JINA LA SIMULIZI............................LISA
AUTHOR...........................JOMBA WAJO
SPONSORED BY......SIMULIZI ZA DULLY
WHATSAPP...........................0628924768
SEHEMU YA................................377-378

Sura ya: 377

Saa saba mchana, Alvin kwa mara nyingine tena aliingia kwenye ofisi za Mawenzi Investments. Hata hivyo, mlinzi katika maegesho ya chini ya ardhi hakuruhusu gari lake kuingia baada ya kusikia maagizo ya Lisa.
Hapo kulikuwa na lifti ya VIP ya kuingilia moja kwa moja kwenye ofisi ya Lisa. Angeweza tu kuingia kupitia lango kuu la kuingilia ndani ya kampuni hiyo.

Mhudumu wa mapokezi alipomuona Alvin akiwa amemshika mtoto wa miaka mitatu na kitu ambaye alikuwa akitema picha yake, alipigwa na butwaa kabisa. Walinzi waliokuwa mlangoni nao walizidiwa nguvu, kila mmoja akaanza kuongea kwa minong'ono.

“Ee Mungu wangu, huyo ni binti wa Bwana Kimaro?”

“Bila shaka. Lazima atakuwa binti yake wa kumzaa.”
“Lini ghafla amepata binti mkubwa kiasi hicho? Anaonekana ana zaidi ya miaka mitatu. Mama yake anaweza kuwa Bosi wetu? Ninahisi kama anafanana kidogo na Bi Jones.”

“Inawezekana sana.”

Hakuna aliyethubutu kumzuia Alvin, akatembea bila kipingamizi mpaka kwenye ofisi ya Lisa. Lisa alikuwa akikutana na wasimamizi kadhaa wa idara wakati Alvin alipoingia ghafla na Suzie mikononi mwake.

Siyo wasimamizi kadhaa wa idara tu ambao walipata hofu, lakini hata Lisa alihisi roho yake ikikaribia kuondoka kwenye mwili wake.
“Mwenyekiti Jones, huyu ni… mtoto wako na Bwana Kimaro? ” Meneja mmoja aliuliza kwa tahadhari.

Lisa alikuwa njia panda. Je, angeweza kukataa? Je, Suzie alikuwa amefichuliwa ndani ya siku mbili tu?

Hapo hapo, Suzie alimtazama na kuita kwa upole, “Anti Lisa, nilikukumbuka sana.”

Nini? Ubongo wa Lisa haukuweza kupata mawazo ya haraka ya Suzie.

“Yeye ni binti wa mdogo wangu.” Alvin aliwakazia macho wasimamizi. “Samahani, lakini naomba mtoke nje kwa muda. Nahitaji kuzungumza na mwenyekiti wenu.”

"Ndiyo ndiyo."

Nguvu ya kutisha ya Alvin iliwafanya wasimamizi kuogopa sana nusura ya kushindwa kupumua. Waliondoka haraka mahali hapo na kuwaacha.
Mara moja, ofisi ilikuwa kimya.

Suzie alikumbatia shingo ya Lisa na kusema, “Mimi ghafla nimekumbuka chakula cha Mama. Baba alinileta nijaribu chakula chako siku moja na kilikuwa kitamu. Kina ladha nzuri kama alichopika Mama, kwa hiyo nikamwomba Anko Alvin aniletee kwako.” Kisha, alimkonyeza Lisa kwa siri.
Lisa alihisi kichwani kikiwa kimekufa ganzi. Alitoka kuwa mama hadi kuwa Aunty. Ikiwa Alvin asingekuwa karibu, angekuwa amemfinya tayari.
Haya yote yalihusu nini? Lakini alielewa ujanja wa Suzie.

Lisa hakujibu, uso mzuri wa Alvin ulizama na kusema, “Umesikia alichosema Suzie? Msichana anataka kula kchakula chako."

"Hapana, lakini kwanini mko pamoja?" Lisa alijipapasa na kujiambia atulie na awe na akili timamu. “Yeye si binti wa Jack?”

"Kwa hivyo tayari unajua kuwa Jack ana binti?" Sauti ya Alvin ilibeba uchungu ambao hata hakuufahamu. Hakukasirika kwa kuwa Lisa hakumwambia kuhusu hilo, bali kwa sababu alikuwa karibu sana na Jack japokuwa tayari alijua kuwa ana mtoto wa kike.

"Niligundua hivi karibuni." Lisa hakuweza kuhangaika naye akamsogelea Suzie kumchukua. "Unataka kula nini?"

"Nyama ya nguruwe choma, na samaki wa kuoka."

Lisa alijihisi jasho. Hamu yake ya kula na ladha yake ya chakula ilifanana kabisa na ya mtu fulani. “Sawa, twende tukanunue sasa, sivyo?”

Kwa kuwa binti yake kipenzi alitaka kula chakula chake, kwa kawaida Lisa ilimbidi aweke kazi pembeni na kwenda kumhudumia. Alivaa koti dogo la suti na kumuongoza Suzie nje. Hakuwa amemtazama Alvin tangu mwanzo hadi mwisho.

Alvin aliyepewa bega baridi alikunja uso na kuwafuata. “Unapikia wapi?”

"Nyumbani, bila shaka. Siwezi kupika hapa. Lazima niende dukani kwanza." Lisa alimtazama tena kwa unyonge. "Rudi tu ofisini kwako.
Nitamjulisha Jack aje kumchukua baadaye.”
"Hakuna haja. Nimemleta Suzie hapa, kwa hiyo nitamrudisha mwenyewe.” Alvin aliweka mikono mfukoni na kutembea kando yake, akionekana kupoa na kupendeza.

Wakati wote watatu wakipita kwenye korido, wafanyakazi wote wakawatazama.

“Si Bwana Kimaro anaoa? Kwanini bado anakuja kumuona Mwenyekiti Jones?”

“Huoni? Wana mtoto pamoja. Maadamu wana mtoto, wawili hao hawawezi kuvunja uhusiano. ”

“Msichana huyo kwa kweli anafanana na Alvin Kimaro. Hakika ni binti yake wa kumzaa.”

Kadiri Lisa alivyokuwa akisikiliza maneno yao, ndivyo mazungumzo yao yalivyozidi kuongezeka.

Alvin aliposikia sauti za wafanyakazi hao, bila kujijua alimtazama Lisa. Alimshika Suzie huku Suzie akiikumbatia shingo yake. Walionekana tu kama jozi ya upendo ya baba, mama na binti.

Alvin alipoteza mawazo kwa muda. Ikiwa watoto wao wangekuwa hai, labda kile ambacho wafanyikazi walisema kingekuwa kweli. Angeweza kusema kwamba bila shaka angekuwa mama mzuri.

Katika maegesho, Lisa alifungua gari lake, lakini Alvin aliwahikwenye mlango wa dereva. “Nitaendesha gari. Uketi naye kwenye kiti cha nyuma."

“Wacha Anko aendeshe,” Suzie alisema haraka. Lisa hakuwa na jinsi zaidi ya kumpa funguo Alvin.

Alvin akawasha gari kwa kasi. Kupitia kioo cha nyuma, alimwona Suzie akiwa amekumbatiana na Lisa.
Kwa muda, alihisi kama watatu hao walikuwa familia na alikuwa akimpeleka mke wake na mtoto wake kwenda kufanya manunuzi. Hisia hiyo haikumchukiza. Kinyume chake, alihisi kwamba kifua chake kilijaa hadi ukingoni.

Katika kiti cha nyuma, Lisa alimnong’oneza Suzie sikioni, “Wewe mpuuzi mdogo. Huogopi kugunduliwa?”

"Siwezi, mama. Wote wanaamini kwamba mimi ni binti wa Anko Jack,” Suzie alisema kwa upole, “Mwanamke yule katili alienda kwenye kampuni kumtafuta baba yangu mchafu asubuhi. Simpendi hivyo nikamdanganya atoke nje. Mama, nakusaidia kulipa kisasi."

Lisa hakujua acheke au alie, lakini moyoni mwake kulikuwa na utamu.
Binti yake mwenye akili za haraka alikuwa na akili kweli. “Sawa. Kaa mbali na huyo mwanamke. Bado wewe ni mdogo, kwa hivyo hujui jinsi watu wanaweza kuwa wa kutisha. Mama hataki kukupoteza.”

“Sawa. Baba mchafu ananipenda sana. Hakika nitamfanya anipende zaidi ya yule mwanamke mbaya,” Suzie alisema kwa kujiamini.

Lisa alimtazama kwa umakini. "Suzie, unampenda Alvin?"

“Yuko sawa. Yeye ni mzuri, kwa hivyo yeye sio mtu mbaya." Macho ya Suzie yalikuwa yanametameta alipozungumza. Ilikuwa wazi kwamba alimpenda.

Naam, ilikuwa wazi binti yake alikuwa amemfuata linapokuja suala la ladha yake kwa wanaume. Alijali uso wa mwanaume tu na si kingine. Angepaswa kumsomesha Suzie baadaye.

Katika maduka makubwa, Lisa alichukua toroli na kumbeba Suzie ili akae humo. Hata hivyo, Suzie alikuwa mzito sana na hakuweza kumwinua juu vya kutosha. Kisha, Alvin akaja na kunyoosha mkono kumshika Suzie kwa nguvu, na kumweka kwa urahisi kwenye toroli.
Aliutazama mkono wake, na Alvin akatabasamu kidogo alipomtazama. "Wanaume wana nguvu zaidi."

Lisa alitabasamu. “Ndiyo, una nguvu kuliko mimi. Vinginevyo, nisingesukumwa chini na wewe na kupoteza watoto wangu.”

Tabasamu kwenye pembe za mdomo wake likatoweka taratibu. Alijua kwamba alikuwa akizungumza miaka mitatu iliyopita. Alipomsukuma chini, aliishia kupoteza watoto. Uso wa Alvin mara moja ukageuka kwa huzuni.

Suzie aliuliza bila hatia, “Anko, kwa nini ulimsukuma Aunty Lisa? Ulikuwa unamjua kabla ya hii?"

“Lo, hatukujuana tu. Tulikuwa… tumezoeana sana,” Lisa alisema kwa kumaanisha.

“Oh, ninaelewa. Mlikuwa kwenye mapenzi,” ghafla Suzie alisema kwa kutambua. Lisa akaduwaa.

Alvin hakuthubutu kuendelea na mazungumzo hayo akatazama huku na huko ili kubadilisha mada. “Nyama za nguruwe ziko wapi?”

"Kuna chokoleti! Nataka kuinunua.” Suzie ghafla alielekeza mbele.

"Hapana. Meno yako yataoza.” Lisa alikataa mara moja.

"Anko, nataka kula chokoleti. ” Suzie alifoka na kuanza kudeka kwa Alvin.

“Sawa. Ni sawa ikiwa unakula mara moja kwa wakati. ” Alvin alimruhusu bila masharti.

Lisa alihisi kichwa kinamuuma. Suzie angeharibiwa uozo huo. Baada ya kununua viungo, wote watatu walirudi Karen Estate. Alvin alipoingia ndani aliona samani zote za ndani zimebadilika. TV, kiyoyozi, sofa, jokofu, na hata vitu vya jikoni vilibadilishwa.
Alijua kwamba Thomas Njau alikuwa ameivunja nyumba yake, lakini hakutarajia uharibifu kuwa mkubwa sana. "Je, ... samani zote zilibadilishwa?"

“Si unaona mwenyewe? Hata Ukuta ulihitaji kubadilishwa rangi. Kila kitu kiliharibiwa kabisa. ” Lisa alimtazama kwa hasira.

Alvin alinyamaza kwa muda kabla ya kutoa kadi ya benki mfukoni na kumkabidhi. “Iligharimu kiasi gani? Nitakufidia.”

Alifikiri kwamba Lisa angeweza kukataa, lakini bila kutarajia, alichukua bila neno. “Unapaswa kutufidia,” Lisa alisema kwa upole, “alikwepa jela, lakini hakulazimika kulipa hata senti moja. Kwa kweli unapaswa kuzungumza na familia ya Njau. Huku sio kuomba msamaha wa dhati.”

Sura ya: 378

Lisa alipeleka vyakula jikoni kupika. Suzie alikaa kwenye sofa na kutazama Tv. Baada ta muda, harufu nzuri ilitoka jikoni. Alvin alikuwa hajala chakula cha mchana, hivyo tumbo lake lililalamika kwa kusikia harufu ile ya kuvutia.

Dakika 40 baadaye, Lisa alitoa chakula jikoni na kuweka mezani. Alvin alitazama nyama ya nguruwe iliyochomwa, ndizi, samaki wa kuchomwa, kachumbari na madikodiko mengine pale mezani, na akajikuta anapata hamu ya kula kwa njia isiyoelezeka.

Lisa alimpa Suzie sehemu yake. Alvin hakutarajia kuhudumiwa, hivyo akaenda kujitafutia sahani. Hata hivyo, alipokuja, hakukuwa na kitu chochote kwenye mabakuli. Vyote vilikuwa vimeishia kwenye sahani za Suzie na Lisa

"Lisa, chakula changu kiko wapi?" Macho yake yalimtoka.
“Kwani ulisema unataka kula? Isitoshe, nilikubali kumpikia Suzie tu, sio wewe. Tayari ni saa tisa mchana na bado hujala, Bwana Kimaro?”

Alvin akauma mdomo. “Tumeambata wote mjini mjini mchana huu kukua chakula. Ningepata wakati gani wa kula?”

“Lo! Ikiwa una njaa, unaweza kwenda kumtafuta Sarah. Siwajibiki kwako.” Lisa alimsaidia Suzie kupata vipande bora zaidi vya nyama ya nguruwe choma na kuchambua mifupa kutoka kwenye samaki kabla ya kumpa. Mashavu ya Suzie yalikuwa yamejaa wakati akila, akionekana kama nguruwe mdogo.

“Anko Alvin ameacha chakula tele ofisini alicholetewa na mchumba wake.” Suzie akapasua jipu. “Hana hata njaa. Kama ana njaa ataenda kula chakula chake kibaya.”

“Umesikia?” Lisa alicheka. “Umeacha chakula cha mkeo huko halafu unakuja kudowea chakula cha mtoto.”



Baada ya kumeza chakula, Suzie alisema huku akimtazama Alvin kwa jicho la pembeni kana kwamba anamrusha roho. “Upishi wako ni mzuri sana, Mama.”

Alvin aliyebaki ameduwaa na sahani yake kubwa mkononi, alimeza mate ya uchu. Alijua chakula hicho kilikuwa kitamu, hivyo alitaka kukila pia.
Ni kana kwamba Suzie alikuwa akisikia mawazo ya ndani ya Alvin. Kwa huruma alimpa kipande cha nyama ya nguruwe. “Hebu onja kidogo Anko Alvin mapishi ya Aunty yangu.”

Alvin alikipokea kipande kile na kukitupia mdomoni fasta. Kilikuwa kitamu sana! Angeweza kula chote peke yake kama angeachiwa. Hata hivyo, Suzie alimpuuza baada ya kumpa kipande kimoja tu. Lakini hakumzuia kula. Angeweza tu kutumia uma kuchukua chakula mwenyewe.

Lisa hakuwa amepika chakula kingi, na baba na binti yake walikuwa waroho kweli kwenye nyama. Kwa muda mfupi, nyama ya nguruwe iliyochomwa ilikuwa karibu kumaliza.

Suzie alishika bakuli na kusema kwa huzuni, “Anko, umetosha. Zimebaki nyama zangu mimi bado sijashiba.”

Alvin alipokitazama kile chakula kitamu kikiingia mdomoni mwa Suzie, tumbo lake lilizidi kumkosesha raha. Alitamani ampokonye.

Lisa alisafisha meza na kumpa Suzie mtindi uliotiwa strawberry ili ashushie chakula chake. Suzie alikunywa kikombe kikubwa kwa kuridhika na kushukuru, "Maziwa ni matamu, Mama."

Mikono ya Lisa ilitetemeka. Ilikuwa ni mara ya pili sasa Suzie anajisahau na kumuita Lisa ‘Mama’.

Alvin alimtazama Suzie kwa mshangao. "Umemwitaje?"

Suzie nusura akose cha kujitetea. Lakini kwa haraka akarekebisha mambo na kusema, “chakula cha Aunty Lisa ni kitamu kama cha mama yangu, ndiyo maana najisikia kama nipo na mama. Aunty Lisa, si baba atakuoa ukuwe mama yangu, seti eeh?”

Lisa alichoka kwa uwezo wa kuigiza wa bintiye na kwa upole akampigapiga kichwa chake. "Ukipenda nitakuwa."

Alvin kidogo atapike nyama zote alivyosikia hivyo. Lisa awe mke wa Jack?

“Nataka ukuwe mama yangu.” Upesi Suzie aliitikia kwa kichwa na kupepesa macho kwa nguvu na kusababisha machozi kumdondoka. “Kila ninapokula chakula chako, Aunty, namfikiria Mama. Sasa hivi, nilikufikiria kama mama yangu.” Kisha, ghafla akaruka mikononi mwa Lisa. "Aunty, unaweza kuwa mama yangu?"
Umahiri wa malkia yule mdogo wa maigizo ulikuwa ukiongezeka haraka sana. Hata Lisa, aliyejiita gwiji wa kuigiza, hakuweza kuendana na mdundo wa bintiye. Ilikuwa ni huruma kwamba msichana huyu hakuwa tasnia ya uigizaji. Kwa kweli angeweza kucheza kama nyota wa watoto.

Kabla hajajibu, sura ya Alvin ikabadilika na kusema kwa sauti ya hasira. "Hapana."

Suzie alimtazama na kuogopa sana hadi akajizika mikononi mwa Lisa. Alianza kulia. "Anko anatisha sana."

"Mbona unakuwa mkali sana kwa mtoto?" Lisa alimtazama kwa hasira.

Alvin hakuwa na nia ya kumtisha Suzie, lakini wazo tu la Lisa kuolewa na Jack liliufanya moyo wake ukose raha bila hiari yake. "Suzie, samahani." Haraka haraka akaomba msamaha kwa sauti ya chini. “Lakini wewe bado ni mdogo, kwa hiyo kuna baadhi ya mambo huelewi.
Aunty Lisa hawezi kuolewa na baba yako.”

"Kwanini isiwe hivyo? sielewi.” Suzie alijifanya kutojua. “Baba hajaoa, na Aunty Lisa pia hajaolewa. Kwanini wasioane?”

“We mtoto, nimesema haiwezekani, husikii? ” Alvin alizidiwa na hasira na kukataa kabisa. “Aunty Lisa ni mke wangu wa zamani kwa hivyo hawezi kuolewa na baba yako. Babu na babi zako hawatakubali.”

“Oh.” Suzie alifikiria jambo hilo kwa uzito. “Sasa kwa nini usimuoe Aunty Lisa, Anko? Kwa njia hiyo, Aunty Lisa pia atakuwa mtu wa familia yangu.”

Baada ya maneno yake kuanguka, sebule ikawa na kimya cha ajabu.
Alvin alimtazama Lisa kwa mshangao.

Lisa aliinamisha kichwa chake na kuweka banio la nywele nyuma ya masikio yake, akionyesha wasifu wake mzuri na wa upole. “Hatuwezi,” alisema kwa upole. "Tulifunga ndoa hapo awali, lakini tuliachana kwa sababu tulishindwana. Anko wako ataoa hivi karibuni pia. Atakuwa na mke mpendwa, kwa hiyo lazima ukubali hilo.”
“Oh, nakumbuka sasa. Atakuwa ni yule Aunty nilimwona asubuhi. ” Suzie ghafla akampa Alvin sura ya kufurahi. “Anko, wewe una hasara sana. Chakula cha mkeo si kizuri, sitakuja kwako, lakini ninaweza kuja kwa Aunty Lisa wakati wowote nikitaka kula chakula kitamu.”

Alvin alihisi kama amepooza tena, na maneno yale yalimkosesha raha sana. Hakuwa amefikiria hivyo hapo awali, lakini kwa wakati huo aligundua kwamba alipendelea kutumia muda wake mwingi na Lisa badala yake.

Wawili hao walikuwa wameendana vizuri walipoambatana na Suzie kwenye supermarket. Ikiwa wangekuwa familia ya watu watatu, wangeweza kula vyakula vitamu vilivyopikwa na Lisa na mara kwa mara kwenda kwenye uwanja wa michezo pamoja. Hiyo ilikuwa imekaa vizuri sana.

Hata hivyo, alielewa kwamba tayari alikuwa ameamua kumuoa Sarah. Hakukuwa na kurudi nyuma kwa mambo mengi.

“Sawa, unapaswa kuondoka sasa. Tayari nimempigia simu Jack. Atakuja kumchukua Suzie baadaye.” Lisa alimfukuza Alvin. “Haikuwa rahisi kumaliza kukarabati nyumba hii. Sitaki Thomas Njau anikodishie tena watu wa kuharibu mahali hapa ikiwa familia ya Njau itagundua kuwa uko hapa.”

Alvin alikasirika. “Hakuna haja, nitaondoka na Suzie. Hujui kutunza watoto hata kidogo, kwa hiyo sikuamini kuwa utaitunza vyema hazina ndogo ya familia yetu ya Kimaro."

"Sijui kutunza watoto?" Lisa alidhani amesikia mzaha. Alikuwa peke yake akilea watoto wawili. Mpaka hapo anamwona Suzie, ni yeye ndiye aliyemlea.

“Nimesema kitu kibaya?” Alvin aliuliza kwa jeuri.

"Sawa, kila kitu unachosema ni sawa. Nendeni sasa.” Lisa akawafukuza. “Nina jambo la kufanya baadaye.”
“Anti Lisa nitamwambia baba kesho aniletee kwako tena. ” Suzie alipunga mkono. Ingawa hakutaka kuondoka upande wa mama yake, ikiwa angesisitiza kukaa kwa muda mrefu, baba yake mchafu angetilia shaka.

Alvin alimbeba Suzie pale chini na kuchuchumaa huku akimwambia kwa umakini, “Suzie, huwezi kuendelea kumwambia baba yako akulete kwa Aunty Lisa.”

"Kwa nini isiwe hivyo?" Suzie alikasirika mara moja. “Anko, kama ningejua mapema nisingekuomba uniletee kwa shangazi. Ninampenda sana, lakini huniruhusu kukutana naye.”.......ITAENDELEA....

Unafikiri nini kitafuata hapo, maana simulizi inazidi kuwa tamu kila siku lakini sina budi kuhitimisha kipande hiki ila niwasihi tukutane katika episode zijazo ili kujua nini kitafuata kwenye mkasa huu wa kusisimua na kuelimisha unaokwenda kwa jina la LISA.