno yao ya tamaa.
"Kwa hiyo?” Nina aliuliza kwa nyodo. “Ingawa kila mtu anajua kwamba Bwana Kimaro ameondoka KIM International wakati fulani, Jack hana uwezo wa kusimamia kampuni vizuri.”
Melanie alisema kwa kiburi, “Hata kama Bwana Kimaro hatapata kuchukua uongozi wa KIM International, utambulisho wake kama kaka mkubwa wa familia bado ni bora. Hakuna mtu mwingine ambaye ningependa kuolewa naye maishani mwangu isipokuwa yeye.”
Nina alijawa na tabasamu. "Wote wawili mlipendana mara ya kwanza na mmeundwa kwa ajili ya kila mmoja."
Joel alifichua chembe ya kero. "Kwa hivyo ulihudhuria hafla ya familia ya Kimaro kwa ajili hiyo. Kwanini mlinificha? Mliogopa kwamba ningemwomba Lisa ajiunge pia, huh? Kwanini mna mawazo mabaya kama hayo?"
Melanie alipiga kelele. “Kuna maana gani ya kumtaka ajiunge nayo? Kwa kuzingatia kwamba hajawahi kuona tukio kubwa kama hilo, nilikuwa na wasiwasi kwamba angeiletea aibu familia yetu. Zaidi ya hayo, si tayari ana mchumba? Ikiwa atakutana na watu wengi matajiri hapa Nairobi, anaweza kuamua kumwacha mchumba wake ambaye ni masikini kama yeye mwenyewe.”
“Wewe…” Joel alikasirika sana hadi akapiga meza na kusimama. Hata hivyo, dakika tu alipomwona Lisa akiwa amesimama kwenye ngazi, aliganda ghafla. “Lisa…”
“Lo, Lisa, usimchukie Melanie.” Nina alivaa tabasamu. “Kwa kweli, Melanie alikuwa na wasiwasi kwamba hujazoea kuhudhuria karamu kama hizo, ikizingatiwa kwamba wewe bado ni mgeni hapa. Zaidi ya hayo, hafla za familia ya Kimaro huwa za ajabu kila wakati.”
Lisa aliinua macho yake kwa siri. Mama yake wa kambo alikuwa mbunifu sana katika kutamka maneno yake. Mwisho wa siku, walitaka tu kumdhihaki kwa sababu eti hajatembelea sehemu kubwa ya ulimwengu. Hawakujua kwamba Lisa alikuwa ametembea sana na hata kusoma Chuo Kikuu Marekani. Na huyo Alvin Kimaro waliyekuwa wakimshobokea kwake alikuwa zilipendwa!
“Haijalishi. Kuweza kuwa binti wa familia ya Ngosha ni heshima kwangu. Sina nia ya kujipandisha hadhi kwa kudandia wanaume matajiri hata kidogo.” Lisa alitoa tabasamu hafifu na la upole.
Nina na Melanie walipigwa na butwaa. Je, Lisa alikuwa akijaribu kuwakejeli kwa kuwa na pupa ya kutamani familia za hadhi ya juu licha ya asili yao yenye nguvu tayari? Hakika Joel alionekana kukasirika zaidi huku akiwatazama Nina na Melanie.
Nina alisema, “Hubby, ninafanya hivi kwa ajili yako. Ikiwa binti yetu anaweza kuolewa na Bwana Kimaro, hali yako itakuwa tofauti.”
"Baba, mimi sasa ni rafiki wa kike wa Bwana Kimaro," Melanie akaongeza kwa kufoka, "Bwana Kimaro alisema atakuja usiku wa leo kula chakula cha jioni."
"Nini? Bwana Kimaro anakuja?" Nina alitetemeka kwa fadhaa. “Hubby, umesikia hivyo? Inaonekana Melanie ataolewa na Bwana Kimaro hivi karibuni."
Joel pia alishangaa sana. Hata hivyo, ikiwa Bwana Kimaro alikuwa anakuja kweli, ilimbidi amtendee kwa uangalifu. "Sawa, nitamwomba mtumishi wa jikoni aandae chakula kizuri zaidi na divai nzuri usiku wa leo."
Akiwa na furaha kupita kiasi, Melanie alisema upesi, “Baba, nadhani nina kabati ndogo. Nahitaji kuvaa vizuri kwani Bwana Kimaro anakuja usiku wa leo!”
"Sawa, nenda kachukue nguo na mama yako." Joel akatupa kadi. “Usiendelee kumnunulia Melanie nguo pekee. Lisa amekuja na ana nguo chache sana, kwa hivyo mpe seti 20 hadi 30 za nguo pia. Agiza maduka yakuletee hapa mara moja."
Tabasamu za Nina na binti yake zikawa ngumu. Melanie alipokuwa karibu kudhihirisha kufadhaika kwake, Nina alimkazia macho. Baada ya hapo, wawili hao walienda kufanya manunuzi.
Joel alihema huku akiwatazama wakiondoka. “Lisa, natumai huna shida. Dada yako ni mpenda mali na amedekezwa sana na mama yake.”
“Baba, ni sawa. Usijali.” Lisa akatikisa kichwa kwa tabasamu mwanana. Macho yake meusi yalikuwa angavu na ya kupendeza. Hakuwa amepaka kitu chochote usoni mwake, na alionekana aking’aa kama theluji.
Joel alipigwa na butwaa kidogo. Moyoni alimuonea huruma. Kwa mrembo kama Lisa, kwa kweli alikuwa anamfaa kabisa Bwana Kimaro. Kwa bahati mbaya, hatima ilikuwa ya kikatili. Alitamani angemleta nyumbani mapema.
"Twende, nitakupeleka kwenye ofisi za Ngosha Corporation kwa ziara fupi."
Lisa hakupendezwa na Ngosha Corporation. Hata hivyo, alitembelea ofisi hiyo kwa kuwa hakuweza kukataa ombi la fadhili la baba yake. Alirudi tu kutoka ofisini na baba yake saa moja jioni. Taa zilizokuwa zimewashwa katika nyumba ya Ngosha zilimulika sana. Mimea na maua mengi ya bei ghali pia yaliongezwa kwenye ua uliokuwa umesafishwa vizuri.
Walipoingia ndani ya nyumba hiyo, Nina alikuwa akiwaamuru watumishi wafanye usafi katika eneo jirani. Melanie alikuwa amebadilika na kuvaa vazi la juu la sufu ambalo lilikuwa la gharama kubwa zaidi msimu huo. Alivaa sketi ambayo ilikuwa imeunganishwa na jozi ya tight. Pia kulikuwa na kitambaa cha manyoya kikiwa kimezungushiwa mabegani mwake. Alitengeneza nywele zake ndefu kimakusudi pia. Sehemu ya mbele ya nywele zake ilikuwa imejikunja na nyuma yake ilikuwa imesukwa. Alionekana kama binti wa kifalme.
“Hubby, nilisikia umempeleka Lisa ofisini leo, sivyo?” Nina alimsogelea Joel na kumuuliza huku akijua kila kitu.
“Kuna ubaya wowote kumpeleka binti yangu ofisini?” Joel alikunja uso.
"Bila shaka hapana." Huku akizuia chuki yake ndani kabisa, Nina alisema huku akitabasamu, “Lisa, nimekununulia nguo nyingi za chapa maarufu leo. Nguo hizi pengine hazipatikani Dar es Salaam. Nenda ukajaribu nguo sasa. Huwezi kuvaa vibaya wakati Bwana Kimaro atakapokuja baadaye.”
Lisa alipopanda ghorofani na kufungua kabati lake, alitabasamu baada ya kuona nguo zile mle ndani. Hakika zote zilikuwa nguo zenye chapa maarufu, lakini, zote zilikuwa aimepitwa wakati miaka kadhaa iliyopita na hazikuweza kuuzika kwa sababu ya rangi zake za kizamani. Ikiwa angekutana na kina Janet huko Dar es Salaam akiwa amevaa mojawapo ya nguo hizo, bila shaka angechekwa hadi azimie. Lakini, haikuwa muhimu kwake kwani alijiamini juu ya uzuri wake.
Dakika 20 baadaye, alishuka ngazi. Nina na Melanie, ambao walikuwa wakimtarajia aonekane wa kizamani katika mavazi yale, walipigwa na butwaa mara moja. Lisa alivaa koti refu la kijivu ambalo Nina alinunua. Jacket ilikuwa kubwa sana ilionekana kama blanketi juu yake. Bila shaka, mtu yeyote wa kawaida aliyevaa koti hilo angeonekana kuwa kituko, lakini, Lisa hakufunga zipu ya koti hilo, akaliacha wazi. Aliiunganisha na kitop cheupe cha rangi ya cream na suruali nyeupe ya kawaida. Hakuwa amepaka chochote usoni mwake, isipokuwa ndomoni aliweka lipstick nyekundu. Alionekana kama binti safi na mrembo mwenye umri wa miaka 17 au 18. Ikilinganishwa na Lisa kando yake, Melanie alionekana mwenye urembo mwingi zaidi na uso uliopambwa sana hadi ukapitiliza.
Lisa kwa makusudi alisema huku akitabasamu, “Asante kwa nguo, Aunty Nina. Zinanipa joto sana na hili baridi la Nairobi. Nimezipenda sana.”
"Nimefurahi kwa kuwa umezipenda." Nina alikuwa akihema kwa hasira. Wakati huo, aligundua kuwa Joel alikuwa akimwangalia sana.
Ijapokuwa Joel hakuwa mzoefu wa nguo, aliona wazi nia ya mkewe. Kwa bahati nzuri, Lisa alikuwa na mwili wa kuvutia na mwonekano bora zaidi, kwa hivyo angeonekana mzuri katika nguo yoyote.
Wakati huo, mtumishi aliingia na kusema, “Bwana Kimaro yuko hapa.”
Wale wanne wakatoka mara moja kwenda kumpokea. Gari aina ya Rolls-Royce lilisonga taratibu kuelekea kwenye jumba la kifahari. Baada ya gari kusimama, dereva alitoka na kufungua mlango wa nyuma. Mtu mtukufu, mashuhuri alitoka nje. Alivaa koti la kijivu na suti ya kijivu. Kwa kuzingatia mavazi yake, ilikuwa ni lazima kabisa kuzingatia sura ya mtu huyo. Kwa kushangaza, mavazi hayo yalimfaa vizuri. Miguu yake mirefu ilifanana na ya mwanamitindo wa hali ya juu, ilhali uso wake ulikuwa mzuri sana hivi kwamba hakuweza kupatikana hata kasoro ndogo.
Kipindi Lisa alipomtazama vizuri mtu huyo usoni, kichwa cha Lisa kilianza kuunguruma bila kukoma. Inawezaje kuwa yeye?!
Alijua kwamba Willie alikuwa anamuogopa Alvin, hivyo aliamini kabisa kwamba Alvin alikuwa na hadhi ya juu kabisa katika familia ya Kimaro. Hata hivyo, asingeweza kamwe kutarajia kwamba alikuwa akitetemekewa kiasi kile na familia tajiri za kitongoji kile maarufu, mtu tajiri zaidi katika eneo lote lile lililokaliwa na matajiri wa Kitanzania waliowekeza nchini Kenya, na pengine kitongoji tajiri kuliko vyote jijini Nairobi!
Pamela alikuwa amemuelekezea kwa bahati mbaya wakati huo, na kumfanya ahusishwe na mtu maarufu kama huyo. Sasa ujio wake pale ulimaanisha kwamba alikuwa mpenzi wa Melanie. Alikuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa shemeji yake katika siku zijazo.
Sura ya 150
Uso wa Lisa ulibadilika polepole. Alipata hisia kali kwenye kifua chake, ambayo ilimsababishia maumivu. Ikiwezekana, alitamani asingemwona tena maishani mwake.
“Umefika Bwana Kimaro!” Melanie alimsogelea Alvin kwa unyonge na kumshika mkono wake kana kwamba walikuwa wanandoa kwenye mvuto wa kwanza wa mapenzi.
“Ndiyo.” Alvin alikunja uso kwa namna isiyoonekana, akijiuliza ni nini kinamsibu binti huyo. Walikuwa wamecheza pamoja tu jana yake usiku, lakini alijifanya kuwa karibu kwake kana kwamba walikuwa kwenye uhusiano kwa muda mrefu. Wakati tu alipokaribia kuachana naye, Joel na Nina walimkaribia.
"Habari, Bwana Kimaro." Joel alimpa mkono Alvin taratibu.
“Habari, Mr. Joel. Ni mara yangu ya kwanza kukutembelea. Pole kwa kukusumbua." Iilipokuja suala la kutangamana na Joel, Alvin alimtendea kwa adabu na heshima.
"Bila shaka, hakuna tatizo. Ni heshima yetu kuwa na wewe hapa,” Nina alijibu kwa pupa huku akiwa amejawa na tabasamu.
Joel alimtazama mkewe akiwa hoi. Kisha, akasema kwa upole, “Ingia ndani ukaketi. Nje kuna baridi.” Joel na Nina walimtengenezea njia.
Kabla Lisa hajasogea, Alvin alifika kwake na macho yao yakagongana. Mara ya pili alipokutana na macho yake, haraka akatazama pembeni. Alikuwa na wasiwasi kwamba kadiri alivyomtazama kwa muda mrefu, ndivyo angehisi maumivu zaidi. Zaidi ya hayo, akili yake ilikuwa katika hali ya mkanganyiko muda huo.
Macho meusi ya Alvin yalimkazia mara baada ya kumwona. Hapo hapo, hisia kali zilimtawala kutoka chini kabisa, lakini, alificha vizuri sana hivi kwamba hakuna mtu aliyetambua. Kila mtu alimuona tu akimtazama Lisa kwa makini huku akiwa ameganda palepale.
Alipoona hivyo, Melanie aliingiwa na wivu ndani kabisa. Mara moja alishika mkono wa Alvin na kusema kwa sauti, “Bwana Kimaro, unatazama nini? Huyu ni binti wa nje wa baba yangu ambaye amefika hapa jana tu, lakini hatushiriki mama mmoja.” Maneno yake yalikuwa mazito ya dharau.
Alvin alielewa kila kitu sasa. Kwa muda mrefu alikuwa akijua kuwa Lisa ni binti wa Sheryl, lakini hakutarajia kuwa Joel ndiye mwanaume ambaye Sheryl alikutana naye hapo awali. Alifikiri kwamba asingemwona Lisa tena. Bila kutarajia alikuwa ametokea mbele yake tena wakati huo. Alikuwa hata binti wa familia mashuhuri ya Ngosha.
Hatimaye Alvin alipata utulivu, lakini akapata hisia nyingine nyingi. Wakati huu, alijawa na uchungu.
"Bwana Kimaro, huyu ni binti yangu mkubwa, Lisa." Joel alimtambulisha Lisa kwake huku akionekana kutoridhika na utambulisho ambao Melanie alitoa.
“Oh, binti yako mkubwa? Si binti yako tu wa haramu?” Kauli ya kikatili ilitoka kwenye midomo mizuri ya Alvin.
Lisa alikodoa macho. Hakutarajia kwamba Alvin angekubaliana na maelezo ambayo Melanie alisema. Kauli hiyo ilionekana kumpeleka kwenye dimbwi la kukata tamaa. Hakika, hii ndiyo ilikuwa asili ya kweli ya Alvin. Alikuwa mkatili na mwenye dharau. Nina na Melanie walishangilia kwa furaha. Hawakuwa wametarajia Alvin kuchukua upande wao.
Joel alikuwa na shida kidogo. Alvin alimtupia jicho kisha akasema kwa upole, “Kuwa na mtoto wa nje kumezingatiwa kuwa ni jambo lisilofaa katika familia ya Kimaro. Ulikuwa mzembe sana, Mr. Joel."
Joel aliipokea kauli ya Alvin kwa machungu, lakini hakuwa na ujasiri wa kujibu. Baada ya yote, familia ya Kimaro ilikuwa na hadhi ya juu sana, hivyo hakuweza kudiriki kumkosea Alvin vinginevyo angeharibu biashara zake.
Akishindwa kuvumilia tabia yake, Lisa alimwendea Alvin na kumwangalia machoni kwa namna isiyo ya jeuri wala kujidharau. "Hata kama Baba yangu alikuwa mzembe au la, haina uhusiano wowote na wewe. Baada ya yote, yeye ndiye mwenyeji wako, unatakiwa uwe na heshima kwake."
Macho ya Alvin yaligeuka kuwa mabaya, na Nina akamwambia Lisa kwa ukali. “We mwanaharamu, unawezaje kuthubutu kuongea na Bwana Kimaro kwa njia hii? Omba msamaha haraka.”
“Hasa. Bwana Kimaro alitushauri tu kwa wema. Wewe ni mkorofi sana.” Kwa hayo, Melanie aliinua kichwa chake na kumwambia Alvin, “Usikasirike, Bwana Kimaro. Lisa alikulia katika familia isiyo na uwezo na hajaona sehemu kubwa ya ulimwengu.”
Alvin alikunja midomo yake mizuri na kutoa tabasamu dogo. “Inaonekana sijakaribishwa hapa. basi nitaondoka tu…”
Dakika alipogeuka, kila mtu alianza kuingiwa na hofu. Melanie alishika mkono wake kwa nguvu na kunguruma. "Baba, mwambie Lisa aombe msamaha sasa!"
Joel alikunja ngumi. Ikiwa Alvin angetoka nje ya nyumba ya familia yake muda mfupi baada ya kuingia, watu wote wenye nguvu huko Nairobi wangejua kwamba alikuwa amewaudhi familia ya Kimaro. Katika hali hiyo, familia ya Ngosha ingetengwa huko Nairobi. “Lisa, omba msamaha."
Alipomaliza tu sentensi hiyo, alitoa tabasamu la uchungu na kuhema. Lisa akiwa ameduwaa akakunja ngumi. Hakuwahi kuchukizwa sana na sura nzuri ya Alvin hapo awali. Alishusha pumzi nzito na ndefu na kusema. “Samahani, Bwana Kimaro. Sijaona mengi ya ulimwengu na sijui jinsi ya kuishi kwa heshima katika jiji. Ninatoka mashambani, kwa hivyo natumai hautakwazika na mapungufu yangu.”
Kutoka mashambani? Alvin alicheka.
"Ingia, Bwana Kimaro." Joel alibadili mada huku akitumai Alvin angesahau tukio lile.
Alvin alipoingia ndani ya nyumba hiyo, Melanie bado alikuwa amemshikilia mkono. Hapo awali alipanga kujinasua kutoka mikononi mwake, lakini alipambana na tamaa hiyo baada ya kuona sura ya Lisa iliyochanganyikiwa. Baada ya kukaa kwenye kochi, Melanie alienda mpaka kumuegemea begani.
Lisa alisikitishwa na tukio hilo. Sehemu hiyo ilikuwa ya kipekee kwake, lakini sasa ilikuwa ya mtu mwingine. Je, mwanamume huyo alikuwa akimpenda kweli wakati huo? Angewezaje kubadilika hivyo?
“Mungu wangu, mbona umeleta zawadi nyingi za gharama? Uwepo wako unatosha, Bwana Kimaro. ” Nina alipiga kelele ghafla na kutazama mbele. Alimwona dereva wa familia ya Kimaro akibeba zawadi nyingi kuingiza ndani ya nyumba, ambazo zote zilikuwa adimu na za gharama kubwa.
Alvin akageuza kichwa chake karibu na kushangaa ghafla. Alijua uikuwa ni mpango wa Bibi Kimaro. Alitaka kumfanya aonekane kana kwamba alikuwa akitoa zawadi za harusi kwa familia ya Ngosha. Alikaa kimya kwa muda kabla ya ghafla kusema kwa tabasamu, “Ni wajibu wangu. Kwani, umemlea binti mzuri kama Melanie.”
“Bwana Kimaro…” Melanie aliguswa sana hivi kwamba macho yake yakawa mekundu. Alihisi kusukumwa, aliukandamiza mwili wake kwa nguvu kifuani mwa Alvin. Mwili wa Alvin ukawa mgumu. Hakuwa na la kusema. Je, mabinti wa familia ya Ngosha walikuwa wazi na wasio na aibu? Ilikuwa Lisa zamani na Melanie baadaye. Lisa alitazama pembeni. Hakutaka kulifikiria wala kulitazama.
“Baba, mimi ni binti wa nje ya ndoa. Nitapanda ghorofani kwani uwepo wangu humfanya Bwana Kimaro kukosa furaha.” Aligeuka na kumtaarifu Joel.
Joel alielewa kuwa ilikuwa inamkera kukaa pale. Alipokaribia kuitikia kwa kichwa, ghafla Alvin alizungumza kwa sauti ya kejeli, “Nadhani unahisi kutaka kuondoka kwa sababu huna furaha kwamba nilikulazimisha kuomba msamaha.”
“Hapana…” Lisa alifadhaika. Sasa kwa kuwa wawili hao walikuwa wameachana, kwanini alilazimika kumsemesha?
Alvin alikoroma. Baada ya hapo, aliashiria sahani ya matunda na karanga kwenye meza kwa kutumia kidevu chake. “Kwa kuwa unatoka mashambani, nina hakika unajua kazi za hali ya chini. Nenda kanimenyee matunda na karanga uniletee kwenye sahani. Melanie nami tungependa kula.”
Moyo wa Melanie ulijawa na furaha. Hakufikiri kwamba Bwana Kimaro angemjali sana. Alikuwa akimtesa Lisa kwa niaba yake, akijua kwamba anamchukia Lisa. “Lete matunda haraka. Bwana Kimaro anataka kula.”
*Sawa.” Lisa alilazimisha tabasamu. Kwa vile alitaka kumtesa, basi angemruhusu tu.
Aliinama na kuchuchumaa kuanza kumenya zabibu. Baada ya hapo, alianza kumenya karanga. Hakuwa amezowe na ilisababisha vidole vyake kuuma. Alipomenya za kutosha, aliweka kwenye sahani na kwenda kuwatengea wale wapendanao!
Kwa upande wa Melanie alimuegemea Alvin na kumlisha matunda na karanga ambazo Lisa alikuwa ametoka kumenya na kuwatengea. Lisa hakujishughulisha kutazama tukio hilo kwani aliliona kuwa la kuchukiza......ITAENDELEA.....
Unafikiri nini kitafuata hapo maana mambo ni moto mambo ni fire, lakini sina cha kusema nikuombe tuungane pamoja katika sehemu inayofuata ya mkasa huu wa kusisimua unaokwenda kwa jina la LISA.
<<<HIKI NI KITABU CHA 3 TUNAHITIMISHA LAKINI L.I.S.A. ITAENDELEA KITABU CHA 4 TUKUTANE JIOI>>>
Bila shaka unaendelea kufurahia mfululizo wa hadithi hii ya kusisimua.
