JINA LA SIMULIZI............................LISA
AUTHOR...........................JOMBA WAJO
SPONSORED BY......SIMULIZI ZA DULLY
WHATSAPP..........................0628924768
SEHEMU YA................................287-288

Sura ya: 287

“Nilifikiria kuhusu hilo pia. Lakini hakujitapa kuhusu hilo mara ya mwisho alipokuja kwa hivyo sifikirii hivyo.” Charity akatingisha kichwa huku sura ngumu ikitawala uso wake. "Alisema alitaka kumchukua Alvin wake na kurudisha wadhifa wa Bi Kimaro. Unapaswa kuwa mwangalifu dhidi yake.”
Lisa alishtuka. Ilionekana kuwa mawazo yake yalikuwa sawa. “Kweli? Lakini hasemi hivyo mbele ya Alvin na marafiki zake.”
"Siku zote amekuwa kama kinyonga." Midomo ya Charity ilitetemeka. "Amewateka wote Alvin na genge lake, wanamchukulia kama binti wa kifalme."
Lisa alicheka. “Najua. Hivi ulijua kabla ya hii kwamba Sara hakuwa amekufa? Hata akawa mwanasaikolojia maarufu, Nyasia. Yeye ndiye anayemtibu Alvin kwa sasa.”
Charity alionekana kushtuka kweli. “Nilifikiri kweli amekufa. Miaka kadhaa iliyopita, alikuwa anafanya utafiti wake kwenye msitu wa Garisa baada ya kuhitimu masomo yake nje ya nchi. Alitekwa nyara na magaidi wa Al-Shabaab alipoenda msituni na marafiki zake. Magaidi hao waliwageuza kuwa wako zao wakawa wanawabaka kila siku. Lakini alifanikiwa kutoroka kwenye kambi ya magaidi huko Somalia na kuzamia Ulaya.”
“Kwanini hakuwasiliana na familia yake au hata Alvin? Badala yake, aliishi kwa siri na kuwa mwanasaikolojia maarufu.” Lisa aliuliza.
“Kuna kitu hakiko sawa kuhusu hili.” Charity naye hakuweza kuelewa.
Lisa alijiuliza mambo mengi sana baada ya kusikia kisa cha kutoweka kwa Sarah. Ghafla, Charity akasema, “Lisa, achana naye kama unaweza. Uko peke yako bila msaada. Nina wasiwasi huwezi kushindana na Sarah na mwishowe utapoteza kila kitu.”
Lisa alizama katika mawazo. Bila shaka, alikuwa amefikiria kuacha naye pia. Hata hivyo, moyo wake ulipata maumivu makali kila alipokuwa akifikiria kumtoa Alvin kwa mtu mwingine, au alipowaza taswira ya yeye na Sarah kuwa mke na mume. Kwanini amwache aende? Alikuwa mume wake. Baba wa watoto wake.
Charity alishusha pumzi akimtazama. “Vinginevyo, hutakiwi kumruhusu amtibu Alvin. Ni mchakato mrefu na itambidi kutumia muda mwingi akiwa na mpenzi wake huyo wa zamani. Sara hakika ataleta matatizo katika kila nafasi anayopata. Huenda usiweze kumshughulikia hasa kwa kuwa wewe ni mjamzito.”
Lisa alitabasamu kwa uchungu. Hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa yakienda. Kabla ya kuondoka, aligeuka na kumwambia Charity kwa huruma, “Hata iweje, siku zote, nitakuwa rafiki yako na hutawahi kuwa peke yako.”
Charity alishtuka na kufadhaika. Haikuelewa chochote mpaka Sarah alipoenda kumwona muda si mrefu baadaye ndipo hatimaye alielewa ukweli.
Alasiri, Lisa alishangaa kumkuta Alvin nyumbani baada ya kurudi kwa Mzee Kimaro. Alikuwa amekaa kwenye kochi sebuleni. Alitembea moja kwa moja hadi kwenye ngazi bila kumtazama.
"Lisa, subiri." Alvin alimkimbilia kumshika mkono. “Njoo tupumzike sebuleni, nimeleta mpishi maarufu atupikie chakula kizuri sana leo.”
Lisa alimtazama mwanaume huyo juu na chini kwa mashaka. "Huna hasira kwamba nilimsukuma Sarah asubuhi hii?"
Alvin alishtuka, akakuna pua. "Nilikuwa karibu kukasirika lakini nilipojifikiria mara mbili, nikajua mke wangu asingemsukuma mtu bila sababu."
Wakati huo huo, uvimbe ulijitengeneza kooni mwa Lisa na machozi yakaanza kumtoka papo hapo. Mungu pekee ndiye aliyejua jinsi alivyokasirika siku hiyo. Alikuwa amejipanga kugombana tena na Alvin lakini hakutarajia kwamba angemwamini safari hii.
Moyo wake uliokuwa umechoka ghafla ukapata nguvu ya kujiamini kuendelea na safari hii ya maisha pamoja naye.
“Haya, mbona unalia tena?” Alvin alishikwa na mshangao. "Machozi yako yamekuwa kama mvua tangu upate mimba na yanakuja bila kualikwa, kwanini?" Alipapasa huku na kule kutafuta kitambaa.
"Alvlisa." Lisa alimkumbatia na kuuzika uso wake kifuani mwake.
“Ndiyo, niko hapa.” Alvin akampigapiga Lisa kidogo mgongoni. Ilikuwa ni muda mrefu sana tangu alipomwita jina hilo. Kulikuwa na hisia mchanganyiko katika moyo wake. Labda hakuwa akimjali vya kutosha jambo ambalo lilimfanya awe na huzuni. “Lakini nilikuwa na hasira kidogo leo. Hukupaswa kuendesha gari kwa kasi hivyo leo. Je, wewe na watoto mkijeruhiwa?”

“Sitafanya hivyo tena.” Alitikisa kichwa. Baada ya kufikiria kwa ufupi, aliinua macho yake na kusema, “Kwa kweli, sikumsukuma kimakusudi leo. Sarah aliniambia kwenye kaburi la Aunty Jennifer limezikwa jeneza tupu. Maiti yake waliitelekeza mochwari na imezikwa na city kwenye makaburi yasiyojulikana. Sikuweza kuvumilia…”
Mshtuko mkubwa uliandikwa usoni mwa Alvin. Lisa hakushangaa kuona mwitikio wake huo. “Najua hutaniamini na pengine hata kufikiria kuwa nampakazia. Lakini haijalishi.”
“Ni vigumu sana kuamini hivyo,” Alvin alisema kwa uaminifu huku akiendelea kumbembeleza mgongoni. Asingemsamehe Sarah hata kidogo ikiwa angejua ni kweli alifanya hivyo. Hata kama Jennifer alikuwa mvunja nyumba ya mama yake, alikuwa tayari amekufa. Isingekuwa sawa kuitupa maiti yake kusikojulikana.
“Hmm, hata mimi sitaki kuamini hivyo pia. Natumai alikuwa anadanganya tu,” Lisa alijibu kwa uchovu.
“Sawa, acha kuwaza kupita kiasi. Nitamwambia Aunty Yasmine alete chakula." Akambeba mpaka bustanini.
Jua lilikuwa linawaka na kulikuwa na joto kiasi ndani ya bustani. Lisa aliegemeza kichwa chake kifuani mwa Alvin huku akimlisha chakula. Alichangamka baada ya hapo na kwa namna fulani akalala huku akiwa amejiegemeza kwenye mikono yake.
Baada ya kumbeba na kumrudisha chumbani, alitoka chumbani na kumuita Hans. "Nenda uchunguze indani ya kaburi la Jennifer kuna jeneza tupu."
“Itakuwa imeenda wapi tena maiti yake, imefufuka?" Hans alishangaa.

“Fanya hivyo mara moja!” Alvin alimfokea msaidizi wake.
Siku iliyofuata. Sarah alifika mapema nyumbani kwa Mzee Kimaro kumtibu Alvin. Lisa na Alvin walikuwa wakimsubiri pale sebuleni. Lisa alikuwa ameghairi makusudi kwenda ofisini siku hiyo.
Sarah alionekana mrembo akiwa amevalia vazi jepesi la majira ya joto la waridi na mikono iliyochanika. Macho yake bado yalionekana kuwa na kichefuchefu kidogo kutokana na kilio cha msibani, ambacho kilimfanya aonekane mwenye huzuni kiasi fulani.
Hata hivyo, Lisa alikuwa tayari ameona unyama uliojificha nyuma ya sura hiyo nzuri. Mwanamke huyo alikuwa muovu mara elfu zaidi ya Lina.
"Bibi mdogo." Dokezo la vitisho likaangaza machoni pa Sarah. Baada ya kupeana salamu za kawaida, alimgeukia Alvin.
"Wacha tuanze kipindi chetu cha pili cha matibabu."
Lisa alisimama na kuhoji. “Bibi Njau, unaweza kunieleza undani wa kipindi hiki cha pili? Ni aina gani ya njia ya matibabu inahitajika?"
"Tiba ya huzuni. Kwa maneno rahisi, inamfanya mgonjwa kudhibiti kwa makusudi msisimko, furaha, na kusahau wasiwasi wake katika mtazamo hasi, na hivyo kubadilisha hisia zake kuwa mtazamo chanya.”
Lisa alikunja uso kwa sauti hiyo. "Inaonekana kuwa hatari sana."
Tabasamu likatanda usoni mwa Sarah. “Uko sahihi. Lakini Alvin amekuwa mgonjwa kwa miaka 20 na hali yake haiwezi kuponywa ikiwa tutakwepa hatari. Isitoshe, kusema ukweli, akikataa matibabu, hali yake inaweza kuwa mbaya na kuwa sawa na ugonjwa wa Alzheimer katika muda wa chini ya mwaka mmoja.”
Uso wa Alvin ulianguka. “Kwanini hukusema hivi kabla?”
"Sikutaka kukuhangaisha au kukufanya uhisi kulemewa kupitia vipindi vya matibabu." Sarah alicheka kwa uchungu. “Sina jinsi zaidi ya kukuambia kwa sasa maana nahisi kama huniamini sana. Lazima nikueleze kwa uaminifu uzito wa hali hiyo.”

Sura ya: 288

“Twende ghorofani kwa matibabu,” Alvin alisema kabla ya kuelekea kwenye ngazi.
Lisa aliuma midomo yake alipoona watu wale wawili wakitoweka juu ya ngazi. Sarah bila shaka alikuwa mwanamke mjanja. Kwa maneno machache tu, alimfanya Lisa kuonekana hajali hali ya Alvin kwa sababu tu ya wivu wake.
Lisa alisubiri sebuleni muda wote tangu kipindi cha matibabu kianze. Dakika 40 hivi baadaye, sauti ya vitu vikivunjwa na sauti ya mwanamke akipiga kelele ghafla ikasikika kutoka juu. Alikimbilia kwenye chanzo cha mzozo huo mara moja, na kukuta chumba kilikuwa kimefungwa kwa ndani.
“Shangazi Yasmine, leta funguo haraka,” Lisa aliamuru.
Mlinzi wa nyumba alipanda ngazi kwa wasiwasi akiwa na funguo ya ziada. Wakati anakaribia kufungua mlango, mara ulifunguka wenyewe kutoka ndani. Alvin ambaye alikuwa amevalia suruali ndefu alionekana kufadhaika huku akitoka nje ya chumba kile kwa kasi akiwa amembeba Sarah mikononi mwake. Kichwa cha mwanamke huyo kilikuwa kinavuja damu na kulikuwa na kamba iliyozungushwa shingoni mwake.
"Nini kimetokea?" Lisa aliuliza kwa mshtuko.
Alvin alikuwa anataka kueleza kitu pale Sarah alipougulia maumivu ghafla.
“Usilie. Nitakupeleka hospitali sasa hivi.” Alvin alimfariji kwa upole. Bila hata kumwangalia Lisa, alitoka nje ya nyumba haraka huku Sarah akiwa bado amemkumbatia.
Jumba kubwa la kifahari liligeuka ghafla kuwa kimya. Lisa alihisi kutetemeka hadi kwenye uti wa mgongo wake.
Alitazama ndani ya chumba kilichovurugika. Meza na viti vilikuwa vimesambaratika huku na kule. Alikuwa amemwona Alvin hapo awali alipokuwa amerudiwa na ugonjwa wake. Huenda mbinu za matibabu ya Sarah zilimfanya arudiwe na hali yake tena na baada ya kupata fahamu zake aljikuta amemdhuru Sarah. Lisa alikuwa amemtahadharisha hapo awali kuwa mbinu hizo za kusisimua ugonjwa wake ni hatari lakini Sarah akasisitiza tu kuzitumia.
“Bibi Mdogo…” Shangazi Yasmine alimtazama kwa wasiwasi.
“Sijambo. Fuatilia kujua anapelekwa hospitali gani. Nitakwenda kumtembelea,” Lisa alisema.
Dakika 20 baadaye, aliambiwa kwamba walikuwa katika hospitali ya Chester. Shani alimkimbiza huko mara moja.
Lisa alisikia sauti nyororo ya Alvin ikimbembeleza Sarah mara baada ya kuukaribia mlango. "Unajisikiaje sasa?"
“Niko sawa. Ni mkwaruzo mdogo tu...”
“Mkwaruzo mdogo? Ninajua jinsi ninavyoweza kuwa mkali wakati wa kurudi ugonjwa tena. Kwanini hukuniambia mapema kwamba matibabu yanaweza kuwa hatari?”
“Haijalishi. Sijali kuumia kwangu hata kidogo ikiwa inamaanisha kuponya hali yako." Sarah alisema kwasauti nyororo.
“Sarah…”
“Sawa, huna haja ya kusema lolote. Sikustahili lakini natumai unaweza kuwa na maisha ya kawaida. Kusoma saikolojia halikuwa lengo langu lakini wewe ndiye uliyenipa motisha iliyonifanya niendelee mbele. Tafadhali niruhusu nitibu ugonjwa wako. Nataka uwe na maisha ya kawaida yenye furaha.”
“Samahani… Sarah…” Sauti nzito ya mwanamume huyo ilijawa na majuto na kufadhaika.
Lisa hakuweza kusikia neno lingine. Alikuwa karibu kuusukuma mlango ili aingie ndani wakati mkono ulipomvuta ghafla. Alitazama begani na kukutana na sura isiyojali ya Rodney ikimtazama. “Hebu tuzungumze.”
Rodney akampeleka kwenye korido tulivu na kuwasha sigara kabla ya kukaa kwenye ngazi. Moshi uliotoka kwenye midomo yake ulionyesha upweke machoni pake.
“Ikiwa lengo lako nikuniambia nimwachie nafasi yangu Sarah, basi samahani, lakini sitakubali hilo," Lisa alisema kwa upole.
"Lazima utakuwa umefikiria na kugundua hilo pia. Sarah hajaacha kumpenda Alvin na bado anamjali,” Rodney alijibu huku akionekana kuudhika. "Lakini mambo yamefikia hivi kwa sababu yako."
Lisa alicheka kwa kejeli. “Kwanini Sarah hakurudi nyumbani mapema ikiwa hakuwa amekufa? Kwani kosa langu ni lipi hapo? Yeye alikuwa amekufa na Alvin akaamua kunioa. Angekuwa anataka kuolewa naye si angemfahamisha mapema kuwa bado yupo hai amsubiri? Kwanini alimua kukaa kimya, alifikiri Alvin angemngoja milele?”
"Siyo kwamba hakutaka kurudi nyumbani lakini alihisi kuwa hastahili kuwa Alvin tena. Ni kwa sababu yeye…” Macho ya Rodney yakamtoka. "Hujui amepitia nini."
"Sijui na sina mpango." Midomo yake ilitetemeka.

"Lisa, unawezaje kuwa na moyo mgumu kiasi hiki?" Rodney alichukia. “Sarah alianza kabla yako. Kimsingi wewe huna haki ya kuwa na Alvin baada ya Sarah kurudi.”
Lisa alihisi kama hana la kusema. “Najua unampenda Sarah lakini tafadhali usitumie hilo kuwaumiza wengine. Unataka nimuonee huruma? Kweli, lakini vipi kuhusu ndoa yangu na watoto wangu? Nani atanihurumia?”
"Unajua jinsi walivyokutana?" Akavuta pumzi ndefu ya sigara. “Alvin alikutana na Sarah alipopelekwa katika hospitali ya magonjwa ya akili. Sarah hakuwa mgonjwa lakini alipelekwa huko na familia ya Njau. Sarah alimjali sana Alvin kama rafiki yake, hatua kwa hatua hali yake ilibadilika kuwa bora na chanya. Alikuwa kama mwanga wa jua wakati wa siku za giza. Pia ni kwa sababu yake nilimfahamu Sarah. Yeye ni mtu mzuri sana. Ingawa walikuwa hawasomi katika shule moja, alimwandikia barua za kumtia moyo kila siku kuanzia shule ya msingi hadi walipokua na kufaulu maishani. Amefahamiana naye kwa miaka 20. Sawa, umeolewa na Alvin lakini ni baada ya kufikiria kuwa Sarah amekufa. Alvin ni mwanamume anayewajibika, lakini sasa umemweka njia panda. Wewe ni mjamzito, lakini bado anamuona Sarah kama mke wa maisha yake. Unafikiri ni vizuri kuwa katikati yao?”
Kila neno lililotoka kinywani mwa Rodney lilipenya moyoni mwa Lisa kama kisu kikali. Hakujua kuwa wawili hao walikuwa wamekutana katika hospitali ya magonjwa ya akili.
“Sarah alisomea saikolojia kwa sababu ya Alvin. Anajitolea maisha yake yote kwake, "Rodney alisema kwa upole. "Kwa nini huwezi kuwapa baraka zako?"
Lisa alicheka kwa kejeli. "Ni nani atakayenipa mimi na watoto wangu baraka basi?" Aligeuka kuusukuma mlango mzito wa mbao. “Rodney, huwezi kunifanya nionekane sina haki kwa sababu tu unampenda Sarah. Kwanini wewe ndiye unajitia kimbelembele sana kumpigania Sarah? Sijamwona Chester akifanya hivyo, hata Alvin mwenyewe hapambani kama wewe. Wewe una nini hasa na Sarah? Amekupa nini?”
Badala ya kurudi kwenye wodi ya hospitali, aliamua kuondoka kabisa hospitalini. Alitembea kando ya barabara kwa muda mrefu bila mpango wowote.
Alvin alimpigia akiwa ametembea hadi miguu imeanza kumuuma. "Shani alisema ulikuja hospitalini. Uko wapi? Mbona sikuoni?”
“Niliondoka,” Lisa alijibu kwa upole, "Utarudi lini nyumbani?"
“Lisa, samahani. Sarah amejeruhiwa kwa sababu yangu na Thomas hayupo. Ninaweza kukaa kwa muda mrefu zaidi…”
“Ndiyo, ni sawa.” Lisa alikata simu na kuelekea nyumbani kwa Pamela.
Alimkuta Pamela akiwa anapakia vitu vyake. “Unaondoka lini?”
"Aamh! Mwezi ujao. Naenda Marekani lakini bado sijapata visa. Ninapanga kurudisha vitu hivi vyote Dar es Salaam.” Pamela aliutazama uso wa rafiki yake uliopauka kwa wasiwasi. "Kuna nini?"
“Hakuna kitu, nimechoka tu.” Lisa alimkumbatia rafiki yake huku machozi yakimtiririka bila kujizuia. “Hatimaye unaondoka! Ninaogopa siwezi kuvumilia kwa muda mrefu zaidi. Inaonekana kama kila mtu katika jiji hili ananiona kama adui. ”
“Ikiwa…nitakaa?” Pamela aliuliza na kuuma mdomo.
“Hapana, sahau. Huwezi kunisaidia hata ukikaa.” Lisa alifuta machozi yake kwa nyuma ya mikono yake. “Ni kwamba mengi yametokea hivi karibuni. Sarah ameanza kufanya harakati zake. Alvin anasema hatarudiana naye lakini najua bado anamjali.”
Pamela alishusha pumzi baada ya kumwona yule mwanamke aliyekuwa akihangaika. “Lisa, najua unajaribu kuokoa ndoa yako kwa sababu ya watoto lakini inaonekana juhudi ni za upande mmoja. Itakuchosha. Kwa nini usipumzike tu?”
“Pamela…”.....ITAENDELEA.....

Unafikiri nini kitafuata hapo, maana simulizi inazidi kuwa tamu kila siku lakini sina budi kuhitimisha kipande hiki ila niwasihi tukutane katika episode zijazo ili kujua nini kitafuata kwenye mkasa huu wa kusisimua na kuelimisha unaokwenda kwa jina la LISA.