JINA LA SIMULIZI............................LISA
AUTHOR...........................JOMBA WAJO
SPONSORED BY......SIMULIZI ZA DULLY
WHATSAPP...........................0628924768
SEHEMU YA................................385-386
Sura ya: 385
Alvin alitazama kivuli chake kimyakimya kikitoweka. Ijapokuwa alijua kwa muda mrefu kwamba alikuwa na mawazo fulani juu yake, alijipa moyo kwamba mawazo hayo hayakutosha kuathiri hisia zake kwa Sarah. Lakini, kile kitu kilichotokea usiku wa jana kilikuwa kimebadilisha mtazamo wake juu ya Sarah.
Labda Sarah hakuwa mwema kama alivyowazia, na Lisa hakuwa mbaya kama alivyofikiri. Lakini bado alijiaminisha kuwa hisia zake kwa Lisa haziwezi kumpindua Saraha moyoni mwake.
Tambi ilikuwa rahisi sana kuandaa. Ndani ya dakika kumi, ilikuwa tayari kuliwa. Alvin aliifuta sahani ya tambi ndani ya dakika chache. Ilikuwa tu ni tambi ya kawaida, lakini Lisa alikuwa ameiroga na kuwa ya tamu sana. Ilionekana kana kwamba anapoona chakula cha Lisa, anakuwa na hamu nzuri kila wakati.
Baada ya kula tambi, kikombe cha maji ya moto na vipande vya tangawizi viliwekwa mbele yake pamoja na kkwangulio.
"Hutanisaidia kukwangua tangawizi na kuchanganya?" Alvin aliinua nyuso zake. Alionekana kama mtoto ambaye hakutaka kugusa chochote kwa sababu alikuwa hajisikii vizuri.
“Namba ya Sarah nipatie. Nitampigia simu na kumwambia aje akusaidie badala yake.” Lisa akatoa simu yake. Hakuwahi kukutana na mwanamume asiye na shukrani kama Alvin. “Kwa mtindo huu hata kama ungesema nikuelekeze chooni, ungeniita nikutawaze baada ya kumaliza.”
Alvin alinyanyuka kimya kimya na kukwangua tangawizi peke yake. Uso wake dhaifu na wa kupendeza ulimfanya aonekane mwenye huzuni.
Dakika ishirini baadaye, sauti ya kilio ilisikika chumbani. Lisa alikimbia mara moja. Muda si muda, Suzie aliacha kulia, na sauti ya vicheko ikasikika. Alvin alienda mlangoni na kumuona Lisa akisuka nywele za Suzie pale kitandani. Punde, Suzie alivalia kama binti wa kifalme, mzuri na mrembo.
Joto likajaa ghafla moyoni mwake. Asubuhi hii mapema ilimfanya ahisi kama walikuwa familia ya watu watatu.
Hata hivyo, katika muda mfupi tu, kengele ya mlango ililia. Hans alisimama mlangoni kwa heshima. “Bwana Mkubwa, Bi Jones kanipigia akisema kwamba hujisikii vizuri. Nitakupeleka hospitali sasa hivi.”
Uso wa Alvin ukazama. Alimtazama tena Lisa, ambaye alikuwa akitoka na Suzie. “Ulimpigia simu Hans?”
“Duh? Nina shughuli nyingi. Sina muda wa kukutunza. Isitoshe, hatuna uhusiano wowote mimi na wewe. Siwezi kukaa na mume wa mtu nyumbani kwangu, nitashikwa ugoni. Hans, mpeleke.” Lisa aliongea huku akimtengea Suzie kifungua kinywa.
Suzie alikuwa na pancakes, mayai ya kuchemsha, na juisi. Alikumbuka bakuli la tambi alilokuwa nalo. Kwa mara nyingine tena, Alvin alihisi kama hakutendewa haki kwa kupewa sahani ya tambi peke yake.
“Anko nimesikia una mafua. Unapaswa kwenda hospitali haraka." Suzie alimtazama kwa huruma. "Baba atakuja kunichukua na kunipeleka shule ya chekechea baadaye."
“Shule ya chekechea?” Alvin aliganda.
“Ndio, Aunty Lisa aliniambia jana usiku kwamba niende shule ya awali. Nitakuwa na marafiki wengi huko ili nisijisikie mpweke tena. Na sitalazimika kukunisumbua kazini wakati wa kupumzika tena.”
Suzie alikuwa na sura ya kujali. Hata hivyo, Alvin alihisi huzuni Hakuwa na wasiwasi hata kidogo na alipenda sana usumbufu wa Suzie. Ikiwa angeenda shule ya chekechea, bila shaka asingemwona kwa muda mrefu. “Suzie, hunisumbui,” Alvin alisema kwa bidii.
“Najua, lakini Anko anakaribia kuoa. Aunty Lisa alisema kuwa Aunty Sarah hatakuwa na furaha ikiwa utanisindikiza kila siku. Sitaki anichukie,” Suzie alisema bila hatia.
Alvin alimtazama Lisa kwa hasira. “Nimesema sangapi maneno hayo?” Macho mazuri ya Lisa yalimpa changamoto. “Au unafikiri Sarah hawezi kulea mtoto?”
Ikiwa ingekuwa zamani, Alvin angeweka dau kwamba Sarah hakuwa mtu wa aina hiyo, lakini sasa, hakuwa na uhakika. Alikenua meno yake kwa Lisa.
“Fanya haraka uondoke, usije ukamwambukiza Suzie mafua.” Lisa alimfukuza tena.
Alvin aliamua kujiuzulu tu kuondoka. Mara moja akiwa ndani ya gari, alitoa amri. "Nipeleke ofisini. Tayari nimekunywa tangawizi najisikia vizuri. Sihitaji kwenda hospitali.”
Hans alimtazama na hakusema kitu kingine chochote. Baada ya yote, ukiweka kando ugonjwa fulani wa akili, Bwana wake alikuwa na afya kabisa. Hakuwahi kupata homa mwaka mzima, siku hiyo ilikuwa ya kwanza.
“Oh sawa. Piga simu na mwambie Jack aje kwa kampuni mara moja. Kisha, upange jambo la dharura asipate nafasi ya kuondoka ofisini.,” Alvin alisema tena. Hakutaka kuiona sura ya upendo ya Jack, Lisa, na Suzie wakiwa pamoja.
Hans alikosa la kusema. Aliweza mara moja kukisia nia ya Bwana Mkubwa wake.
“Pia…” Alvin akaongeza tena, “Nenda ukamchunguze Erick Malugu.”
Hans hakuweza kujizuia kusema, “Bwana Mkubwa, nijuavyo mimi, familia ya Malugu ni familia ya kuheshimika sana. Erick Malugu ni mstaarabu, mwenye kipaji, mwenye tabia njema…”
“Inatosha.” Hans alikatishwa na uso mkali. “Nataka mapungufu yake. Kila mtu ana udhaifu wake, kama vile kutokuwa mwaminifu, kashfa, au kuwa na mazoea mabaya.”
Hans alikasirika. “Nilisikia hana kashfa yoyote. Erick ni mtu mungwana na mpole, huwezi kumkuta maeneo mabaya…”
“Sitaki ulichosikia. Ulichosikia kinaweza kuwa si kweli.” Alvin alimkumbusha. “Kuna vitu vingine vinavyoweza kumfanya aonekane hafai. Kwa mfano, miguu yake inanuka? Au mdomo wake unanuka? Labda hana nguvu za kiume, au ana sifa za kishoga. Yoyote kati ya hayo yatafaa.”
“… Vizuri sana.” Hans alishtuka kwa aibu. Alielewa kuwa Alvin alikuwa akijaribu tu kuweka kabari kati ya Erick na Lisa. Hans hakujua ni nini Alvin anataka. Alikuwa karibu kuoa hivi karibuni, lakini bado alikuwa akimdhibiti mke wake wa zamani.
Wakati Alvin anaingia ofisini, Sarah alikuwa amekaa kwenye sofa kwa muda mrefu. Alipomwona, mara moja aliuliza kwa wasiwasi, “Suzie yuko wapi? Yuko sawa?”
Alvin aliinua macho yake kumtazama. Sasa kwa vile alikuwa hajisikii vizuri, alichokuwa akitaka ni amani na utulivu. Hata hivyo, sura ya Sara ilikuwa imevuruga tena akili yake.
“Sarah, niambie. Suzie alianguka vipi jana usiku?” Alvin aliuliza ghafla.
Moyo wa Sarah ulitetemeka, akakosa raha baada ya kuona uso wa Alvin ukiwa umekufa. Hakujua kama Suzie alikuwa amemweleza juu ya kile kilichotokea jana yake usiku.
Alipomuona akiwa kimya, uso mzuri wa Alvin ulizidi kuwa mweusi zaidi. "Je! ni ngumu kujibu swali langu?"
“Ulielewa vibaya. Nilihisi tu kwamba ninawajibika kujua hali yake kwa kuwa alianguka nikiwa naye.” Sarah aliuma midomo yake na kusema bila kufafanua, “Ni kosa langu. Ikiwa ningekuwa mwangalifu na mvumilivu zaidi, labda asingeanguka. Samahani."
Alvin alimkazia macho. Ikiwa ingekuwa zamani, angeweza kuchagua kumfariji bila masharti. Hata hivyo, kilio cha Suzie usiku wa kuamkia jana kilimfanya awe na akili timamu na kutambua kwamba ingawa Sarah alijilaumu, lakini sababu zilizomfanya Suzie aanguke hazikuwa wazi.
Ilikuwa ni kama… Suzie hakuanguka kwa sababu Sarah alikuwa mzembe. Ilikuwa ni kwa sababu Sarah alikuwa na wasiwasi kuhusu kulowanisha na kuchafua nguo zake, hivyo akamsukuma Suzie chini.
"Sarah, hupendi watoto?" Aliuliza ghafla.
Sarah alishtuka, lakini alijaribu kudumisha tabasamu usoni mwake. “Bila shaka nawapenda. Watoto hawana hatia na wanapendeza, kama malaika wadogo. Nawapenda sana.”
Sura ya: 386
Alvin akainua midomo yake. Sarah alimshika mkono na kushusha macho yake. “Alvin, najua kosa langu la jana usiku lilikukera sana, lakini ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kumshika mtoto, kwa hiyo nilishindwa. Ninaahidi sitafanya tena katika siku zijazo. Unaweza kumletea Suzie mara nyingi zaidi kucheza wakati ujao, na ninaweza kufanya mazoezi zaidi kuhusu jinsi ya kutunza watoto.”
“Mazoezi? Unataka ufanye mazoezi kwa Suzie” Alvin alikunja uso. “Yeye ni mtoto mdogo tu. Ulifanya uzembe kidogo tu ukamjeruhi. Hata mfupa wa samaki tu ulishindwa kutoa ukampalia. Unataka umfanyie mazoezi ili umuue kabisa?”
Akiwa na uso uliopauka, Sarah alieleza upesi, “Hilo silo nililomaanisha. Nitakuwa makini sana. Sitaruhusu jambo kama hilo litokee…”
“Sarah, sidhani kama unafaa kuwa na mtoto kwa sasa.” Alvin akamkatisha ghafla.
“Kwanini? Kwa sababu tu sikumtunza Suzie vizuri jana?” Sarah alikuwa na wasiwasi sana hivi kwamba alikaribia kulia. “Alvin, huoni kuwa hivi karibuni umekuwa na upendeleo? Yeye ni mtoto wa Jack, sio wako. Ndiyo, nakiri kwamba sikufanya kazi nzuri, lakini huwezi kuninyang’anya haki yangu ya kuwa mama. Nina hakika nitakuwa makini sana na mtoto wangu mwenyewe.”
"Sarah, kwanini ulimtishia mtoto kuhusu kuharibu uhusiano wangu na wewe?" Alvin alikuwa tayari hajisikii vizuri, hivyo Sarah alipoanza kulia, alipasuka kwa hasira moja kwa moja. “Kwa sababu yeye si mtoto wangu, ulimwambia kuwa mimi na baba yake hatuelewani na kwamba yeye ni mimi nitabaki kuwa Anko wake tu. Ulisema kwamba akiharibu uhusiano wetu, utanifanya nisimpende nikiwa na mtoto siku za usoni.”
Sarah alipigwa na butwaa. Alifikiri kwamba ukimya wa hofu wa Suzie jana yake baada ya kumtishia ulimaanisha kwamba tishio lake lilifanikiwa. Baada ya yote, Suzie alikuwa bado mdogo sana. Ustadi wa kuzungumza wa watoto wengi katika umri huo usingekuwa mkubwa kiasi hicho, Suzie alikuwa na ubongo gani? Hata hivyo, yule mtoto mnyonge aligeuka na kumwambia Alvin.
Alvin alimshutumu, “Ulimsukuma chini kwa sababu tu amelowanisha nguo zako. Muda wote, alikuwa anaoga peke yake huku wewe ukicheza na simu yako. Sarah, huna huruma. Hupendi watoto hata kidogo. Huna upendo."
Tofauti na Lisa, ambaye angepika kifungua kinywa chenye lishe na vitafunwa kwa mtoto, na pia kuchana nywele zake na kumpigisha mswaki, na hakuthubutu hata kufunga mlango wa bafu alipokuwa anaoga kwa sababu alikuwa na wasiwasi na mtoto, Sarah alikuwa hafai kuwa mama. Kadiri alivyokuwa akiwalinganisha ndivyo alivyohisi Lisa alikuwa bora zaidi.
Wakati fulani, alitaka hata kumuacha Sarah awatunze mapacha wa Lisa, akifikiri Sarah angewatunza vizuri. Lakini, ukweli ni kwamba alimtishia mtoto ambaye alikuwa na umri wa miaka mitatu tu. Vipi kuhusu watoto wadogo basi? Hakuthubutu kufikiria juu yake.
Midomo ya Sarah ilitetemeka. Kwa muda wa miaka mitatu kuelekea minne aliyokaa naye, ndiyo kwanza Alvin alimtazama kwa kukata tamaa na hasira machoni mwake.
Wimbi la wasiwasi likatawala juu yake. Sarah alibubujikwa na machozi ya hatia. " Samahani. Sikuweza kujizuia, na sikumaanisha. Jana, wakati nikimuogesha Suzie, wakati mmoja alisema maji ya baridi, na nilipoongeza joto akasema ya moto sana. Nilihisi ananifanyia usumbufu wa makusudi,kwa hivyo nikakosa subira kwake.
“Ndio maana nilisema maneno yale kumtishia. Lakini hiyo ni kwa sababu niliona kwamba baadhi ya kina mama huwatia adabu watoto wao namna hiyo. Sikumaanisha ubaya wowote. Nilihisi tu kama Suzie hanipendi.”
"Lakini unapaswa kukumbuka kuwa Suzie amempoteza mama yake."
Alvin hakuweza kuwa na wasiwasi wa kubishana naye tena. “Kwa vyovyote vile, watoto si mbwa au paka. Ikiwa unaamua kuwazaa, unapaswa kuwatunza vizuri. Mambo mengi lazima yafanywe na wewe mwenyewe. Huwezi kutegemea yaya kwa kila kitu. Baada ya yote, yaya hakumzaa mtoto. Utajuaje kama yaya atakuwa mwema kwake?"
Kama yeye tu. Alikuwa akinyanyaswa na yaya wake. Kwa hiyo, Alvin alitaka kuhakikisha kwamba watoto wake wanakua wakizungukwa na upendo wa wazazi.
“Nitafanya. Nitawatunza watoto wetu vizuri,” Sarah alisema huku machozi yakimtoka.
“Sarah, siwezi kukuamini. Nadhani sisi bado ni vijana. Hebu tusahau kwanza kuhusu kupata watoto sasa hivi. Tutapanga tena kuhusu hilo wakati fulani baadaye. ” Alvin kisha akatazama pembeni. “Unaweza kuondoka sasa. Bado nina mambo mengi ya kushughulikia. Vilevile, huna haja ya kuandaa chakula changu cha mchana na kuleta tena. Nataka uwe na kazi ya kufanya badala ya kutumia maisha yako kunizingatia mimi tu.” Alipomaliza kuongea, alikaa kwenye kiti cha ofisi na kuanza kufanya kazi.
Sarah alikasirika sana hivi kwamba alikaribia kupatwa na wazimu.
Hata hivyo, alichoweza kufanya ni kuigiza sura ya uchungu wakati akitoka nje ya ofisi ya Alvin. Hakuwahi kutarajia kuwa ndoa yake aliyoifanyia kazi kwa bidii sana ingeishia kuchafuliwa na mtoto badala ya Lisa.
Alipofika tu kwenye maegesho ya magari, Hisan Gadaffi alimpigia Sara."Nihamishie shilingi milioni 100 sasa hivi. Nina ukata wa pesa taslimu.”
Sarah akaruka kwa hasira. “Nimekupa pesa nyingi sana muda si mrefu uliopita. Unanichukulia kama mashine ya kuchapisha pesa? Unajua jinsi ilivyo ngumu kupata shilingi milioni 100?"
"Ni vigumu kupata kiasi hicho, lakini si kazi kwa Alvin." Hisan alisema bila kujali, “utaolewa na mwanamume tajiri zaidi nchini Kenya hivi karibuni. Nusu ya mali yake itakuwa yako.”
Maneno yake yaliifanya damu ya Sarah kuchemka. "Hiyo ni sawa. Lakini atashtuka ikiwa nitaendelea kutumia mamia ya mamilioni ya shilingi kwenye kadi yake.”
"Sema tu kwamba unanunua vitu," Hisan Gadaffi alijibu kwa kukosa subira. "Harakisha! Kwa kweli nimekaribia kukata tamaa.”
“Tafadhali, Hisan. Huwezi kutumia pesa vizuri? Usifikiri kuwa sijui unaitumia kwa kucheza kamari, kunywa pombe na kuwagonga wanawake. Niligundua kuwa umeleta wanawake kwenye ghorofa langu mara kadhaa. Bora usiambukizwe.”
“Nyamaza na uchunge mdomo wako. Ninaweza kukutegemea wewe kunitimizia mahitaji yangu ikiwa sitaleta wanawake ndani? Unafurahia maisha yako na Alvin, mimi je, huh? Ukinivuruga nitaliamsha dude,mapema au baadaye!”
Sarah alihisi kana kwamba anapigwa kofi usoni. Muda mfupi baadaye, alishusha macho yake. "Sawa, nitakupa pesa."
Baada ya kukata simu, macho yake yalimtoka kwa hasira na kuapa kumuua. Ilimbidi ajiondoe kwa Hisan. Baada ya hayo, taratibu akatoa simu yake na kupiga namba fulani…
•••
Muda mfupi baada ya Suzie kumaliza kifungua kinywa chake, Lisa alipokea simu kutoka kwa Jack. “Lisa, siwezi kufika. Nilikuwa nimekaribia kufika kwako Alvin akaniambia nirudi ofisini maana kuna kitu cha dharura kimetokea. Nilifanya haraka kurudi, nikakabidhiwa rundo la nyaraka za kufanyia kazi. Ishu ni kwamba hataniruhusu nitoke hadi nilimalize kuhakiki nyaraka zote. Ni wazi alikuwa anajaribu kunizuia nisikuone. Ni mtu wa vitimbi sana."
Lisa alishikwa na neno ghafla. “Ni sawa. Nitampeleka Suzie mwenyewe shule ya chekechea.”
"Endelea. Nimezungumza na mkuu wa shule mapema,” Jack alisema kwa hasira. “Nitamchukua Suzie jioni.”
“Sawa.”
Lisa basi alimpeleka Suzie kwenye shule ya mapema. Suzie alikuwa katika darasa moja na Lucas. Hata mwalimu wa shule ya awali alikuwa hajui kuwa Suzie na Lucas ni mapacha, kwani Lisa alitaja tu kuwa walikuwa marafiki wakubwa......ITAENDELEA.....
Unafikiri nini kitafuata hapo, maana simulizi inazidi kuwa tamu kila siku lakini sina budi kuhitimisha kipande hiki ila niwasihi tukutane katika episode zijazo ili kujua nini kitafuata kwenye mkasa huu wa kusisimua na kuelimisha unaokwenda kwa jina la LISA.
